MAJANGA! : Mastaa twanga wanusirika kifo

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Mbutu, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari lililokuwa likitokea Coca-Cola, kutoheshimu taa za barabarani na kwenda kuwagonga wakati wakisubiri kuruhusiwa na taa hizo.

TASNIA ya burudani imepata janga lingine. Ikiwa zimepita siku sita tu baada ya ajali ya gari iliyochukua uhai wa wanamuziki wawili wa bendi ya Mapacha Watatu na wengine kujeruhiwa, jana alfajiri wasanii wengine wa bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ wakiongozwa na Luiza Mbutu wamenusurika kifo katika ajali ya gari.

Ajali hiyo ilitokea makutano ya Barabara ya Sam Nujoma na Ali Hassan Mwinyi eneo la Mwenge na kuwahusisha Mbutu, Super Nyamwela, Jojoo Jumanne, Lualua na Hilary ambaye ndiye alikuwa dereva wa gari hilo wakirejea nyumbani kutoka Ukumbi wa Jonz Pub walipokuwa na shoo ya bendi hiyo.

Kwa mujibu wa Mbutu, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari lililokuwa likitokea Coca-Cola, kutoheshimu taa za barabarani na kwenda kuwagonga wakati wakisubiri kuruhusiwa na taa hizo.

Gari waliokuwa wakitumia wasanii hao lilipunduka, lakini hakuna kifo zaidi ya kupata michubuko huku dereva wa gari lililofanya tukio hilo akikimbia na kudondosha kibao cha namba za usajili.

Luiza, ambaye amepata majeraha sehemu mbalimbali za mwili, alisema; “Nashukuru Mungu, tumenusurika katika ajali, maana ilikuwa ni mbaya sana, yaani wakati tunasubiri taa zituruhusu pale Mwenge mataa, tukaona gari limetokea Barabara ya CocaCola na kuja kutugonga na kukimbia.

“Hata hivyo Mungu ni mkubwa, wakati gari hilo linakimbia, lilidondosha pleti namba na tunayo,” alisema. Mara baada ya ajali hiyo, wakati wanamuziki hao wakiendelea kujiokoa baadhi waliwapigia simu wenzao kuwajulisha juu ya tukio hilo ambao ni Kalala Junior, Godfrey Kanuti, Chiku, Maria Saloma na mume wa Luiza pamoja na mkurugenzi wa bendi hiyo, Asha Baraka. Hata hivyo, kabla hawajafika wanamuziki hao walikuwa wameshawahishwa katika Hospitali ya Palestina iliyopo Sinza.

Mwanaspoti pia lilifika katika Hospitali ya Palestina saa 10 alfajiri na kuwakuta wanamuziki hao wakipatiwa matibabu, huku kwa upande wa Nyamwela akisema ameumia mguuni na kwenye paji la uso na maumivu kwenye eneo hilo, lakini anashukuru Mungu.

“Nashukuru Mungu sijaumia sana japo nina maumivu makali kwenye paji la uso. Pia, nimeumia mguu wa kushoto lakini nimepatiwa matibabu najisikia kidogo afadhali. Ni ajali mbaya ila tunashukuru hakuna aliyepoteza maisha,” alisema Nyamwela.

Hata hivyo, Jojoo Jumanne alitoka salama bila hata ya mikwaruzo ya aina yoyote, pia naye alisema ajali iliyotokea ni kumshukuru Mungu sana.