Lulu Diva, Belle 9, Bonge la Nyau wahamishiwa Muhimbili

Monday September 7 2020

 

By NASRA ABDALLAH

Wasanii wa Bongo Fleva Lulu Diva, Belle 9 na Bonge la Nyau waliopata ajali wakiwa wanatokea mkoani Iringa wamehamishiwa Hospitaliti ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam kwa matibabu zaidi kutoka kituo cha Afya Chalinze.

Wasanii hao walipata ajali leo Jumatatu Septemba 7, 2020 saa kumi alfajiri maeneo ya Mwidu, Chalinze mkoani Pwani wakiwa wametokea mkoani Iringa kuelekea Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Mkoani humo, Wankyo Nyigesa amethibitisha ajali hiyo na kusema gari waliyokuwa wanasafiria aina ya Toyota IST iliacha njia na kupinduka kwenye korongo.

“Majeruhi wote wamepata michubuko na majeraha madogo madogo miilini na wote wamelazwa na wanaendelea na matibabu katika kituo cha Afya Chalinze” amesema Nyigesa

Akizungumza na Mwanaspoti muda mchache baada ya kufikishwa Muhimbili, Bonge la Nyau amesema walipata ajali hiyo baada ya dereva wa gari aina ya IST walilokuwa wamepanda kulikwepa lori lililokuwa linakuja mbele yao.

"Wakati tukiwa maeneo hayo ya Mwidu, ghafla mbele tuliona lori likiwa linataka kulipita lori lingine na kukutana uso kwa uso na gari letu”

Advertisement

"Hivyo dereva njia pekee aliyoiona ni kulipeleka gari pembeni lakini kutokana na wembamba wa barabara tulijikuta tukidumbikia bondeni," amesema Bonge la Nyau

Hata hivyo amesema anashukuru waliweza kupata msaada kutoka kwa wasamaria wema wa lori jingine la mafuta likipita eneo hilo, ambapo waliwatoa bondeni na kuwaweka barabarani.

Muda mfupi baadaye, amesema walitumiwa gari na mgombea Ubunge wa Kilolo aliyemtaja kwa jina moja la Justine ambaye alikuwa mwenyeji wao walipokuwa mkoani Iringa kwenye kampeni za CCM na kuwafikisha katika hospitali ya Chalinze kabla ya mchana kuhamishiwa Muhimbili.

Kwa upande wake Belle 9 ambaye katika ajali hiyo alipoteza fahamu, amesema kwa sasa anashukuru anaendelea vizuri, isipokuwa anasikia maumivu makali maeneo ya mgongoni.

Lulu Diva ambaye hakuweza kuongea, Mwanaspoti ilimshuhidia hospitalini hapo akiwa analalamika maumivu ya kichwa.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma MNH, Aminiel Aligaesha amesema waliwapokea wasanii hao saa 8:30 mchana na bado wanaendelea kuchukuliwa vipimo zaidi.

Aligaesha amewaondoa wasiwasi mashabiki zao kwamba wasanii hao wote wanaendelea vizuri.

Advertisement