Lulu Afunguka ishu ya Kiba, Diamond

PICHA za ‘mapouda’ za msanii wa Bongo Movie, Elizabeth Michael ‘Lulu’ zinazoonekana katika mitandao ya kijamii kama Instagram na mingine kumbe zina siri kubwa nyuma yake.

Mrembo huyo mwenye sura na umbo ya kupendeza na unaweza kushangaa utakaposikia kuwa hajui kabisa kujiremba yaani kwake sio dili kabisa.

Lulu ambaye picha zake mitandaoni zimekuwa kivutio kutokana na urembo hasa mapambo anayokuwa amejiremba, lakini yote hayo hufanywa na wataalamu wengine kabisa.

“Bora niweke wazi, suala la kujiremba sijui kabisa. Ninachojua ni kupaka mafuta na mambo mengine, lakini kukaa kwenye kioo na kufanya kazi hiyo si mtaalamu, ukiona nimepambwa na kupendeza huwa nakwenda saluni,” anasema Lulu ambaye ni mchumba na mke mtarajiwa wa Francis Ciza ‘Majizzo’.

Amefafanua huwa anafanya hivyo, anapokuwa anakwenda kwenye mitoko maalumu na mambo yake kikazi.

RATIBA YAKE KWA SIKU

Lulu, ambaye kwa mujibu wa mtandao amezaliwa Aprili 16, 1995 sasa ana miaka 23, anasema ratiba yake kila siku huwa inaanza kwa sala.

“Ninapoamka kitu cha kwanza nasali baada ya hapo nafanya mazoezi kisha nakunywa chai baada ya hapo naendelea na shughuli nyingine,” anasema Lulu, ambaye baada ya kutoka gerezani alikokuwa amehukumiwa kifungo kutokana na kifo cha msanii mwenzake, Steven Kanumba amekuwa nyumbani tu.

“Kwa sasa sijaanza kutumia muda wangu mwingi kwa ajili ya kazi, zaidi ni mizungungo ya hapa na pale, hivyo mara nyingi nakuwa nyumbani tu.”

UZITO WAKE BAADA YA JELA

Akiwa gerezani wakati akitumikia kifungo, mwili wa Lulu uliongezeka hadi kufikia kilo 70, lakini sasa ana kiko 59 tu baada ya kupunguza kilo 11.

“Niliamua kupungua kwa kufanya mazoezi tu kwa sababu nilitaka niwe hivyo. Kila kitu ni maamuzi ndiyo maana nikafanikiwa,” anasema Lulu.

“Unajua unapoamua kuchukulia matukio magumu kuwa kawaida ni mipango ya Mungu unaacha tu.

“Lakini ukisema ubishane nayo na kusema haiwezekani au kwa nini kujinyima amani kwa sababu unabaki na kitu moyoni ambacho ndicho kitakachokutesa wakati wote,” alisema Lulu anayeweka wazi kuwa anachoamini matukio yote anayopitia katika maisha yake ni daraja linalomvusha kutoka hatua moja kwenda nyingine.

KWA KICHUYA HUYU

Lulu, ambaye ameweka wazi kuwa yeye ni shabiki mkubwa wa Simba licha ya kuwa si mfuatiliaji mzuri wa soka, anasema anamjua Shiza Kichuya.

“Nampenda Kichuya kwa sababu ndiye namsikia anafungafunga sana mabao,” anasema Lulu huku akishikwa na mshangao baada ya kuambiwa kuwa si mchezaji wa Simba tena, baada ya kusajiliwa na Klabu ya Ligi Daraja la Kwanza ya Misri ya Pharco, lakini amejiunga na kuichezea kwa mkopo ENPPI inayocheza Ligi Kuu ya nchi hiyo.

Kwa upande wa Ulaya, Lulu amekuwa akifuata soka la England, ambapo alianza kuwa shabiki wa Chelsea na sasa mapenzi yake yote yapo kwa wababe wa Old Trafford pale Manchester United.

“Mara nyingi sana huwa nakwenda tofauti na wenzangu. Mfano nikikuta marafiki zangu wakiangalia mpira nawauliza nyinyi ni timu gani, wanayonitajia nakuwa ile wanayoshindana nayo kwa sababu ya ushabiki tu,” anaeleza Lulu aliyeweka wazi kuwa aliipenda Simba kwa sababu ya mama yake mzazi, Lucresia Karugila ambaye ni shabiki wa klabu hiyo.

AGOMA KUWA MWANASIASA

“Zamani nilikuwa napenda siasa lakini sasa niko tofauti. Wakati nasoma nilikuwa napenda mambo ya midahalo na nilikuwa na nguvu ya kuongea na kubishana katika mambo tofauti hasa siasa, lakini kwa sasa sipendi,” anasema Lulu.

Anasema hakuwa na mipango yoyote ya kuja kugombea kwenye siasa na alipoambiwa kama ikitokea Rais Dk John Magufuli atamteua kuwa kiongozi ni kitu gani atachukua, akafunguka haya:

“Unajua mambo mengine maamuzi huwa yanafanyika pale tu tukio linapotokea. Nikichaguliwa nitajua cha kufanya kwa wakati huo,” anasema Lulu.

BAADA YA KUTOKA JELA

Kutokana na imani aliyonayo na Mungu wake, Lulu anasema kitu cha kwanza alichofanya mara baada ya kutoka gerezani ilikuwa sala.

“Nilifika nyumbani na moja kwa moja nilikwenda kusali kwa sababu niliamini kila kitu kilikuwa ni kwa ajili ya Mungu. Kwanza sikutegemea kama jambo lile la kuachiwa kwa wakati ule lingeweza kutokea,” anasema Lulu.

ISHU YA ALI KIBA, DIAMOND

Kuhusu ishu ya Ali Kiba na Abdul Naseeb ‘Diamond’ Lulu anasema hataki kuamini kama bifu ndiyo linachangia mafanikio katika maisha, lakini umoja ndiyo jambo muhimu zaidi.

“Unapowaza kumshusha mtu nafasi alipo ili ufanikiwe wewe sio jambo sahihi, lakini umoja ndiyo kitu muhimu zaidi.

“Wawili hao kama wataamua kuungana wakafanya mambo yao pamoja watanyanyuka na kufika mbali zaidi na si hao tu, wawabebe na wengine zaidi,” anasema Lulu na kuongeza.

“Tuige mfano wa Wanigeria, jamaa wale wana umoja na wanafanikiwa kwa sababu hiyo lakini, sisi tumebaki na kina Ali Kiba na Diamond tu wakati kuna wasanii wengi tu.”

SIKIA HII YA STEVE NYERERE

Lulu anamtaja Steve Nyerere kama baba, rafiki na mtu wake wa karibu, na hakubaliani na tuhuma ambazo anapewa na watu kutokana na kuwa mstari wa mbele katika misiba tofauti.

“Unajua wanapoongea mambo yao huwa ni hulka tu hivyo, huwezi kuwazuia na kama hauko hivyo, kamwe maneno hayo hayawezi kukuumiza. Steve Nyerere ni mtu tofauti sana na ni nguzo katika sanaa ya Tanzania kwa sababu amesaidia mambo mengi sana na ni mtu wa watu.”