Kumbe tatizo ni mameneja

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti, Jimmy ameyataja baadhi ya mambo hayo ni mameneja kuwa sio watu sahihi katika kuendeleza muziki kwa aslimia kubwa, kwa sababu hawajui mipango wala masoko, wala kutumia mitandao ya kijamii na hata jinsi ya kuuza nyimbo kwa njia ya mitandaoni.

MWANAMUZIKI wa Mapacha Music Band, Jimmy Golla ambaye kwa sasa anatamba na wimbo wake wa ‘Mazoea’ amesema yapo mambo machache tu kwa sasa yanayowaangusha na kuonekana muziki kushuka.

Akizungumza na Mwanaspoti, Jimmy ameyataja baadhi ya mambo hayo ni mameneja kuwa sio watu sahihi katika kuendeleza muziki kwa aslimia kubwa, kwa sababu hawajui mipango wala masoko, wala kutumia mitandao ya kijamii na hata jinsi ya kuuza nyimbo kwa njia ya mitandaoni.

“Wala siwezi kupindisha kuhusiana na baadhi ya mambo yanayosababisha kuangusha muziki wetu wa dansi, kwa sasa ni mameneja ambao wanaofanya kazi asilimia kubwa sio watu sahihi kwa sababu utakuta meneja hajui mipango ya kazi zake ili kuendeleza bendi.

“Yaani hapa hata sijui bendi ngapi zina akaunti ya Instagram, YouTube, na Facebook ni za kuhesabu, lakini Tanzania ina bendi ngapi ambazo zina akaunti hizo? Ni ngumu kujua hilo kwa kweli.

Gola alisema umefika wakati bendi ziangalie ni nani zinataka kufanya naye kazi na vigezo na uwelewa na sio elimu wala kujulikana, kwani mambo yamebadilika. Amesisitiza dunia hii sio ya mtu kukufuata na kukupa dili mkononi.

Gola aliwahi kutamba na Wimbo wa ‘Nalingiyo’ alisema siku akibahatika kupata meneja wa kusimamia kazi zake, atataka kuwa na mtu mwenye uelewa wa mambo.

“Sitaki kupata meneja ambaye atakuja kuninyonya na kuleta majungu kwangu zaidi ya uelewa na uwezo, nataka mtu wa kufanya kazi,” alisema.