Kumbe Sinta alimpa ulaji Kakere buana!

Muktasari:

  • Kakere anasema wimbo huo ulimpatia umaarufu kwa wadau wa muziki wa dansi na watu wengine na wala hakutarajia kama ungepokelewa kwa staili hiyo.

WAPENZI wa muziki wa dansi wanaukumbuka sana wimbo wa ‘Pole kwa Safari’ wa Juma Kakere ulivyobamba na hasa video yake iliyonakishiwa na staa wa zamani wa Kaole Sanaa, Christina Manongi a.k.a Sintah.

Sintah aliyewahi kuimbwa na Sir Juma Nature ‘Kibla’ aliitendea haki video hiyo akiingiza kama mpenzi wa Kakere anayempokea mtu wake toka safari na kuwavutia wengi, huku ukikimbiza kwenye vituo vya runinga.

Wimbo huo hadi leo bado unambamba vilivyo masikioni mwa mashabiki wa miondoko hiyo, ulimpa jina kubwa Kakere na juzikati Mwanaspoti lilipata nafasi ya kupiga naye stori mbili tatu na kufunguka mengi ikiwamo kukiri video hiyo ya Sintah ilivyompa ulaji ndani na nje ya nchi.

Kakere anasema wimbo huo ulimpatia umaarufu kwa wadau wa muziki wa dansi na watu wengine na wala hakutarajia kama ungepokelewa kwa staili hiyo.

“Kwanza nashukuru kwa kuniuliza hili swali, ambalo sikuwahi kulielezea kwa wadau wa muziki wa dansi, Pole kwa Safari ni wimbo uliyoniongezea umaarufu kwa wapenzi na wadau wa muziki na burudani, video yake ilipendwa sana ilinisaidia kupata shoo nyingi mno,” anasema Kakere.

Hata hivyo, Kakere hakuweza kuweka bayana kiasi cha fedha alichoingiza kupitia wimbo huo, lakini anakiri anajivunia nao na huku akimtaja Sintah na mvuto wake ulichangia kuupa mafanikio, licha ya ujumbe mzuri uliopo katika ngoma hiyo iliyotoka mwanzoni mwaka 2000.

Kulikuwa na taarifa Kakere ameachana na fani ya muziki, lakini amesisitiza kuwa bado yupo sana na bado hajakaa kimya kama inavyofikiriwa na kwa sasa anamiliki vyombo vyake vya muziki na huwa akiwa na kazi ya shoo anawakusanya baadhi ya wanamuziki wanapiga kazi.

“Sijaacha muziki, naendelea kuimba na kutoa kazi kama kawaida, tena kwa sasa namiliki vyombo vyangu vya muziki na napiga kazi kama kawaida,” anasema na kuongeza mbali na Pole kwa Safari na Betty ambazo ndio nyimbo maarufu zilizowahi kubeba pia albamu zenye majina hayo, lakini pia alishatoa Watu Fulani na Kimbembe ambazo hata hivyo, hazikubamba sana.

“Baada ya hizo nilitulia na kuangusha moja moja na mwaka jana tu nimefyatua Happy na Kaa la Moto ambazo ziko YouTube. Muda wowote kuanzia sasa nitaachia wimbo mwingine kwa jina Imbe,” anasema mkongwe huyo.

Mkali huyo anafichua utunzi wa nyimbo alianza mwishoni mwa miaka ya 1970 akishirikiana na kaka yake Belesa Kakere aliyetamba na bendi za Dar International, (Vijana Jazz, hakukaa sana), Juwata Jazz (Msondo Ngoma) na Bima Lee na ndiye aliyemtia moyo baada ya kusikia tungo zake.

“Kitu ambacho wadau wengi wa muziki wa dansi hawakifahmu ni kuwa mimi ni utunzi nilianza 1978-79.
Belesa ni mkubwa sana, ndiye chachu kubwa iliyonifanya kuendelea kutunga kwani yeye ndiye mtu wa kwanza kusikia tungo zangu na kwa jinsi alivyoshangaa uwezo wangu na kunitia moyo ndivyo nilivyozidi kuendelea katika utunzi.”

Kuhusu dansi kudoda na kipi kifanyike, Kakere anasema; “Hali ya muziki wa dansi si nzuri kwa sasa na inahitajika juhudi kubwa za wadau wote wa dansi kwa pamoja. Mazingira ni tofauti na ya zamani, mtazamo wa kibiashara ya muziki miongoni mwetu wanamuziki na wafanyabiashara ya muziki (burudani) na wamiliki wa vyombo vya habari.

“Hivyo inahitajika wanamuziki tutambue hilo na kufanya ambavyo soko linataka. Nyimbo bora katika mifumo ya kiteknologia ya kisasa, kufanya kama biashara nyingine katika kanuni za matangazo, brandi na kutumia ipasavyo mitandao ya kijamii. Lakini iambatane na kusikika na kuonekana nyimbo zetu bila kubaguliwa.”

Alipoulizwa kama vyombo vya habari vinachangia kuuangusha muziki huo, anasema; “Sina hakika, ila kungekuwa na TV na Redio zenye kurusha muziki wa dansi muda wote, wafanyabiashara na wadhamini wa kuandaa matamasha mengi ya dansi ni wazi hali isingekuwa hii ya sasa.”

Juu ya tetesi kwamba alikuwa akimtungia nyimbo kaka yake, Kagere anasema;

“Sikuwahi kumtungia nyimbo kaka yangu Belesa, yeye ni hodari zaidi ila aliniongezea chachu kwa kuzireko di baadhi ya nyimbo wakati mimi nikiwa bado masomoni (sekondari). Nyimbo kama Asia, Baby Wangu, Chande, Remmy, Ombi na nyingine nyingi akiwa na Orchestra Bima Lee.
Yeye ndiye muhuri wa kwanza wa jina la Kakere katika muziki wa dansi Tanzania.”

Mpaka sasa Kakere amepakua albamu tatu za Betty, Remmy na Pole kwa Safari, kila moja ikiwa na nyimbo sita na baadhi yake ni Catherine, Ndoa ya Lazima, Mtoto Mridhawa, Mimi Mwanamuziki na Mambo ya Kiswahili.

“Hii ni album ya Betty niliyoitoa mwaka 2000, ile ya Pole kwa Safari ni ya 2004 ikiwa na nyimbo kama Mama Monica, Queen Misifa, Fadhili ya Punda, Remmy na Mary.
Nyimbo zote kwenye albumu hizi mbili nilizitunga miaka mingi zaidi ya 10 nyuma,” anasema.