Kingwendu awashtua wenzake

Muktasari:

Kingwendu a.k.a Mzee wa helohelo, kabla ya kugeukia filamu za vichekecho alijijengea jina kubwa kupitia vikundi mbalimbali vya sanaa ya maigizo ikiwamo Kaole Sanaa.   

MCHEKESHAJI maarufu na mkongwe nchini, Rashid Mwinshehe 'Kingwendu' ameiangalia fursa kupitia ugonjwa wa corona na kuwataka wasanii wenzake kujuipambania kwa kufanya kazi zaidi kuliko kipindi hali na mfumo wa maisha ulikuwa wa kawaida.
Kingwendu amesema licha ya ugonjwa huo kugusa kila binadamu na kutikisa mambo mengi, lakini anaona bado kuna haja wasanii kuishi uhalisia wa maisha yao na kuchangamkia kazi kisanii.
"Ugonjwa huu ni mzito, kwanza umeacha somo la usafi na la pili upande wetu kuacha maisha ya maigizo, hivyo kila mmoja apige kazi zaidi ili kwenda sawa na hali ilivyo," amesema.
"Ujue kuna kazi na maisha, wasanii wengi wanafeki hilo linakuwa linapunguza wao kujituma kwa bidii ili kufikia wanachokiishi kwa sasa, lakini kama mtu anayejielewa hiki ndicho kipindi cha kupiga kazi kwelikweli ili maisha yasonge," amesema.
Kingwendu amesema nje na kutoa somo kwa Watanzania na binadamu wote pia anaona ni wakati wa kumrudia Mungu kwani maradhi haya ni kama mtihani kwa waliomsahau Muumba.
"Kama ni jambo lililoyumbisha Dunia kuna haja ya kumrudia Mungu ili ashushe rahema zake, wakatri mwingine Mungu huleta mitihani kwa waja wake pale wanapojisahau," amesema.