King Kiki avunja ukimya

Thursday October 01 2020
king kiki pic

MKE wa mwimbaji mkongwe wa dansi nchini, Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ amewaomba Watanzania waendelee kumuombea mumewe ili afya yake itengemae, huku mwanamuziki huyo akivunja ukimya kwa kutamka maneno machache yenye ujumbe mzito.

Mtunzi na mwimbaji huyo wa zamani wa Marquiz du Zaire na Orchestra Double O anayemiliki kwa sasa Le Capital ‘Kitambaa Cheupe’ aliyefanyiwa upasuaji mkubwa wa pingili za shingoni, amezungumza kwa mara ya kwanza tangu upasuaji huyo na kuhimiza amani na upendo.

Jana, akizungumza na Mwanaspoti nyumbani kwake kwa sauti dhaifu, King Kiki alisema amefurahi kupata ugeni wa Mwananchi Communications Ltd na kutoa wasia akitaka watu waishi kwa amani na upendo.

“Ni vizuri tukaishi kwa upendo na amani, Watanzania waniombee ili nirejee kwenye afya yangu, asante na Mungu awatangulie mnapoondoka,” alisema King Kiki.

Awali, mkewe Costansia Kalanda alisema hali ya mumewe bado haijatengemaa kwa kuwa hajaanza kutembea na kuongea kama awali na kufichua tatizo lililochangiwa na kusumbuliwa na pingili za mgongo zilizoathiri zile za shingo kusagika na kufanyiwa upasuaji, huku akitiwa moyo kuwa ataimarika taratibu kabla ya kurejea katika hali ya kawaida. “Nilianza kuona dalili takribani mwaka mmoja hivi, kwani alikuwa amebadilika kutembea, nikawa nachukulia labda uzee, kama wiki tatu hivi ndio akaanza kuumwa nikampeleka hospitali,” alisema mkewe maarufu kama Mama Kitambaa Cheupe.

Advertisement