Kenny: Video ya wimbo ‘Gere’ ni makubaliano

Muktasari:

Mwongozaji aliyetengeneza video ya ‘Gere’, Kenny amekanusha  kuiga video ya wimbo ‘Brisa’ wa msanii wa nchini Brazili,  Isabel Cristian Correia jina la jukwaani Iza kama inavyodaiwa na watu kwa kueleza kuwa yalikuwa ni makubaliano halali.

BAADA ya kusambaa picha kwenye mitandao ya kijamii, zikionyesha namna vipande vya video ya wimbo wa ‘Gere’ vikiwa vimeigwa kwenye wimbo wa ‘Brisa’ wa msanii kutoka nchini Brazil aitwaye  Iza, mwongozaji wa video hiyo amekanusha uvumi huo.
 
Gere ni wimbo wa Tanasha Donna alioimba kwa kushirikiana na mpenzi wake Diamond Platnumz, ambapo tangu ulipoachiwa  Jumatano Februari 19,2020, umekuwa gumzo huku wafuatiliaji wa muziki wakiweka picha mitandaoni zinazoonyesha mwimbaji Iza, akimshutumu Diamond kuiga kama ilivyo video ya wimbo ‘Brisa’, tofauti na makubaliano yao.

Iza alitoa shutuma kuwa msanii huyo aliomba kutumia wazo la video yake, lakini alichofanya ni kama kahamisha wazo zima.

Kipande kinacholalamikiwa kuibwa kutoka kwa Iza, ni kile kinachoonekana mfano wa nyumba kikiwa na dirisha na mlango huku juu kikiwa kimewekwa makuti.

Vile vile kimepambwa kwa rangi za kijani, nyekundu, njano  na kuwekwa madafu na maua, ambapo kuna sehemu Diamond ameonekana kukaa nje kwenye kiti katika kibanda hicho na wakati mwingine kucheza mbele yake.

Pia kibanda kingine chenye rangi za aina hiyo kina ngazi ambapo Tanasha , Diamond na wacheza shoo wake wanaonekana  wakiimba na kucheza mbele yake huku wengine wakiwa juu.

Ukitizama video ya wimbo  ‘Brisa’  wa Isabela Cristina Correia de Lima Lima maarufu Iza, inaonekana ikiwa na vibanda kama hivyo, vikiwa vimenakshiwa sawa huku mavazi aliyovaa Tanasha yakifanana pia na aliyovaa msanii huyo.

Meneja wa Diamond, Babu Tale alipoulizwa kuhusu sakata hilo amesema kuwa akiulizwa yeye anaonewa kwa sababu siyo mtayarishaji wa video hiyo. “Muulizeni mwongozaji aliyesimamia utayarishaji wa video hiyo," amejibu kwa kifupi

“Hakuna kilichofanyika tofauti, hayo yalikuwa ni makubaliano kati yetu na Iza, msanii kama Diamond hawezi kutumia wazo la mtu bila kumpa taarifa na si jambo la ajabu katika sanaa linafanyika sana, ”amesema Kenny ambaye ni mwongozaji wa video hiyo na mwaka jana alitwaa tuzo ya mwongozaji bora wa video kwenye tuzo za All Africa Music (Afrima).