Kapo zilizobamba Bongo

TASNIA ya burudani nchini imebarikiwa kuwa na watu wa nguvu kweli kweli. Kama hujui, nguvu hiyo hunogeshwa au huwa maradufu pindi wanapokuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na mastaa wenzao. Iwe staa wa Bongo Muvi kwa wa Bongo Flava au kinyume chake.

Tangu mwaka huu uanze na sasa ukikaribia mwishoni, kuliibuka kapo nyingi sana za mastaa wa Kibongo. Baadhi yao zilibamba kinoma na kuteka hisia za mashabiki kuanzia kwenye mitandao ya kijamii hadi katika maisha ya kawaida.

Hapa Mwanaspoti linakuletea orodha ya kapo za mastaa wa Bongo zenye nguvu zaidi na zilizobamba na nguvu zao zipo kwenye lundo la mashabiki walionao, ushawishi wao, utajiri wao na wafuasi walionao kwenye mitandao ya kijamii.

Majizzo na Lulu

Ilianza kama utani. Ni tukio moja kubwa lililowakutanisha. Ilikuwa ni kwenye tuzo za Africa Magic zilizofanyika jijini Lagos, Nigeria. Majizzo alimpa kampani mwigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’ kwenye tuzo hizo na Lulu kuibuka kidede. Ilikuwa ni kama Majizzo amekwenda huko na bahati yake.

Baada ya hapo, safari ya uhusiano wao ikaanza na hadi sasa wawili hao wamefikia hatua ya kutambulishana wa wazazi wa pande zote mbili na mahari imelipwa hivyo kinachosubiriwa ni ndoa tu.

Awali, walifanya siri uhusiano huo hasa baada ya Majizzo kutemana na mzazi mwezake, Hamisa Mobeto ambaye uhusiano wake na Lulu kwa sasa umekuwa juu ya mawe. Kambi zao huko kwenye mitandao ya kijamii ni kurushiana vijembe na maneno ya shombo tu.

Nguvu ya wawili hawa inachagizwa zaidi na umaarufu wa Lulu kutokana na sanaa pamoja na sifa za Majizzo, ambaye ni Dj maarufu aliyewika zamani na sasa akiwa ni bosi wa EFM.

Irene Uwoya na Dogo Janja

Zilikuwa tetesi tu, kutokana na Dogo Janja ambaye ni mkali wa Hip Hop kumtaja Irene Uwoya kwenye wimbo wake wa ‘Nikupeleke Ngarenaro’.

Hata hivyo, huko mitandaoni kulifuka moshi kutokana na mashabiki wa wawili hao kila mmoja kuamini chake. Mapema mwizi Oktoba, kukazuka tetesi wamefunga ndoa. Hapo tena kukafuka moshi, kila mtu akijiuliza hili na lile, lakini ghafla tu wawili hao wakathibitisha kwenye vyombo vya habari kuwa, wamefunga ndoa na sasa ni mke na mume.

Hata hivyo, pamoja na kuingia kwenye orodha ya kapo zilizobamba mwaka huu, wawili hao inadaiwa kwa sasa kila mmoja anapambana kivyake baada ya kutemana.

Harmonize na Sarah

Kutoka kulala stendi hadi kusaini kwenye moja ya lebo kubwa kwa sasa Afrika, Wasafi Classic Baby (WCB) inayomilikiwa na msanii mkubwa Afrika. Bahati iliyoje kwa Konde Boy.

Kama hiyo haitoshi. Harmonize akaanzisha uhusiano na mrembo Jacqueline Wolper, ambaye ni staa mkubwa wa filamu nchini na gwiji wa mitindi.

Hadithi ya uhusiano wao ilivutia pia. Wolper aliwahi kuwa na uhusiano na Diamond, ambaye leo hii wamebaki wakiitana ‘mkwe’, lakini walitemana na maneno machafu mitandaoni.

Hata hivyo, Hamornize baada ya kuachana na Wolper, alikuja kupata mwanamke mwingine wa kizungu, ambaye hadi sasa bado wako kwenye uhusiano ya mapenzi. Wawili hawa wamekuwa gumzo kila kukicha kutokana na mabadiliko ya kimaisha aliyokuwa nayo Hamornize kwa sasa.

Kiukweli ukitaja uhusiano uliobamba mwaka huu, huwezi kuacha huu na umejizolea mashabiki wa kutosha.

Mama Diamond na Shamte

Jina la Shamte Maisala sio geni masikioni mwa watu, anatajwa kuwa ni mume wa mama mzazi wa mwanamuziki wa Bongo Fleva, Diamond Platinumz, Bi Sandra.

Wawili hawa wanadaiwa kufunga ndoa kwa siri mwishoni mwa mwaka jana na uhusiano wao ulianza kwa usiri, lakini wambeya wakaubaini na kuuweka wazi kama upepo.

Wawili hawa wameingia kwenye orodha ya kapo zilizobamba mwaka huu, kwani nyendo zao zimekuwa zikifuatiliwa sana.

Moja ya yaliyoibuliwa na mama Dai kushindwa kuvumilia na kujibu ni kuhusu umri wake na Shamte, baada ya kusema mtu wake huyo kweli ni mdogo, lakiniwamuache kwani kama angekuwa mdogo asingeweza kuoa. Lakini, kwa sababu umri wake unaruhusu ndiyo maana ameweza kuoa.

Diamond na Tanasha

Kapo mpya mjini ambayo inasumbua kinoma. Kwa sasa ndio inayobamba mitandaoni na Afrika Mashariki kwa jumla. Si unajua Diamond anavyobamba kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, sasa kipi atafanya kisijulikane? Hakuna.

Baada ya kuachana na Zari Hassan aliyezaa naye watoto wawili, Diamond aliendelea na maisha yake akijihusisha zaidi na muziki, huku wengi wakiamini atachelewa kurudi kwenye uhusiano kama alivyozoea.

Hata hivyo, baadaye zikaanza kama tetesi za Diamond anajihusisha kimapenzi na mrembo kutoka Kenya, Tanasha Donna Oketch, ambaye ni mtangazaji katika kituo cha redio cha NRG kule Kenya.

Hata hivyo, pamoja na tetesi hizo, Diamond hakupoteza muda, akamtangaza Tanasha kuwa mpenzi wake kupitia tamasha la muziki la Wasafi Festival kule Mtwara.

Huko mitandaoni ndo hakukukalika kabisa kwani, baada ya kuanika video inayowaonyesha wawili hao wakiwa kwenye mahaba mazito. Kwa sasa wale waliokuwa wakimzengea Diamond kila wakiingia kwenye mitandao hasa kurasa zake za mitandao ya kijamii, wanabaki kulia tu.

Ay na Remmy

Msanii wa Bongo Fleva, Ambwene Yessayah ‘AY ‘ na mkewe Rehema Sudi ‘Remmy’ ambaye ni Mnyarwanda nao wameingia katika kapo zilizobamba mwaka huu.

AY amefunga ndoa na mchumba wake wa siku nyingi, Remy mwanzoni mwaka mwaka huu na hadi sasa wamefanikiwa kupata mtoto mmoja wa kiume.

Alikiba na Amina

Hapa Bongo ilisimama unaambiwa kwani, kila mmoja aliamini King Kiba atamuoa mrembo mmoja maarufu sana hapa Bongo, lakini mambo yakawa tofauti kabisa. Kiba akakimbilia zake kuchukua jiko kule Mombasa, Kenya kwa kumuoa Amina Khelef na kufanya bonge la sherehe.

Kiba sio tu anaingia kwenye kapo bomba mwaka huu, pia harusi yake inaingia kwenye zile zilizobamba kinoma kwani, ilirushwa mubashara kwenye luninga kuanzia kule Mombasa hadi hapa Bongo. Azam TV ilihusika zaidi kwenye mpango mzima.

Jux na Vanessa Mdee

Iliwachukua muda mrefu sana Jux na Vanessa Mdee kukiri ni wapenzi. Pamoja na kuamua kuuweka wazi uhusiano wao, bado si watu wanaofurahia sana uhusiano wao. Wana takriban miaka mitatu sasa tangu waanze kuwa pamoja.

Kuna wakati waliamua kuuweka wazi kidogo uhusiano wao kwa kuweka picha zao kwenye mitandao ya kijamii, lakini sasa wameamua kuacha japo kwa walio karibu nao wafahamu namna wawili hawa wanavyopendana na kupeana kampani. Nina uhakika Jux ana ushindani mkubwa kuhakikisha Vee Money anaendelea kuwa wake.

Jux pia kwa upande wake anafahamika kwa maisha ya kifahari aliyonayo na hivyo, kujitengenezea sumaku inayovutia warembo wengi.

Japo hivi karibuni iliibuka kwa kubamba na tetesi za kuachana kwa wawili hawa, lakini baadae Vanessa aliweka wazi kupitia Mwanaspoti kuwa bado wako pamoja na mambo yanakwenda poa sana.

Nahreel na Aika

Hawa wametoka mbali sana. Kutoka kusoma pamoja India wakiwa na kundi la Pah One, hadi kutengeneza si tu kundi maarufu Afrika Mashariki la Navy Kenzo, bali pia kuanzisha studio na lebo yao, The Industry na kuanzisha familia ambayo ni mafanikio makubwa kabisa kwenye mahusiano yao.

Kwa wanaowafahamu vyema, watakubali kuwa Nahreel na Aika si tu wapenzi, bali pia ni mtu na mshikaji wake na kibiashara wanaelewana kinoma.

Kapo hii imekuja kubamba tena mwaka huu baada ya kufanikiwa kupata mtoto na kuwa gumzo huko mitandaoni.

Casto na Tunda

Kwani nani ambaye hamfahamu Tunda? Yaani uliza mtu yeyote ambaye anafuatilia ishu za burudani hapa Bongo atakwambia.

Au kama vipi ingia kwenye google kisha andika Tunda, utaona picha za mrembo mkali kwenye staili yake ya nywele inayokupa mzuka. Sasa Tunda ana mshikaji wake anaitwa Casto, ambaye ni mtangazaji wa Clouds Tv. Hawa walipoanza uhusiano wa kimapenzi, hawakuanza kwa kuficha ficha bali kila mtu alifahamu kwani, kila wanachofanya basi utaona picha kwenye kurasa zao hasa huko instagram.

Hii ni kutokana na Casto kujiamini zaidi na kufanya uamuzi wa kuchora tattoo yenye jina la Tunda mkononi kama ishara ya upendo.

Hata hivyo, pamoja na kelele za mashabiki wake na watu kumshauri juu ya hatua hiyo, Casto hakutaka kusikia la mtu na alizidisha mapenzi zaidi kwa Tunda. Wameingia kwenye rekodi za kapo bomba, japo huko kweye mitandao stori za mjini ni kuwa, wamepigana chini. Hata hivyo, sio Tunda wala Casto ambaye amethibitisha hilo.