MACHA : Kama utani vile, BSS yampa ulaji kutoboa kiulaini

Monday January 14 2019

 

By Thomas Ng'itu

UKISIKIA zali ndilo hili mwanangu. Ndio, kabla ya Shindano la Bongo Star Search 2018, Julius Macha wala hakuwa akifahamika sana.

Alichukuliwa kama tu devera wa bodaboda kama walivyo madereva wengine kijiweni na hata mtaani kwao, lakini kwa sasa yeye ni habari nyingine unaambiwa.

Kumaliza kwake nafasi ya tatu katika shindano hilo la kusaka vipaji vya muziki kumemfanya ajizolee umaarufu mkubwa na kugeuka kuwa staa jambo ambalo hakulitegemea maishani mwake.

Katika shindano hilo, Macha aliziteka hisia za mashabiki wengi kiasi cha kujikuta ndiye msanii pekee anayeimba miondoko ya kufokafoka kusalia katika shindano hilo hadi hatua ya fainali.

Mwanaspoti baada ya shindano kumalizika lilifika mtaani kwake, Kiwalani Migombani jijini Dar es Salaam na kutaka kufahamu mipango yake baada ya kutoka ndani ya BSS.

TATIZO MKWANJA

Pesa ndio kila kitu katika maisha ambayo yanayotuzunguka na kwa upande wa msanii huyo anasema pesa imekuwa ndio chanzo cha kuchelewa kusikika katika gemu licha ya kupambana kitaa kitambo.

“Muziki unahitaji pesa ili kuufanya pia unatakiwa uwe na menejimenti lakini, vyote sikuwa navyo, hivyo nilikuwa nafanya muziki kwa kutumia muda mrefu kusaka fedha ya kula na kuendeshea maisha na siyo ya kuendeshea muziki.”

Anaongeza wakati anapambana kutoka kimuziki alikuwa akishughulika na nyimbo laini, lakini baadaye aliamua kubadili na kuanza kuimba muziki wa kufokafoka.

“Muziki unahitaji uvumilivu sana, kipindi cha nyuma nilikuwa chini ya wazazi, niliamua kuacha muziki na kuendelea na maisha yangu mengine, ila sauti yangu ilikuwa ikiwagusa watu wengi lakini tatizo likawa ni fedha za kuendesha fani, kwani kote kulihitajika fedha.”

BODABODA YAMPELEKA BSS

Macha anafichua hakuwa na mipango wa kujiunga na BSS, lakini alipata ushawishi mkubwa kutoka kwa mteja aliyempakiza aliyekuwa akielekea eneo ambalo shindano lilikuwa linafanyika.

“Nilikuwa nafanya muziki, ila baadaye nikawa niponipo tu, lakini kama utani siku moja nilimpakiza mteja anayejua kipaji changu, aliyekuwa akienda kwenye usaili wa BSS.”

Jamaa alimtia hamasa naye kujitosa na kweli kama utani aliweza kujikuta akipenya hatua moja hadi nyingine kupitia BSS ambayo awali wala hakuwahi kufikiria na pengine kwa vile shindano lilizimika.

Alifunguka na kusema baada ya kufika katika shindano hilo aliweza kupenya katika mchujo na kuanzia hapo ndio alizidi kukaza uzi na kuhakikisha anatoboa.

MAISHA YAMEBADILIKA

Macha anasema baada ya kutoka katika shindano hilo, maisha yake yamebadilika kwa namna moja ama nyingine, kwasababu alivyokuwa anachukuliwa mwanzo ni tofauti na kipindi hiki.

“Baada ya kumaliza nimesaini mikataba na baadhi ya kampuni kuwa kama balozi wao, jambo zuri ambalo nilikuwa nalihitaji kuwa sehemu fulani na nimefanikiwa kwa kiasi,” anasema.

Alifunguka zaidi ameweza kuwa na bodaboda nyingine kiasi cha kumuajiri kijana mwenzake.

“Wakati nikiwa kwenye shindano nilishinda pesa kiasi fulani kwa kutengeneza tangazo, pesa ile nilitumia kununua bodaboda nyingine ambayo inanisaidia kupata pesa ya kula kila siku.”

Aliongeza kwa sasa licha ya kuwa na bodaboda mbili, moja ameamua kuendelea kutumia kama usafiri wake, licha ya kukiri ameacha shughuili ya udereva wa bodaboda ili afanye muziki kwa ufasaha.

AMTAJA MR T TOUCH

Wasanii wengi wanaotoboa kupitia shindano hilo hupotea, lakini Macha kwa upande wake inaweza kuwa tofauti.

Anafichua ameamua kufanya ngoma na mtayarishaji mkubwa wa muziki nchini, Mr T Touch, ili aweze kuendelea kukaa katika vichwa vya mashabiki wake.

“Ni kazi juu ya kazi na video kali nadhani mambo mengine niiachie menejimenti yangu, ila kuna wimbo nimefanya na Mr T Touch siwezi kusema jina kwa sasa ila mkali kinoma,” anasema.

Aliongeza katika wimbo huo ameimba mwenyewe akishirikiana na mtayarishaji huyo ambaye amekuwa akiweka sauti yake katika baadhi ya nyimbo.

SAFARI YAKE YA MZIKI

Julius Macha amefichua harakati zake za muziki zilianza mwaka 2005 akiwa kidato cha pili akiwa anaimba, kabla ya mwaka 2006 kubadilisha upepo na kuanza kufokafoka.

“Rafiki yangu aitwaye Edward Allan aliniambia kutokana na sauti yangu ilivyo, nafaa sana kurap ndipo nikaanza kurap tena nikiwa na kiu ya kutoka kama wasanii wengine wanaotamba.”

Macha anadokeza mbali na fedha kuwa tatizo, lakini pia majukumu ya kimaisha yamechangia kumkwamisha kutoka mapema, lakini kwa sasa amejipanga kwelikweli kutusua.

“Mtoto wa kiume inabidi uwe na maisha yako, kuanzia kujijenga gheto kwani kuna wakati mtu inafikia usile tena nyumbani na kuwa na maisha yako, ndipo nilipoona ngoja nikomae kwanza huko kabla ya BSS kunichomoa na sasa kila kitu poa,” anasema.

Amemalizia kwa kuwaomba mashabiki wa muziki na waliofuatilia jkwa ukaribu BSS kumuunga mkono hasa atakapokuwa akiachia kazi zake hewani, kwani ndio anaowategemea kumuinua kisanii.

“Mashabiki ndio kila kitu, wakiniunga mkono kwa kile nitakachofanya, itanisaidia kuinuka na nawaahidi nitakuwa wanaletea mawe kwelikweli ili wapate burudani.”

Advertisement