K-Lyn azuiwa kuona kaburi la mumewe

Muktasari:

Kupitia mtandao wake wa  kijamii waTwiter,  K-Lyn ameandika kuwa amenyamaza kwa mambo mengi na sasa amenyimwa nafasi ya kwenda kutembelea kaburi la marehemu mume wake na kuweka wazi kuwa hatokubali kuendelea kuona wanawe wakisononeka.

MKE wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kampuni ya IPP na mfanyabishara maarufu nchini, Marehemu Reginald Mengi, Jacqueline Mengi 'K-Lyn' amesikitishwa na kitendo cha kuzuiwa yeye pamoja na wanawe kutembelea kaburi la mumewe.
Mengi alifariki dunia Mei 2 mwaka jana, akiwa kwenye matibabu Dubai, U.A.E, ameacha mke na watoto watano ambao ni Regina, Rodnay, Abdiel, Jayde na Ryan.
Kupitia mtandao wake wa  kijamii waTwiter,  K-Lyn ameandika kuwa amenyamaza kwa mambo mengi na sasa amenyimwa nafasi ya kwenda kutembelea kaburi la marehemu mume wake na kuweka wazi kuwa hatokubali kuendelea kuona wanawe wakisononeka.
"Nimenyamaza kwa mengi sana tu. Mmefikia hatua ya kunizuia mimi na wanangu kuingia kwenye kaburi la mume wangu, tunafukuzwa eti mpaka tuombe ruhusa ya kuingia kwenye kaburi la mume na baba wa watoto wangu! Nimechoka, sitakubali kuendelea kuona wanangu wakisononeka na sitakaa kimya," aliandika K-Lyn
Marehemu Mengi alifariki akimuacha mkwe huyo na watoto mapacha ambao wote ni wa kiume, Jayde na Ryan.