VIDEO: Diamond akubali kumlea mwanaye kwa Hamisa Mobeto

KESI YA MATUNZO MTOTO WA DIAMOND YAFUNGWA, MWENYEWE AFUNGUKA

Muktasari:

Baada ya kutoka mahakamani Diamond alisema walifika mahakamani hapo kwa ajili ya kuweka kumbukumbu ili upande wa ustawi na mahamaka ziwe sawa ili kesho na keshokutwa kisije kikazungumzwa kitu kingine cha uongo.

Dar es Salaam. Hatimaye jalada la kesi ya madai ya matunzo ya mtoto lililofunguliwa na Mwanamitindo Hamisa Mobeto na Mwanamuziki Diamond Platinumz limefungwa rasmi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu upande wa Watoto.
Baada ya kutoka mahakamani Diamond alisema walifika mahakamani hapo kwa ajili ya kuweka kumbukumbu ili upande wa ustawi na mahamaka ziwe sawa ili kesho na keshokutwa kisije kikazungumzwa kitu kingine cha uongo.
Alisema wanategemea mtoto wao aje awe mtu fulani ama kiongozi na kuwashauri wazazi wa kiume na wa kike wajitahidi kuweka majivuno yao pembeni wanapokuwa na migogoro na wasimuingize mtoto.
Kwa sababu kuwa namba moja ama nyingine inamwathiri mtoto.
"Ni lazima kuweka majivuno pembeni ya matatizo yenu binafsi kwa kuwa mtoto ndiyo anaumia, ni lazima muangalie ni namna gani mnatengeneza mazingira mazuri ya kuweza kumlea na kumsaidia mtoto," alieleza Diamond.
Kwa upande wa Wakili wa Mobeto, Walter Godluck alisema ustawi wa jamii unasaidia katika usuluhishi wa kesi za watoto ambazo zinahusu malezi ambapo baba na mama hukubaliana ni jinsi gani wanaweza kulea mtoto.
Na kwamba leo walipeleka ripoti ya usuluhishi mahakamani ambapo kesi ya msingi ya matunzo ya mtoto ilifunguliwa.
Alisema malalamiko waliyoyaleta kuhusu malezi ya mtoto upande wa pili wameridhia na wameona kuna haja ya kuyafanyia kazi na kwamba kiasi cha fedha wamekubaliana ila wamekiweka kifamilia.
Wakili huyo alisema wazazi wamekubali kushughulikia malezi mtoto, Diamond yupo tayari kumlea mtoto na yupo tayari kulifanya hilo kwa kadiri inavyowezekana.
Hamisa Mobeto alisema amefurahia maamuzi hayo kwa kuwa upande zote mbili walikaa na wakakubaliana.
Ameshukuru kwa kuwa kila mtu ameridhika nayo na wamekwisha.
Mobeto alifungua kesi hiyo mahakamani hapo, pamoja na mambo mengine alikuwa anaomba matunzo ya mtoto waliozaa na msanii Diamond.
Mobeto  alikuwa anaiomba mahakama imwamuru Diamond kutoa matunzo ya mtoto ya kila mwezi na alifungua kesi hiyo kupitia mawakili wake Abdullah Lyana na Walter Godluck kutoka kampuni ya uwakili ya Century Attorneys.
Kupitia hati hiyo ya madai, Mobeto  anaomba Diamond amuombe msamaha kwa kumsababishia madhara yaliyoishtua familia yake.
 Diamond aliwasilisha hati ya majibu kinzani akipinga maombi hayo ya Mobeto  akidai  gharama anazodai kulipwa kwa mwezi ya Sh 5 milioni  kwa ajili ya matunzo ya mtoto ni kubwa hawezi kuzimudu.