Ishu ya umri ya Wema Sepetu kumfikisha hapa, Basata wafunguka

HUKO kwenye mitandao ya kijamii habari ya mjini ni ‘birthday’ ya mrembo wa Tanzania wa mwaka 2006, Wema Sepetu ambaye kila Septemba 28 anasherehekea siku yake ya kuzaliwa.

Juzi mrembo huyo aliposti kwenye mtandao wa kijamii akisherehekea siku yake ya kuzaliwa na kueleza kutimiza miaka 30 jambo lililoibua mjadala mzito.

Hata hivyo, hesabu za umri huo na mwaka alioshiriki na kushinda taji la Miss Tanzania viligonga vichwa vya watu, kwani moja ya masharti ya kushiriki shindano hilo ni lazima mhusika atimize miaka 18 hadi 23, hivyo kama Wema alidanganya, alishinda taji hilo akiwa na miaka 16.

Wafuasi wake mitandaoni walimbana kwa maswali kuhusu umri wake na kwa mara ya kwanza juzi akakiri, ndio ametimiza miaka 30.

Mwenyewe akafunguka laivu, amezaliwa mwaka 1990 na wakati anashinda taji la Miss Tanzania alikuwa na miaka 16. Akadai alidanganya umri ili kupata fursa ya kushiriki shindano hilo ambalo Jokate Mwegelo alishika namba mbili. Kitendo cha Wema kukiri kudanganya kisheria ni kosa na kwa mujibu wa wakili Kasanda Mitungo, moja ya adhabu za kudanganya umri na kama itathibitika ni kuvuliwa taji hilo.

Ingawa Kasanda amebainisha, kuvuliwa taji hilo pia kutategemea na kanuni za shindano ingawa kikanuni, mshiriki hapaswi kuwa na miaka chini ya 18 au zaidi ya 23.

Hata hivyo, aliyekuwa Mkurugenzi wa Miss Tanzania wakati Wema anashinda taji hilo, Hashim Lundenga ‘Uncle’ alisema suala hilo limeshapita na hawafikirii kumchukulia hatua zozote ikiwamo kumvua taji hilo, kama ambavyo inaelezwa mitandaoni.

“Kama anasema alidanganya ni yeye, shindano limeshapita na hatuwezi kumchukulia hatua zozote. Alifanya hivyo kwa matakwa yake na suala lake limeshapita,” alisema.

Ingawa Wakili Kasanda alisema kisheria kudanganya ni kosa, lakini ni kwa namna gani amedanganya pia itaangaliwa, na kama ikithibitika alighushi nyaraka, basi adhabu yake ni kifungo cha kuanzia miaka saba jela kama atashtakiwa na itathibitika,” alisema.

Hata hivyo, alisema hakuna sheria ya moja kwa moja ambayo imeanzisha mashindano, lakini kuna vigezo vya mashindano ambavyo kama kuna kigezo cha umri na ikathibitika mshindi alidanganya moja ya hatua anazoweza kuchukuliwa ni kuvuliwa taji na kamati ambayo kama itaamua pia inaweza kumshtaki, lakini iwe na ushahidi unaoweza kuthibitika.

“Kesi za jinai huwa hazina ukomo, hata kama ni miaka mingapi imepita na suala kubwa hapo ni kuwepo na uthibitisho alidanganya vipi? Ingawa kudanganya umri ni kosa la jinai,” aliongeza.

Alisema kingine katika ishu ya Wema kudai alidanganya umri, hakutoshi kumtuhumu moja kwa moja kwani huenda amezungumza akiwa katika hali ya utani au vinginevyo na mjadala gani ulianza kabla ya yeye kueleza amefikisha miaka 30 na mwaka 2006 alidanganya umri.

Akizungumzia sakata la warembo kudanganya umri, Angela Damas ambaye ni Miss Tanzania 2002, alisema ni ngumu kubaini hilo.

“Unajua ukiwa katika kambi ya Miss Tanzania mara nyingi unakuwa unajiangalia wewe tu, hadi kufahamu mwenzako amedanganya umri ni jambo gumu sana.

“Wakati nashiriki, suala hilo sikuwahi kulisikia, hivyo sijui lolote kuhusu baadhi ya warembo kudanganya umri ili washiriki kama ambavyo unaniambia Wema amekiri hilo mitandaoni,” alisema.

Basata kulifuatilia

Kwa upande wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), limeeleza kushtushwa na taarifa hizo za Wema na kuahidi kulifuatilia.

Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza, alisema watafuatilia suala hilo kwa karibu na kwamba, hawako tayari kuona sanaa inatiwa doa kwa watu kutoa taarifa za uongo hasa ikizingatiwa mashindano ya urembo umri ni moja ya vigezo.

Mngereza akaenda mbali kwa kukumbushia sakata la Sitti Mtemvu ambapo, hatua stahiki zilizchukuliwa ili kulinda hadhi ya shindano hilo kubwa nchini.

“Kwa Sitti mliona tulivyofanya, hivyo hata kwa Wema hili halitushindi pamoja na kuwa alishinda taji hilo zamani. Hakuna kinachotuzuia kuchukua hatua na tutashirikisha na mamalaka nyingine,” alisema.

Alipoulizwa kama kuna malalamiko wamewahi kupata enzi za Wema alipotawazwa kuwa Miss Tanzania, Mngereza alisema hana uhakika na kuahidi kurejea katika nyaraka za nyuma kwani, wakati huo alikuwa hayupo kwenye wadhifa huo.

Katika hatua nyingine, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini, RITA, umesema kuwa kisheria hawawezi kumchukulia hatua Wema hadi pale watakapopokea malalamiko kutoka mamlaka husika.

Pia, imesema kuwa kwenye suala hilo wenyewe wanabaki kusimama kama mashahidi.