Huyu ndio Lulu usiyemjua

Tuesday February 12 2019

 

By Doris Maliyaga

WAKATI Wekundu wa Msimbazi wakipambana na Al Ahly ya Misri leo Jumanne katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi kuna shabiki wao mkubwa, Elizaberth Michael ‘Lulu’ anasema leo lazima Mwarabu apigwe tu.

Lulu ambaye alipata umaarufu akiwa na umri mdogo kwenye uigizaji, lakini akapita katika changamoto za kila aina ndani na nje ya kazi hiyo hadi akaishia kufungwa jela kwa kutiwa hatiani kuhusika na kifo cha msanii mwenzake, Steven Kanumba.

Binti huyo mwenye umbo dogo na mweupe kwa rangi na kwa mujibu wa mtandao amezaliwa Aprili 16, 1995 sasa ana miaka 23, alitinga kwenye Ofisi za Mwananchi Communications LTD inazozalisha Magazeti ya Mwananchi, The Citizens na Mwanaspoti ambalo linalokupa fulu stori ya maisha yake sasa na pia utafahamu kuhusu kampeni yake ya Save My Valentine.

Kwanza anafunguka wazi, yeye ni shabiki wa Simba damu na analishabikia chama hilo kwa kuwa mama yake, Lucresia Karugila ni shabiki wa kulia wa wababe hao wa Msimbazi: “Ulikuwa mkumbo tu, lakini mimi ni Simba damu.”

MAUMIVU YA VITU VIZURI

Akiwa katika vazi la suruali aina ya jinzi na tisheti, kichwani amesuka rasta zilizoficha kidogo sehemu ya paji lake la uso ambao lipo katika uhalisia wake, yaani hakuna kipodozi cha ziada zaidi ya mafuta tu, Lulu anasema maisha yake kwa sasa yamebadilika.

“Kila changamoto ninayopita haijaniacha salama, ilinipa funzo na imenivusha kutoka sehemu moja hadi nyingine,” anasema Lulu anayeamini Mungu anayemwamini ndiyo sababu ya maisha yake kuwa hivyo.

“Napenda kueleza kwa mifano ili nieleweke. Katika maisha ya shule unapoanza darasa la kwanza unapotaka kwenda la pili lazima utafanya mtihani, unafaulu au kufeli, unaposonga mbele zaidi mitihani ya madarasa ya juu huwa ndiyo migumu zaidi.”

Ametoa mfano wa pili ni mama mjamzito anapotarajia kupata mtoto, lakini shughuli anayokutana nayo lazima ateseke kuanzia mimba hadi uzazi ndipo anapata anachokikusudia.

“Vitu vingi vizuri katika maisha yangu huwa navipata kupitia njia ya maumivu na nimekuwa navuka kwa sababu navichukulia sehemu ya mapito tu. Lakini kama ningekuwa mtu wa kunung’unika na kutokukubaliana na hali halisi nafikiri lingekuwa tatizo,” anasema Lulu, ambaye alihukumiwa kifungo cha kwenda jela miaka miwili mwaka 2017 na kubadilishiwa adhabu ya kuwa kifungo cha nje mwaka 2018. Anasema kwa sasa yeye ni mfano mzuri wa kuigwa katika maisha kutokana na hatua anazovuka, mbali na kukubaliana na hali hiyo, amekuwa akifanya maamuzi yanayompa matokeo mazuri.

“Ukiamua kuwa Lulu wa sasa lazima ukubali mabadiliko na kufanya maamuzi juu ya maisha unayotaka kuishi kwa wakati huo,” anasema Lulu.

Anasema, kikubwa anachoshukuru ni mzima anapumua, mwenye afya na yalikuwa mapenzi ya Mungu ambayo yametimia.

MAISHA YA GEREZANI

“Nimekutana na watu wa aina tofauti , sasa najua niongee nini na kuishi vipi, hata ninapokaa na mtu kitu anachozungumza huwa nakifanyia kazi na kujua anamaanisha nini,” anaanza kwa kueleza Lulu huku akionekana kuwa mpole zaidi anapozungumzia kuhusu maisha yake ya jela.

Katika maisha hayo ya gerezani ana ujumbe wa kumpa Rais Dk. John Magufuli na anaanza na hili: “Cha kwanza ni pongezi, kesi zimekuwa zikiendeshwa kwa haraka tofauti na ilivyokuwa zamani, watu walikuwa wanakaa kwa kipindi kirefu gerezani. Pili, ni changamoto, gerezani kuna msongamano wa watu na mazingira si mazuri.”

“Makazi hayaridhishi na hata kama ni fundisho kwa mhusika si kwa aina ile ya maisha, ungefanyika mpango kwa baadhi ya kesi na kulingana na uzito wa makosa, mshtakiwa angekuwa nje kwa dhamana na ahudhurie mahakamani akitokea nyumbani

Akizungumzia suala la kutoka gerezani akiwa amesuka nywele alisema “Nimekaa gerezani kama mshtakiwa mwingine yeyote sikuwa napendelewa au namna gani. Jamani gerezani kusuka kwa mwanamke ni maamuzi yake jambo ambalo watu wengi hawalijui,” anasema.

MAJIZZO NDIYO KILA KITU

Lulu, ambaye ni mke mtarajiwa wa Francis Ciza ‘Majizzo’ ambaye anapatikana pale EFM, ameshamvisha msanii huyo pete ya uchumba na wanatarajia kufunga ndoa hivi karibuni.

“Majizzo ana mchango mkubwa katika maisha yangu, naweza kusema amenibadilisha kwa sehemu kubwa, ananielekeza mambo mengi ambayo yana faida,” anasema Lulu huku akigoma kuweka wazi walikutana wapi na lini.

KULEA WATOTO SI WAKE

Pamoja na kuvishwa pete na Majizzo, Lulu bado hajapata mtoto na mwanaume huyo, ambaye ana watoto aliyezaa na wanawake wengine akiwemo mwanamitindo Hamisa Mabetto.

“Niko tayari kuwa mama bora wa watoto wa Majizzo kwa sababu nimefanya maamuzi. Nimekubali kuwa wa Majizzo kwa sababu tunaendana ananisikiliza na namsikiliza,” anasema Lulu.

“Kila kitu ni maamuzi, kama nimeamua na tukakubaliana kwa hao wengine sipendi kuwazungumzia kwa sababu huenda walikuwa hawataki au yeye hakuwa tayari. Pia, huenda ni makubaliano yao siwezi kujua na tuyaache kama yalivyo,”anasema Lulu ambaye alipokuwa gerezani kulikuwa na video ikizunguka mitandaoni ikimwonyesha mtoto wa Majizzo aliyezaa na Hamisa kuwa akisema amemmisi.

“Kusema kweli ile video niliiona, iliniumiza na nilijisikia vibaya kwani mtoto kama yule kuonyesha hisia zake si jambo rahisi,” anasema Lulu na kufafanua mtoto huyo anamjua kwa sababu wamekuwa wakionana mara kwa mara.

KAMPENI YA SAVE MY VALENTINE

Lulu ambaye Februari 14, mwaka jana alikuwa gerezani anafafanua sababu ya kampeni ya Save My Valentine, ambapo aliandaa nguo 62 alizozipenda na ameziuza ili kupata fedha kwa ajili ya watu wenye uhitaji.

“Lengo ni watu wenye uhitaji, wengi wanajua Valentine ni kwa wapenzi lakini kuna wazee ambao wako peke yao, mama aliyefiwa, baba aliyefiwa na wengine wasiokuwa hawaoni umuhimu wowote juu ya jambo hilo,” alisema Lulu ambaye mbali na kuuza nguo hizo, amekusanya michango nguo, vyakula na mahitaji mengine kwa ajili ya watu hao.

“Nimewakumbuka kwa staili hiyo na wao wajue kuwa wanakumbukwa. Nakumbuka siku kama hiyo mwaka jana nilipokuwa gerezani, tulichofanya ni kuandikiana ujumbe na kutumiana. Nimepitia maisha hayo na kugundua kundi lenye uhitaji ni ngumu,” anasema Lulu na kuweka wazi Februari 14 ndiyo ataweka wazi ataanza na kundi lipi.

Advertisement