He! kumbe filamu ya uchawi Hamisa, Diamond iko hivi

KATIKA mitandao ya kijamii kuna mtu ameshikwa uchawi. Ni mwanamitindo Hamisa Mobetto. Sakata hilo ndilo limenikumbusha hekaheka za Manyaunyau anapotaka kufanya kile huaminika na wengi, ni kuibua uchawi.

 

BY LUQMAN MALOTO

IN SUMMARY

  • Manyaunyau ni jasiri sana. Anaweza kuingia sehemu ambayo hayupo mwingine mwenye ujasiri wa kuingia. Atazama kwenye mtaro wenye maji machafu au bwawa la majitaka na kuibuka na pembe ya swala au tunguli na kueleza huo ndiyo uchawi uliokuwa umetegwa.

Advertisement

KATIKA mitandao ya kijamii kuna mtu ameshikwa uchawi. Ni mwanamitindo Hamisa Mobetto. Sakata hilo ndilo limenikumbusha hekaheka za Manyaunyau anapotaka kufanya kile huaminika na wengi, ni kuibua uchawi.

Manyaunyau ni jasiri sana. Anaweza kuingia sehemu ambayo hayupo mwingine mwenye ujasiri wa kuingia. Atazama kwenye mtaro wenye maji machafu au bwawa la majitaka na kuibuka na pembe ya swala au tunguli na kueleza huo ndiyo uchawi uliokuwa umetegwa.

Basi Manyaunyau na sanaa zake za kuibua na kukamata wachawi, watu wengi tu ameshawanasa na kuwaumbua. Kimsingi Manyaunyau yeye amejikita kwenye uhodari wa kushughulika na wachawi. Kama mbunge wa zamani wa Korogwe Vijijini, marehemu Profesa Majimarefu alipoitwa kiboko ya wachawi miaka ya 1990, ndivyo Manyaunyau anavyotamba katika zama mpya.

Kama Profesa Majimarefu zama hizo, pia kama Manyaunyau anavyotikisa kizazi kipya cha imani za ushirikina na uchawi, ndivyo na familia ya supastaa Diamond Platnumz inavyoibuka kwa kasi. Hamisa hana hamu jinsi alivyofanyiwa u-Manyaunyau au u-Profesa Majimarefu.

Sauti zinazodaiwa ni za Hamisa akizungumza na mtu anayetajwa ni mganga wa mambo ya ulozi, zimewekwa mtandaoni. Madai ni Mganga alimpokea Hamisa kama mteja. Kama ilivyo mgonjwa kwa daktari, inadaiwa Hamisa alianza kushusha mahitaji yake.

Unajua tena siku hizi ni dotcom. Hata waganga nao wamekuwa wa dotcom. Watoto walegevu wasio katika mitandaoni wanaita kudamshi. Naam, waganga nao wanadamshi. Inadaiwa Hamisa alikutana na sampuli ya waganga wa dotcom ambao nao hudamshi. Hawana koromeo wala vifua. Siri ya mteja haikai kabisa.

Mganga anadamshi siri ya mteja wake! Eti baada ya kuzungumza na Hamisa, mganga akamrekodi. Sauti ya Hamisa akaituma kwa mama Diamond, kule Instagram anaitwa Mama Dangote, sio mama yake Aliko Dangote (bilionea wa Dola za Trump), ni mama mzazi wa Diamond.

Mama Dangote akaona ameshinda bingo, akaivujisha sauti mitandaoni. Ndipo watu na upambe wao wakaibuka kushangilia na kushadadia kama vile ni Taifa Stars imefuzu Fainali za Kombe la Dunia. Hamisa akapakwa na kupewa majina mengi ya hovyo. Hamisa na urembo ule eti siku hizi anaitwa kigagu. Dunia ina mambo hii!

U-MANYAUNYAU ULIVYOFANYIKA

Hamisa amekaa kimya. Diamond ameshaibuka kuelezea hilo. Alisema alimfuata Hamisa na kumweleza kuwa zile sauti kweli ni zake. Kwamba Hamisa alitaka huduma ya ulozi kutoka kwa mganga, amfungefunge Diamond na ndugu zake ili apate kuolewa. Hamisa anapigania kuolewa na Diamond jamani.

Diamond na Hamisa ni wapenzi wa muda mrefu. Wana mtoto sasa. Inadaiwa Hamisa anamwona Diamond ni miyeyusho linapokuja suala ndoa. Hivyo, alihitaji msaada wa mganga ili aweze kumtuliza. Diamond mwenyewe anajijua hajatulia, sasa kwa nini mtoto wa watu asihangaike kumtuliza? Ikibidi kwa sangoma. Si usangoma nao ni kudamshi?

Anyways, kivuna ubuyu cha mtu mzima kimepokea ndogondogo kwamba u-Manyaunyau wa familia ya Diamond ni tego ambalo Hamisa alitegwa kupitia shosti wake. Shosti mtu alimfuata na kumpa somo ili mambo yake na Diamond yanyooke, yupo fundi ulozi ambaye angemuunganisha naye ni moto balaa.

Tena kwa sauti zao zilee: “Nakwambia huyo mganga anadamshi balaa. Mimi mwenyewe kanidamshia ya kwangu mpaka sasa mambo yangu ni meupeee!” Hamisa akaona mambo si ndiyo hayo. Akaomba aunganishwe fasta na huyo mganga wa dotcom ili aweze kumdamshia mambo yake na Diamond.

Hamisa kaambiwa na shosti wake anayemwamini. Kampa na namba ya simu. Wasiwasi wa nini? Akamvutia waya mganga wa kudamshi. Mwenyewe akajiachia kueleza aliyoyahitaji kwa fundi ulozi, pasipo kutambua kuwa fundi ulozi huyo ni feki, aliyetengenezwa kupitia shosti wake. Kwa kifupi Hamisa akapigwa bei na shosti wake.

Baada ya sauti hizo kuvuja, Hamisa kila akimpigia simu shosti wake hapokei simu. Hiyo ilikuwa na uthibitisho kamili aliuzwa kwa mganga feki ili ajieleze kwa simu, arekodiwe kisha sauti ivujishwe, aumbuliwe. Hizo ndizo nyakati za kudamshi. Si mnajitapa kuwa mnadamshi? Basi na mashosti pia wanadamshi. Shosti kamdamshia Hamisa.

Kama vipi usidamshi na hiyo, damshi na hii ‘vesi’ ya pili; Hamisa kweli alimwendea hewani fundi wa ulozi, akamweleza shida zake. Sasa jiulize ilikuwaje huyo fundi ulozi aache kuzingatia utoaji tiba kwa mgonjwa wake na kuhamia kwenye udukuzi wa umbea? Akamrekodi mazungumzo yote na kuvujisha sauti.

Taarifa zinasema huyo fundi ulozi baada ya kupata sauti ya Hamisa akibwabwaja kuhusu mpango wa ‘kumtengeneza’ Diamond ili afunge naye ndoa, moja kwa moja alizitupa hizo sauti kwa Mama Dangote. Unajiuliza; bi mkubwa ndiye ana mtandao wa waganga na wote wanamjua kiasi wanamtumia kila kinachomhusu na mwanaye?

Je, huyo fundi ulozi aliyemdamshia Hamisa, Mama Dangote ni mteja wake? Maana inaonekana kuna ukaribu kati ya bi mkubwa na sangoma mwenyewe. Usiache pia kujiuliza; je, Mama Dangote amesambaza mitego kwa waganga wote kiasi Hamisa akipeleka pua kokote anapewa taarifa? Utakuwa umeuona ukweli mahali!

SASA TUNGUMZE KI-UTU UZIMA

Tukubali hapa kuna staili za kina Manyaunyau, hivyo mchawi hakatizi anga fulani fulani kule maeneo. Au tunaweza kusadiki mtandao wa mafundi ulozi ndani ya Dar es Salaam upo hapo, hivyo ukienda kuomba huduma ya kumchawia Diamond lazima ishu ivuje tu.

Kwamba ndiyo maana Hamisa amenaswa na sauti zake zimevujishwa. Tusipuuze taarifa Hamisa alitegwa kupitia shosti wake, aliyemwongopea kuhusu kuwepo kwa fundi ulozi kiboko, kumbe lengo lilikuwa kumpiga bei ili aingie maboya, arekodiwe sauti kisha aumbuliwe kama alivyoumbuliwa.

Hata hivyo, swali lipo; nani anaweza kuthibitisha kitaalamu sauti zenye kusikika ni za Hamisa? Katika ulimwengu uliojaa mafundi wa kuiga sauti za watu, inashindikana vipi kuamini kuna mtu mwenye utaalamu wa hali ya juu, aliiga sauti ya Hamisa ili kumuumbua kama anavyoumbuliwa?

Narudia tena kuuliza; nani anaweza kuthibitisha kitaalamu kweli sauti ni za Hamisa? Siyo useme tu “huyu ni mwenyewe, naijua sauti yake!” Hapa lazima uzungumze kitaalamu. Ndiyo maana hata mahakamani huitwa wataalamu wabobezi wa utambuzi wa sauti. Siyo kujibu kiwepesi tu!

Kwa hoja hiyo, Hamisa akiamua kufungua kesi mahakamani ya udhalilishwaji (defamation), kinga ya wanaomshambulia itakuwa nini? Mahakamani hakuna kupeleka blah-blah. Inatakiwa kwenda kuthibitisha ukweli unaousimamia. Gharama za kuthibitisha ukweli kuwa sauti ni ya Hamisa watu wanazijua?

Tanzania ni Jamhuri isiyoamini katika uchawi na ushirikina. Kitanzania uchawi na aina zote za ushirikina ni imani potofu. Wewe unasema umebaini mtu alikuwa anataka kukuroga. Ushahidi wako ni sauti akiongea na mganga. Sasa Hamisa akienda mahakamani kushtaki kwa kudhalilishwa uhusika wake (defamation of character), huo uchawi utakwenda kuthibitishwa mahakama za nchi gani?

Ni wazi Hamisa akiamua au akivutwa sikio na wataalamu wa sheria kuna pesa zake nyingi kwa baba wa mtoto wake. Amefanyiwa udhalilishaji mkubwa. Ila nikipata nafasi ya kumshauri, nitamwambia awe mtulivu, asikuze uhasama. Nyakati zijazo zinaweza kujaa upendo, furaha na amani kupitia kusamehe kuliko kuvimbiana.

Kwa mashabiki wote wa sakata la uchawi wa Hamisa, nawaambia mambo ya giza si ya kushadadia sana. Nyumba nyingi tu watu wanashikana uchawi sema tu hayawi hadharani. Wanawake wengi kwenye nyumba nyingi wanaitwa wachawi, wanaloga waume na wachumba zao. Shabikia hayajakukuta, kesho yakikukuta usisahau.

Nasikia Wema naye ameshabikia Hamisa kuitwa mchawi. Amesahau alivyodhalilishwa sauti yake akibembeleza penzi la Diamond, ilivyovujishwa au alivyotolewa nishai jukwaani na Diamond Mlimani City alipotaka kumtuza pesa. Uchawi hauna shabiki, haushabikiwi, hauna timu, punguzeni kiherehere jamani.

More From Mwanaspoti
This page might use cookies if your analytics vendor requires them. Accept