Godzilla kuagwa sehemu tatu kuzikwa Kinondoni

Thursday February 14 2019

 

By Rhobi Chacha

Dar es Salaam. Mwili wa mwanamuziki, Golden Jacob ‘Godzilla’ uenda ukaagwa sehemu tatu kabla ya kuzikwa kwenye makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Baba mlezi wa Godzilla, Antoni Kato amesema hapo awali walipanga bajeti ya mazishi milioni sita na nusu, lakini imeongezeka kuwa milioni nane kutokana na jana usiku saa nne baadhi ya wasanii kuomba aagwe Leaders msanii huyo.

Kato alisema familia ilipanga Godzilla aagiwe nyumbani kwao Salasala na baadae kanisani, lakini limejitokeza suala la wasanii wenzake kuomba aagiwe Leaders.

Hata hivyo Kato alisema leo jioni watakaa kikao kuamua kama itawezekana Godzilla mwili wake ukaagwa sehemu tatu ambazo ni nyumbani, kanisani na Leaders sababu watu wote wanaumuhimu kwake.

"Habari iko hivi, sababu Godzilla alikuwa mtoto wa Salasala, watu wa Salasala wameomba wamuagie Salasala, sasa kuna uwezekano tukafanyia Salasala tu, na suala la Leaders wasanii wenzake jana usiku walikuja kuomba, hili ombi tunalifanyia kazi, lakini kama ndugu wa karibu wakisema aagiwe Salasala tu tutamuaga Salasala, kwa sababu Salasala ndio ibada itafanyika hapo nyumbani.

"Si unaona huo mkanganyiko, ndio maana tunajaribu kuona kama ratiba itawezekana, tujipange tufanyie Salasala, halafu twende kwenye ibada na baadae twende Leaders tukimaliza hapo tunaenda Makaburi ya Kinondoni kuzika, sababu ni maeneo ya hapo hapo, ndio maana nasema bado tunalifanyia kazi na yote yawezekana tu na hatuwezi kumuuzi huyu tukamfurahisha huyu," alisema Kato.

Kato alisema yeye amemlea Godzilla tangu alivyokuwa na umri wa miaka miwili pindi alipofiwa na baba yake, hivyo kwa upande mwingine ni jirani yake.

Godzilla amefariki dunia usiku wa kuamkia Jumatano ya Februari 13, 2019 majira ya saa 10 alfajiri nyumbani kwao salasala jijini Dar Es Salaam, baada ya kusumbuliwa na Malaria pamoja na presha.

Advertisement