Fid Q: Eti nimezeeka,niwaachie vijana 'mic'

Muktasari:

Hata hivyo, haikuchukua muda mrefu kabla ya Fid tena kujikuta kitovu cha mvutano baina ya Tamasha la Wasafi Festival la Diamond Platnumz na Fiesta la Clouds FM, pale alipochagua kufanya kazi na Fiesta akiwapiga dongo Wasafi.

WANAZENGO buana hawana dogo. Baada ya kumsikiliza Fid Q kwa miaka mingi tangu alipotamba na ngoma yake ya kwanza ‘Huyu na Yule’ aliyoiacha mwaka 2000 akimshirikisha Mr Paul, wanaona sasa inatosha, apumzike, gemu awaachie kina Young Killer.

Lakini rapa huyo ambaye jina lake halisi ni Fareed Kubanda, analo jibu zuuri kwa ajili ya kila anayejaribu kumpiga zengwe.

“Napata sana ushauri wa watu wengi kuhusu suala la kuachana na muziki, ila niseme tu ushauri wao nitaukamilisha baada ya kumaliza kutoa albamu zangu nilizonazo maana nina albamu nyingi sana,” anasema.

Fid anayetamba na wimbo ‘Bam Bam’ aliowashirikisha Isha Mashauzi, Rich Mavoko na Big Jahman, anasema ipo siku ataacha kufanya muziki lakini siyo sasa kwani bado ana albamu nyingi ambazo inabidi azitoe kwanza ziishe.

“Ndiyo maana nimekuwa nikitoa nyimbo kila wakati japo zile za nyuma hadi leo bado ziko kwenye chati,” alisema rapa huyo ambaye alijikuta katika wakati mgumu baada ya ngoma yake ya ‘Fresh Remix’ aliyomshikirisha Diamond Platnumz kumfanya ashambuliwe sana katika mitandao na Team Kiba akituhumiwa na mashabiki hao kumpa nafasi Mondi amchane Ali Kiba katika mashairi ya wimbo wake huo.

Fid alijaribu kwa kila awezalo kuonyesha kwamba yeye si ‘team yeyote’ kati ya wakali hao wawili wa Bongofleva wanaoongoza kwa kupendwa nchini.

Hata hivyo, haikuchukua muda mrefu kabla ya Fid tena kujikuta kitovu cha mvutano baina ya Tamasha la Wasafi Festival la Diamond Platnumz na Fiesta la Clouds FM, pale alipochagua kufanya kazi na Fiesta akiwapiga dongo Wasafi.

Mvutano huo ulikuwa mkubwa ukiwajumuisha mameneja wa Diamond, ambapo Babu Tale aliandika katika ukurasa wake wa Instagram: “Nasikia hana gari na analelewa,” wakimtuhumu rapa huyo kuwa licha ya kufanya muziki kwa miaka mingi lakini hajaweza kununua hata gari.

Hata hivyo, Fid Q alimaliza malumbano hayo kwa kuwaomba radhi Wasafi.

Akizungumzia hip hop ya Tanzania ambayo amefanya kazi kubwa katika kuipa hadhi, Fid anasema muziki huo sasa una kipimo kipya cha ubora wa msanii.

Rapa huyo aliyetamba pia na wimbo uitwao ‘Kiberiti’ aliomshirikisha msanii wa nyimbo za asili, Saida Karoli, amesema kipimo kimojawapo cha sasa ni msanii kuangalia mauzo yake, licha ya kwamba sanaa hiyo inaweza kumpa pesa msanii ambaye hana uwezo kabisa tofauti na zamani.

“Kwa sasa kipimo cha msanii bora wa hip hop ni kuangalia mauzo yake, hip hop ya sasa inaweza kumpa pesa mtu ambaye hana kabisa uwezo, tofauti na zamani na ndiyo unakuta huyo anakuwa msanii bora kwa sababu anapata pesa nyingi kuliko wengine na sababu shoo zake zinajaza.”

Akizungumzia ndoa yake, Fid Q anasema anashukuru kwa sasa mwili wake umeongezeka baada ya kuoa, na pia amekata kiu ya mashabiki wake waliokuwa wakililia kila siku aoe.

Alisema: “Kwasasa niko sehemu salama na nashukuru tangu nimeoa naona mwili wangu unazidi kuongezeka na siyo mwili tu hata akili ya kutafuta imezidi kukua.

“Pia kwa upande wa mashabiki zangu nimefurahi sana kutimiza kile walichokuwa wakinipigia kelele kila siku kuwa wanataka nioe, sasa nishaoa na kinachofuata ni kama hivi kuwapa burudani bora ya kutosha.”

Fid ametimiza miezi mitano tangu alipofunga ndoa Januari 1, 2019 na mwanadada anayeitwa Karima a.k.a ‘Mama Cheusi’.