Fanya haya mwenza wako azidi kukupenda

Sunday September 23 2018

 

By Kalunde Jamal

Habari za muda huu wasomaji wa safu ya Anti K. Karibuni tena tuendelee kujuzana na kukumbusha mambo yatakayoboresha uhusiano wetu.

Licha ya kuwa hakuna mjuzi wa mapenzi aliyefaulu kwa asilimia 100 lakini ukiyapatia unaweza kupingana na wanaosema mapenzi karaha.

Kuyapatia mapenzi siyo jambo la ghafla wala la kufikirika, kunahitaji ufanye kazi uache kazi, hususani kwa wanawake ambao wanakabiliwa na kazi nyingi za kila siku, lakini pia wanapaswa kuwapa raha wenza wao.

Kama mwanamke kuna mambo kadhaa unapaswa kufanya, kubwa kuliko yote ni kuhakikisha mwenza wako hakuchukulii poa.

Namaanisha hasemi “ Tunaishi kwa mazoea”, ukiruhusu aseme hivyo ina maana muda si mrefu atakuchoka na mkichokana ndiyo hakuna ndoa hapo.

Ni sumu kuruhusu jambo hilo kwenye ndoa yenu. Kwa sababu akipata mtu mwingine ni rahisi kukusahau, atakuwa hana cha kupoteza wala cha kukumbuka kwako.

Haya mambo matatu unayopaswa kufanya ili msichokane na mwenza wako.

Usikubali kupitwa

Jifunze vitu vipya kila siku ikiwamo vya kimahaba. Asikuambie mtu urafiki kati ya mwanamke na mwanaume unaimarishwa na mapenzi na si vingine.

Kama kila siku utakuwa unakutana naye faragha kwa mazoea atatafuta sehemu ambayo atakatwa kiu yake.

Ikitokea akapata mahali anapokatwa kiu andika umeumia kwa sababu hawezi kurudi kwenye mapenzi ya kutafuta mtoto badala ya kuburudishana.

Mbali na kujifunza vipya vya kimahaba ambavyo ndiyo muhimu, unapaswa pia ujifunze mambo mbalimbali ikiwamo mapishi, kutunza nyumba, kusoma vitabu ili kujiongezea ujuzi, ilimradi usipitwe.

Jiamini ili akuamini

Hakuna kitu kinachomvutia mwanaume yoyote kama mwanamke anayejiamini katika kufanya uamuzi mbalimbali.

Ukijiamini na yeye atakuamini zaidi, kuliko ukiwa unajishtukia kwa kila jambo eti kila kitu lazima mwanaume afanye.

Wengine kuna japmbo dogo tu ambalo angaweza kulimaliza lakini hajiamini anakusubiri uje ufanye.

Pamoja na kwamba ni kitu cha kawaida, hata balbu ya umeme (taa) kama imeungua, haangaiki kununua wala kufikiria kuibadilisha zaidi kukusubiri. Kweli balbu! Lazima mwanamke ujiamini kwa mambo madogomadogo na hata makubwa japo haitapendeza kujiamini kwa kupitiliza.

Usisahau silaha ya mwanamke ni usikivu na huruma

Ili msikilizane na akuelewe hata kwa mambo magumu unapaswa uwe msikivu na mwenye huruma.

Huruma huanzia kwake, kwa jamaa zake, mwanaume yeyote anataka kusikilizwa, kuhurumiwa na kupendwa, kama utakuwa unamuona kama chuma “asiyechoka” unataka kila kitu afanye yeye atakuchoka.

Yapo mambo mengi yanayopaswa kufanywa ili kudumisha penzi kwa wenza, lakini hayo matatu ni muhimu pia.

Tukutane wiki ijayo tujadili namna ya kumteka mwanaume atulie nyumbani baada ya kazi.

Advertisement