Dude, JB wote wanachekana

Tuesday February 19 2019

 

By Rhobi Chacha

BAADA ya mchezo wa Simba na Yanga Jumamosi kumalizika kwa Yanga kufungwa bao 1-0, baadhi ya wasanii wametoa mitazamo yao.

Wengi wameonesha kuamini uwepo wa imani za ushirikina kutokana na matukio ya uwanjani siku ya mchezo.

Tukio la Yanga kuingia uwanjani ikitumia sehemu isiyo rasmi. Timu hiyo haikupita katika eneo maalumu ‘Tunnel’ ili kufika uwanjani na kukaguliwa. Wachezaji wa Yanga walipita nje na kuwaacha wa Simba pamoja na wale viongozi wa mchezo huo wakipita sehemu hiyo.

Matukio hayo na mengine yamewaibua wasanii mbalimbali wa Bongo, ambao wametoa mitazamo yao juu ya mchezo huo.

Aunt- Simba

Anashangaa timu yake imekufunga bao moja tu na kukosa mengine manne dhidi ya Yanga. Staa huyo ambaye marehemu baba alikuwa staa wa zamani wa Simba, Ezekeil Grayson, anasema mabao hayo hayakufungwa kwasababu ya Yanga kufanya mambo ya ushirikina.

“Kwanza nina furaha sana Simba kuifunga Yanga,ila kiukweli watani zetu wapunguze kuroga, haiwezekani Boko (John) yuko peke yake kwenye lango la Yanga ameshindwa kufunga lile goli. Hata Okwi (Emmanuel) amekosa mabao matatu ya wazi kabisa.”

Wema- Yanga

Mnyange huyu wa Tanzania mwaka 2016 anasema kama sio watani zao, Simba kuroga wasingeweza kuifunga timu ya wananchi Yanga. Wema anawaomba watani wao, wapunguze kuroga kwani kuna maisha baada ya mechi.

“Watani zangu Simba wafahamu kuna maisha baada ya mechi,hilo bao moja walilolipata ni kwa sababu ya kuroga. Maana bila ya hivyo ushindi ulikuwa wa Yanga.”

MwanaFA- Simba

“Yaani watani wametia fora, wanatutuhum sisi uchawi lakini siku zote mtu akimuhisi mwenzake mchawi, basi ujue wanaroga wote. Timu imeingia uwanjani kwa kuchepuka kuhofia ushirikina na bado ikafungwa. Wao ndio wameroga, Simba sio wa kufunga goli moja kwa mechi hii bana, ilikuwa zaidi ya moja.”

JB-Simba

Anasema hadi sasa haelewi kwanini Simba imefunga bao moja. Na kutokana na hilo, anawatupia lawama Yanga kwa ushirikina.

“Miye najiuliza tu watani wangu kulikuwa na haja gani ya kupita sehemu isiyohusika kwa kuhofia kurogwa ili wasifungwe? Sasa mbona wamefungwa? Hiki kitendo cha ajabu unaenda kuroga unapitiliza unajiroga mwenyewe sasa na matokeo ndio kama hayo Kagere (Meddie) kawatia aibu.”

Dude- Yanga

Anaamini Simba imepata bahati kufunga bao hilo moja. Na anasema kama sio ushirikina bao hilo lisingefungwa.

“Watani zangu wamepata bahati kwa kagoli kamoja. Nguvu yao ya ushirikina ndio imewasaidia sana. Haiwezekani kwa mpira wa Yanga ule waliocheza halafu washindwe kuifunga Simba.Tunajua tu kawaida yao huwa hawachezi mechi ya na Yanga hadi waende kwa sangoma.”

Mkude Simba)

Msanii huyu wa vichekesho naye hakubaki nyuma, kama jina lake la utani linavyosemeka, yeye ni mnazi wa kutupwa wa Simba.

“Yaani nimeamini uchawi upo. Simba wa kufunga bao moja? Siamini kabisa, hapa watani zangu (Yanga) watakuwa tu wamefanya mambo kwa sangoma haiwezekani kabisa.

“Tumewakosakosa mabao kama matano hivi. Ilikuwa Boko akifika lango la Yanga anaona makengeza,” alisema.

Advertisement