Diamond yulee tuzo za Grammy

Muktasari:

Mbali ya kuhojiwa na waandaaji tuzo kubwa za muziki za Grammy, kwa mwaka huu, tayari Diamond katajwa katika tuzo kubwa mbili ikiwemo ile ya African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) na African Entertainment Awards, USA (AEAUSA).

Dalili za kuwa msanii wa Tanzania, Diamond Platnumz kuingia kwenye tuzo za Grammy mwaka huu zimenukia.

Hii ni baada ya kuhojiwa na mtandao wa tuzo hizo duniani, ambazo wasanii wengi nchini wanatamani kufika huko.

Mahojiano hayo yaliyofanyika kupitia mtandao wa Googlemeet unaofanana utendaji wake kazi na mtandao wa Zoom.

Grammy wanafanya hivyo ikiwa ni siku chache tangu Diamond ashirikishwe katika wimbo wa Wasted Energy na msanii wa Marekani, Alicia Keys.

Katika mahojiano hayo, Grammy wamemuhoji msanii huyo anayefanya vizuri kwa sasa katika nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla mambo mbalimbali ikiwemo kuhusu historia ya maisha yake katika muziki, asili ya muziki wa bongo fleva na kolabo yake aliyoifanya Alicia Keys na mafanikio yake ya kuendelea kuwa msanii mkubwa katika kipindi cha miaka kumi mfululizo.

Akielezea kuhusu muziki wa Bongo Flava, Diamond alisema ni muziki wa aina ya Afrobeat, ambayo uhalisia wake unatokea Afrika Mashariki na una ladha fulani ya kiarabu kwa mbali.

Wakati kuhusu kuendelea kuwa msanii mkubwa kwa miaka kumi tangu alipoingia kwenye muziki, anasema siri ni kufanya kazi kwa bidii na kuwapa mashabiki kitu wanachokipenda.

Wakati kuhusu kolabo yake na Alicia Keys, amesema ilikuwa kipindi kabla ya kuzuka kwa ugonjwa wa corona, akiwa nchini Marekani, kwenye shughuli zake za kimuziki, Swizz Beatz ambaye ni mume wa Alicia na prodyuza mkubwa wa muziki alimpigia na kumtaka aende kuwatembelea.

Diamond aliendelea kueleza kuwa, alipofika huko alimkuta Alicia akiwa ndio anarikodi wimbo huo wa Wasted Energy ambao upo katika abamu yake mpya aliyoipa jina la ‘Alicia’ na kumtaka kuingiza ladha ya bongo fleva katika wimbo huo na hapo ndipo ilipokuwa chanzo cha kuimba na msanii huyo mkubwa duniani.

Ukiachilia mbali Grammy kumuhoji, kwa mwaka huu, tayari Diamond katajwa katika tuzo kubwa mbili ikiwemo ile ya African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA), ambapo ameingia katika vipengele sita akichuana na msanii mkali kutoka nchini Nigeria, Burna Boy.

Tuzo zingine ambazo katajwa hivi karibuni msanii huyo ni zile za African Entertainment Awards, USA (AEAUSA), ambapo ameingia katika vipengele vitano, ambazo zinatarajiwa kutolewa Desemba mwaka huu nchini Marekani.