Diamond amwaga ugali, Zari aapa kwa watoto!

Thursday April 25 2019

 

By Mwandishi wetu

KAMA noma na iwe noma ndio hii mwanangu. Supastaa wa Bongo Flava, Diamond Platinumz, baada ya kukaa na mambo mazito kifuani sasa kaamua kutema nyongo.

Yaani, mwenyewe anasema yapo mengine mengi ambayo ameyaficha chini ya moyo wake lakini, kwa haya aliyofunguka ikiwa ni mara ya kwanza tangu walipopigana chini na mzazi mwenzake, mama wa watoto wawili, Zarina Hassan a.k.a Zari, jamaa kamaliza kila kitu.

Juzi usiku kabla watu hawajapanda vitandani kulala Diamond alikuwa akitema cheche kwenye luninga ya Wasafi TV, ambayo anamiliki hisa akieleza vimbwanga vyote alivyokuwa akifanyiwa na mzazi mwenzake huyo wakati wakiwa kwenye mahusiano.

Zari na Diamond waliteka hisia za mashabiki wa Afrika Mashariki kutokana na uhusiano wao ambao, ungeishia kwenye ndoa lakini baada ya wakamwagana huku kila mmoja akificha sababu.

Hata hivyo, baadaye Zari alieleza kuwa sababu za kumwagana na Diamond ni staa kuendelea kuwa na karibu na mzazi mwenzake mwingine, Hamisa Mabetto ambaye naye alitikisa kwelikweli penzi la wawili hao.

Wakati Zari akifunguka hayo kwenye kituo cha BBC na katika mitandao ya kijamii Diamond alikuwa kimya akiendelea na shughuli zake, lakini jana akaona isiwe shida ngoja nifunguke.

Advertisement

Sasa iko hivi. Diamond ameeleza kuwa Zari hakuwa mwaminifu kwenye uhusiano wao na kwamba, alikuwa na mahusiano na wanaume wengine akiwemo pacha kutoka kundi la P Square, Peter na mkufunzi wake wa mazoezi.

Katika mahojiano hayo baadhi ya mashabiki wamedai kuwa, Diamond ana mkakati wa kuutangaza wimbo wake mpya wa The One, ambao ndio unatamba kwa sasa kwenye Youtube.

Alisema kuwa uhusiano wao umekuwa na misuguano mingi na kikubwa ni Zari, ambaye amekuwa akijificha kwenye kivuli cha upole akionekana kama mtu mtulivu, lakini kiuhalisi hakuwa hivyo hata kidogo.

Diamond alisema kuwa baada ya kubaini kuwa, Zari hakuwa mwaminifu hakuona sababu ya kuwa chini na kuamua kujirusha na wanawake wengine na hata kuzaa na Mobetto.

“Zari ni mtu ninayemheshimu sana kwa sababu amenizalia, lakini mwenzangu amekuwa na mambo mengi sana ya kisirisiri. Nakiri kuwa alikuwa amenizidi mapenzi ila nami nilikuwa na vitu vyangu vya kijinga nilivyokuwa nafanya. Lakini, kuna kitu aliwahi kunifanyia kibaya na alikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na Peter wa P-Square.

“Haikuwa siri kwa sababu nilishawahi kukuta meseji kwenye simu yake hata kabla hatujapata mtoto, aliacha simu na nilipoitazama nikaona aah si huyu ni Peter. Nilichukulia poa sababu nilikuwa na vitu nafanya,” alisema.

Diamond, ambaye uhusiano wake na Zari ulimalizwa kupitia ukurasa wake wa Instagram wa mama huyo wa watoto watano huku ukisindikizwa na picha ya ua waridi jeusi, alijigamba kuwa hajawahi kuachwa na mwanamke bali yeye ndio huacha.

Pia, alisema kuwa mwanamke anapomfanyia mambo ya ajabu basi humfanyia vitimbi na matukio kibao hadi mwenyewe anajiondoa kwenye himaya yake.

Kwa upande wake, Zari ambaye anaishi kwenye makazi ya Diamond nchini Afrika Kusini, alitumia ukurasa wake wa Instagram akimshangaa mzazi mwenzake huyo kwa kuamua kuongea uongo ili aendee kusikika.

Pia, alisema kuwa hajawahi kuchepuka nje ya uhusiano wake na Diamond na kwamba, kama aliwahi kufanya hivyo basi jambo baya liwatokee watoto wake.

“Mtu muziki wako umeanza kuishiwa nguvu sasa unaona kutumia jina la Zari ili uendelee kusikika. Sijawahi kuchepuka na kama niliwahi kufanya hivyo basi jambo lolote baya liwatokee wanangu. kKama mtu ameweza kuikana damu yake hadharani, kuna uongo gani mwingine ambaye atashindwa kuusema,” aliandika Zari.

Advertisement