Diamond: Sumbawanga mmenishinda jamani

Muktasari:

 

  • Tamasha la Wasafi Festival tayari limeshafanyika katika mikoa minne ikiwemo Mtwara, Iringa, Morogoro na Sumbawanga.

Dar es Salaam. Siku moja baada kudondoka jukwaani kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga mwanamuziki Diamond platnumz amewavulia kofia wakazi wa mkoa huo.

Diamond kupitia akaunti yake ya Instagram aliandika; Hakika mchezo usiuchezee… Sumbawanga mmenishinda tabia jamani.  Rayvanny, Mbosso Zanzibar! Zanzibar! tukutane Uwanja wa Amani siku ya Jumanne Desemba  11.’

Tukio la kuanguka jukwaani kwa Diamond lilitokea jana kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, wakati akiimba wimbo wa ‘Zilipendwa’ akiwa na wasanii Rayvanny na Mbosso.

Diamond aliyekuwa kifua wazi huku akiwa amevaa suruali yenye ufito mweupe pembeni, ubao uliokuwa umewekwa chini ulisogea na kujikuta anaanguka kwa kudumbukia chini ya jukwaa hilo, jambo lililozua gumzo mitandaoni.

Akizungumzia tukio hilo, Meneja wa Diamond, Babu Tale alikiri kuwa kilichoonekana kwenye video mtandaoni ndicho kilichotokea.

Tale amesema moja ya sababu ya msanii wake huyo kudondoka ni kutokana na kucheza kwa kurukaruka kwa nguvu jukwaani.

Meneja huyo ambaye alikuwa akijibu kwa mkato kila swali alilokuwa akiuliza, amesema kuhusu hali ya msanii wake huyo yumzima wa bukheri wa afya.

Onyesho hilo lilifanyika bure jana Jumapili baada ya siku ya Jumamosi kushindwa kufanyika kutokana na kunyesha mvua kubwa wakati Diamond akiwa jukwaani.