Bushoke, baba mtu waanzisha bendi

Muktasari:

Bushoke amepiga stori na MCL Digital na kusema kwa sasa wameanza kufanya shoo ya kutambulisha bendi yao kabla hawajafanya uzinduzi rasmi, na katika shoo hizo wanapiga nyimbo zote alizotunga Max Bushoke alipowahi kupitia bendi mbalimbali kipindi hicho na za Bushoke.

Mwimbaji wa muziki wa kizazi kipya, Ruta Bushoke na Baba yake mkongwe wa muziki wa dansi, Maxmillian Mathew Bushoke maarufu ‘Bushoke’, waanzisha bendi yao.
Bendi hiyo imepewa jina la 'Baba na Mama' imeanza kupiga katika kumbi mbalimbali za starehe hapa jijini  Dar es Salaam.
Bushoke amepiga stori na MCL Digital na kusema kwa sasa wameanza kufanya shoo ya kutambulisha bendi yao kabla hawajafanya uzinduzi rasmi, na katika shoo hizo wanapiga nyimbo zote alizotunga Max Bushoke alipowahi kupitia bendi mbalimbali kipindi hicho na za Bushoke.
"Hii ni bendi ambayo niko mimi, na Baba yangu, tumeanza kufanya shoo ya kuitambulisha kwanza bendi kabla hatujafanya uzinduzi rasmi, na katika shoo zetu tunazopiga kama vile ulivyoona tunapiga nyimbo zote alizotunga Max Bushoke alipokuwa bendi mbalimbali kipindi hicho na za kwangu nilizowahi kuimba," alisema Bushoke.
Aidha Bushoke amesema katika familia ya Max Bushoke ili kudhihirisha kuwa familia nzima ina vipaji vya kuimba, wameamua kumchukua Angel Bushoke ambaye pia ni mtoto wa Max Bushoke nae anaimba katika bendi hiyo.
Bushoke aliwahi kutamba na nyimbo kama Barua, Mume Bwege, Dunia Njia, Nalia kwa Furaha na nyingine nyingi.
Kwa upande wa Maxi Bushoke aliwahi kutamba na bendi  nyingi alizojiunga nazo, miongoni mwa hizo ni DDC Mlimani Park ambapo wimbo ‘Kiu ya Jibu’ ulimpandisha chati kabla ya kuimba nyimbo nyingine ukiwamo ‘Adinani Mandali’.
Wakati alipokuwa na bendi ya Bima Lee, alitunga na kuimba nyimbo nyingi, ambapo baadhi ya hizo ni ‘Visa vya Mesenja’ ambao kutokana na maudhui yaliyomo humo, hadi sasa upigwapo hudhaniwa kuwa ni mpya, kadhalika katika bendi ya Orchestra Safari Sound (OSS) alitamba na ‘Kata ya Maji Ukweni’.