Bella aukana muziki wa dansi

Muktasari:

  • Mkali huyo wa masauti, amefafanua yeye ni mwanamuziki tu na anafanya vitu bila kuchagua aina ya muziki na anapiga muziki anaouona unaofaa kwa wakati husika.

KAMA unadhani Mwanamuziki, Christian Bella anapiga muziki wa dansi, basi utakuwa umekosea ile mbaya.

Bella amefunguka yeye si mwanamuziki wa dansi kama wengi wanavyodhani bali ni mwanamuziki tu kwa jumla.

Mwanamuziki huyo raia wa DR Congo anawashangaa wanaomshambulia eti ametoka katika muziki wa dansi na kwenda kuimba Bongo Fleva.

Mkali huyo wa masauti, amefafanua yeye ni mwanamuziki tu na anafanya vitu bila kuchagua aina ya muziki na anapiga muziki anaouona unaofaa kwa wakati husika.

“Nachukizwa na watu wanaoniambia nimepotea kwa kwa kuimba Bongo Fleva na kuacha muziki wa dansi. Mimi ni msanii ninayefanya muziki ndani ya Tanzania, sio muziki wa Bongo Fleva, sio dansi, sio msanii wa taarab wala singeli,” alisema Bella.

“Kamwe usiseme Bella ni msanii wa dansi au Bongo Fleva, taarab au R&B, inatakiwa kusema Christian Bella ni mwanamuziki tu basi, inatosha.”

Bella alisema anafanya muziki wa kumfurahisha kila mtu bila ya kujali kama anapenda hip hop, Bongo fleva, dansi, taarab ndio maana anaitwa mwanamuziki na anaangalia wapi kwa muda huo muziki unawateka mashabiki.

“Yaani ninaangalia upepo wamuziki gani unavyobamba kwa wakati, na miye naenda nao sambamba ili mkono uende kinywani,” alifafanua.

Aidha Bella anasema mwanamuziki wa kweli hawezi kuimba dansi wakati anajua singeli ndio inawika. Au hawezi kuimba Bongo Fleva wakati taarab ndio inabamba, lazima atafeli na kuuchukia muziki.

Anabebwa na Akudo

Huko mtaani kuna madai eti Bella anatembelea nyota ya Bendi ya Akudo,ndio maana akipanda jukwaani na Bendi ya Malaika, anapiga nyimbo za Akudo Impact aliyokuwa akiitumikia zamani.

Mwanamuziki huyo anapangua tuhuma hizo na kudai hawezi kuimba nyimbo za Akudo wakati ana nyimbo nyingi nzuri zilizokubalika kwa mashabiki, mfano ‘Nakuhitaji’, ‘Rudi’, ‘Nani kama Mama’ na nyingine nyingi.

Bella anasema hata hao wanaomtuhumu kuimba nyimbo za Akudo, wajue ana haki ya kuimba nyimbo alizozitunga alipokuwa na bendi hiyo kama vile ‘Yako wapi Mapenzi’, ‘Bomoabomoa’ na ‘Safari Siyo Kifo’.

Bella anasisitiza Bendi ya Malaika ina nyimbo nyingi nzuri ambazo nyingine hawajawahi kuziimba. Na nyingine wameziimba na mashabiki wamezikubali.

“Hata nikiimba nyimbo za Akudo haziniathiri kitu, kwa sababu ninaimba nyimbo ambazo ni mali yangu. Ambazo nilizozitunga nikiwa huko na nina haki nazo,” anasema

Tofauti ya Congo na Bongo

Bella anasema Congo kuna vipaji vingi tofauti na Tanzania na bendi kubwa ni chache.

“Ukiwa Congo bendi kubwa ni chache, hivyo kama upo kwenye bendi ndogo ni vigumu kupata mafanikio.

“Pia, muziki wa Congo unaendeshwa na kusimamiwa na na wanamuziki Lakini hapa bendi nyingi ni za watu binafsi ambao si wanamuziki na hawajui muziki na ndiyo maana bendi hazifiki mbali ama hazitimizi malengo,” anasema Bella.

Tamaa ya kusaka mafanikio

Bella anasema katika safari yake ya muziki alikutana na changamoto nyingi lakini hakukata tamaa kwani lengo lake lilikuwa ni kupata mafanikio kama wanamuziki wakubwa wa Congo. “Nimepitia mambo mengi magumu ya kukatisha tamaa lakini nilipambana kwa lengo moja tu la kupata mafanikio kupitia kipaji changu cha muziki. Nilijua ni lazima siku moja nitatoka na kuwa mwanamuziki mkubwa.

“Nilianza muziki nikiwa na miaka 15 na nilikuwa kiongozi wa Bendi ya Chateau Du Soleil ambayo ilikuwa ya mtu mmoja aitwaye Frank ni rafiki mkubwa wa Marehemu Papa Wemba.

“Kabla ya hapo tulianzia tu mtaani kwa kujikusanya na kuimba tukiwa na Fally Ipupa ambaye baadaye alikwenda kwa Koffi Olomide ambako nilienda kuomba kazi nikiwa na miaka 16 nilikubaliwa lakini sikupewa nafasi ya kupanda jukwaani wala kuimba mahali popote.

“Kila nikienda nilikaa benchi tu kwani waliniona sina uwezo, wakati huo bendi kubwa zilizokuwa zinakubalika zilikuwa chache, hivyo ilikuwa vigumu lakini nilijipa moyo kuwa ipo siku nitapata nafasi, hapo tayari Fally Ipupa alikuwa ametoka,” anasema Bella.

Bella aliongeza: “Kwa sasa namshukuru Mungu kwa hatua niliyofikia ya mafanikio katika muziki, japo ninaendelea kupambana zaidi ili niyapite malengo niliyopanga.”

Bella hapendi hiki

Kuna vitu ambavyo Bella anavichukia kwa wanamuziki wenzake na wadau kwa jumla. “Kwa kweli sipendezwi na tabia ya wanamuziki kutopendana na kuoneana wivu usiokuwa na maendeleo. Yaani chuki, majungu, kufanyiana dharau.

“Sipendi kumchukia mwanamuziki bila sababu, eti kwa sababu tu tumepishana Kiswahili. Utakuta mwingine anamchukia mwanamuziki ambaye hajawahi kumkosea. Wapo wengine wanakuwa na chuki kwa sababu ya kuwashusha wanamuziki tu, kutokana na maneno yao ya kejeli na dharau.”

Bella anaongeza: “ Wanamuziki tuache kuoneana wivu na kukatishana tamaa. Tuwe na wivu wa kushindana katika kazi tutafika mbali zaidi.”

Bella anasema wanamuziki wanatakiwa kuwa na wivu wa maendeleo.

“Ukiona mwenzako katoka kwa staili fulani, basi na wewe jaribu kufanya hivyo, sio kuleta maneno ya kuchaguliana muziki wa kuimba,” anasema Bella.

Hii ndio mpango yake

Bella anasema bado anajipanga na anajua anafanya ‘show’ nyingi kuliko wasanii wote, hivyo hana haraka na kutoa nyimbo mpya. “Hapa Bongo mimi ndiye kinara wa kufanya shoo nyingi kuliko msanii yeyote, chunguza utalibaini.”