Asia Daruwesh : Mkali wa kinanda anayekumbukwa

Muktasari:

Miaka ya 1960 humu nchini kulianzishwa bendi ya kinamama watupu ikiitwa Women Jazz, ambao walikuwa wakitunga na kuimba nyimbo, wakipiga ala zote za muziki magitaa, saxophone, tarumbeta, tumba na nyinginezo, isipokuwa kinanda hakikuwapo wakati huo.

KWA wale waliokuwa wapenzi na mashabiki wa muziki humu nchini na pengine Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla, majina ya Asia Daruwesh, hayawezi muwa mageni kwao.

Anaweza kutajwa kama mpiga kinanda wa kwanza mwanamke kuwahi kutokea kwenye rhumba letu la Kitanzania.

Miaka ya 1960 humu nchini kulianzishwa bendi ya kinamama watupu ikiitwa Women Jazz, ambao walikuwa wakitunga na kuimba nyimbo, wakipiga ala zote za muziki magitaa, saxophone, tarumbeta, tumba na nyinginezo, isipokuwa kinanda hakikuwapo wakati huo.

Wasifu

Asia Daruwesh alizaliwa mwaka 1964, ingawa alikuwa na asili ya Zanzibar, maisha yake kwa kiasi kikubwa ameyaishi akiwa nchini Zambia kuanzia utotoni hadi alipokua.

Akiwa nchini humo, ndiko alikopata hamu ya kuwa mwanamuziki.

Kinanda chake kilisikika hapa kwetu Tanzania, kwenye safu ya mwanzo kabisa ya wanamuziki wa bendi Orchestra Double O. Bendi hiyo ilikuwa ikimilikiwa na kuongozwa na Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ mwaka 1984.

Kwenye bendi hiyo alikutana na wanamuziki wengine kina Mumba Kisi, Kapelembe Coco, Samba wa Mikalay, Zahoro Bangwe, Mohamed Idd Control, Matei Joseph na wengine wengi.

Darwesh alishiriki kupiga kinanda kwenye nyimbo kadhaa za bendi hiyo iliyokuwa ikitumia mtindo wa ‘Embalasasa Shika Breki’.

Baadhi ya nyimbo hizo ni Kinyume, Dodoma Capital, Njimina, Mimi na We, Kibwanange, Malalamiko na nyingine kadhaa.

Baadhi ya mashabiki wa muziki wa dansi walimpachika jina la ‘Super Mama’ kutokana na juhudi zake za kubofya kinanda kwa weledi mkubwa.

Hakuwa mchoyo wa ujuzi alionao kwakuwa katika nyimbo za ‘Lamanda’ na ‘Kitoto Chaanza Tambaa’, alimuachia abofye kinada mwanamuziki mwenzake Ally Hemed ‘Star’ ambaye hivi sasa ni mtunzi na mwimbaji maarufu mzuri wa taarabu katika kundi la Tanzania One Theather (TOT).

Hata hivyo, mwaka 1986 mwishoni Asia aliihama bendi hiyo na kujiunga kwenye safu ya mwanzoni ya bendi ya MK Group wakati huo.

Bendi hiyo wakati huo ilikuwa iikipiga muziki ghorofani katika ukumbi wa Bandari Grill katika hoteli ya New Afrika iliyokatikati ya jiji la Dar es Salaam.

Asia Darwesh alibofya kinanda katika takribani nyimbo zote za kuanzia toleo la kwanza hadi la tatu za bendi hiyo ya MK Group.

Super Mama kipindi chote alikuwa akipendelea kuvaa suruali, huku nywele zake zikiwa zimenyolewa katika mtindo wa Panki.

Katika bend hiyo walikuwepo wapiga magitaa kina Joseph Mulenga ‘King Spoiler’ akilicharaza gitaa la solo, Omari Makuka kwa upande wa rythm, Kawele Mutimanwa akipiga gitaa la rythm na solo na baadaye aliingia Miraji Shakashia, alikuwa kipiga gitaa la solo, wakati huhuo akiwa bado mwanafunzi wa shule ya msingi.

Mwaka 1989 Darwesh alikuwa miongoni mwa wanamuziki wanne walioihama MK Group na kwenda kuasisi bendi ya Bicco Stars.

Akiwa na bendi hiyo aliungana na wanamuziki wengine kina, Ramadhani Kinguti ‘Systeme’, Fresh Jumbe, Athuman Cholilo Mashida, Seif Rengwe, Sidy Morris ‘Super Konga’ aliyekuwa akizidunda tumba, Mafumu Bilal ‘Super Sax’ akipuliza tarumbeta.

Pia alikuwapo muungurumishaji wa gitaa zito la besi Andy Swebe Ambassador’ na wengine wengi.

Asia Darwesh alionyesha ni jinsi gani yeye ni mwanamuziki aliyebobea baada ya kutunga wimbo wake kwa mara ya kwanza wa “Bwana Kingo” pia akashiriki kikamilifu kuimbisha wimbo huo.

Mwaka 1992 alianzisha bendi yake mwenyewe akiita Zanzibar Sound, ikitumia mtindo wa Wesaka Dance. Katika bendi hiyo alishirikiana na kina Bob Gad William, Hezron Ludala ama Bob Ludala, Fariala Mbutu, na baadaye wakajiunga kina Mohamed Idd Control na Shaban Lendi.

Wimbo Banana ambao baadaye Bob Gad alikuja kuurudia akiwa na Twanga Pepeta ulirekodiwa kwa mara ya kwanza na bendi hii.

Aidha, wimbo wa Hadija ambao Fariala Mbuttu, alikuja kuurudia akiwa katika bendi ya Kilimanjaro Connection, ulirekodiwa nao huku Bob Rudala akiwa mwimbaji kiongozi.

Kufariki dunia kwa Asia Darwesh mwaka 1995, ndiko kulikohitimisha safari ya bendi hiyo.

Mungu aipumzishe roho yake pahala pema peponi, Amina.

Makala haya yameandaliwa kupitia vyanzo mbalimbali.

Mwandaaji anapatikana kwa namba: 0713331200, 0736331200, 0767331200 na 0784331200.