Aa!Ray wa Tambwe anawaza pesa tu

Saturday June 1 2019

 

By Doris Maliyaga

KILA mfuatiliaji wa soka la Bongo atakuwa anamfahamu Amissi Tambwe. Jamaa anakipiga Yanga mwaka wa tano sasa amekuwepo nchini tangu 2013, ambapo alianza kwa kucheza na Simba kuanzia mwaka huo mpaka mwaka 2014 alipohamia kwa watani wao wa Jangwani.

Jamaa amekuwa akicheza kwa kiwango ingawa kwa sasa anasuasua kiasi kutokana na majeraha.

Ukimuona Tambwe uwanjani, akifanya yake, usifikiri anafikia hatua hiyo hivi hivi tu, nyuma ya mchezaji huyo kuna mrembo ambaye ni mkewe anayekwenda kwa jina la Raiyan Mohammed, maarufu kama Ray wa Tambwe.

Dada huyu ambaye amefunga ndoa na Tambwe mwaka jana ndiye kichocheo cha mafanikio ya mume wake. Na mara kwa mara amekuwa akianika kwamba siku zote amekuwa mstari wa mbele kuhakikikisha mume wake anafanya vizuri.

Maisha Dar

Dada huyo ni Mtanzania mwenye asili ya Kiarabu. Mama yake anatoka mkoa wa Mbeya na baba yake anatokea Uarabuni.

Advertisement

Raiyan, tangu aanze maisha na Tambwe wana zaidi ya miaka mitano na wamebahatika kupata mtoto mmoja anayeitwa Ayman.

Tambwe anatokea Burundi, lakini hilo halimpishida kwa kuwa anafahamu kwamba mpira una mwisho na kuna siku watahamia Burundi.

“Ninampenda mume wangu na nipo tayari kuishi kwao mpira wake utakapoisha. Nimeshachagua maisha ya Burundi.

Hatma ya Tambwe Yanga

Hakuna asiyejua kwamba Yanga msimu huu imeyumba kifedha. Na kama viongozi wapya wasipojipanga watashindwa kuongezea mkataba baadhi ya wachezaji au wakashindwa kukidhi mahitaji yao. Kuhusu hilo anasema;

“Usajili wake ndiyo utatufanya tujue mpango mzima hapa Tanzania, ikishindikana tutahama nchi. Hata hivyo, mipango yote hiyo itategemea maslahi katika suala zima la usajili,” alisema Raiyan ambaye anaamini mumewe ana uwezo mkubwa wa kucheza mpira na kinachomrudisha nyuma ni nafasi ya kucheza.

“Mwanzo alikuwa majeruhi lakini kwa sasa hapati nafasi ya kucheza na anapopangwa kucheza si unaona anachokifanya uwanjani. Hata hivyo, rekodi ya Tambwe msimu huu si nzuri kwa sababu amecheza mechi chache na nyingi anaingia kama mchezaji wa akiba.

Biashara

Raiyan, ambaye ana asili ya Uarabu, hataki kabisa kutulia nyumbani na kusubiri mume wake amletee kila kitu. Ameamua kujishughulisha ili kuingiza kipato. Amegundua ana kipaji cha upishi, anakitumia. Raiyan amekuwa akifanya biashara ya kuuza vyakula mbalimbali kwa watu wa matabaka tofauti. Kati ya vyakula vyake, kinachopendwa zaidi ni biriani na amekuwa akipata oda nyingi zaidi siku za Ijumaa. Ukiachana na biashara hiyo, amekuwa akiuza mikoba ya wanawake. Amekuwa akijitangaza katika mitandao na kisha kupokea oda kutoka kwa watu tofauti.

Advertisement