Kilichomuua Mabera hiki hapa, kuzikwa Goba leo

Muktasari:

Mabera ameacha historia kubwa katika muziki wa dansi ambapo tofauti na wasanii wengine ambao wamekuwa na tabia ya kuhamahama bendi, yeye ameweza kudumu kwa miaka 48 bila kuhama Msondo  Ngoma tangu alipojiunga nayo mwaka 1972.
 

MABERA Said ambaye ni mtoto wa mwamuziki Said Mabera, ameeleza kilichogharimu uhai wa baba yake aliyefariki usiku wa kuamkia leo Jumanne, Septemba 29, 2020.

Akizungumza na Mwanaspoti Digital, Said amesema baba yake alifariki baada ya kupata presha ya kupanda.

Amesema ni muda sasa wamekuwa wakimuuguza baba yao kwa ugonjwa huo lakini jana Jumatatu saa 11 jioni hali yake ilibadilika na kulazimika kumpeleka hospitali ya Masana iliyopo Tegeta kwa matibabu zaidi.

Hata hivyo amesema baada ya kufika saa 3 usiku,  hali yake iliimarika na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

“Tukiwa nyumbani baada ya masaa kama mawili hivi hali yake ilibadilika tena presha kupanda na hapo ndipo umauti ulipomkuta wakati tukiwa tunafanya utaratibu wa kumrudisha hospitali,” amesema Said.

Kuhusu mazishi ya baba yake, mtoto huyo amesema baba yake anatarajiwa kuzikwa leo Jumanne saa 10 makaburi ya Goba jijini Dar es Salaam.

Moja ya sifa alizokuwa nazo Mabera katika muziki wa dansi tofauti na wasanii wengine ambao wamekuwa na tabia ya kuhamahama bendi, yeye alidumu kwa miaka 48 bila kuhama Msondo  Ngoma tangu alipojiunga nayo mwaka 1972.

Akiwa huko alishiriki kutunga nyimbo mbalimbali na kupiga gitaa la solo ambalo ndilo lilimpa umaarufu katika muziki wake.