ROGART HEGGA: Katapila lililopitia mengi katika dansi

WATU wa burudani ya muziki wa dansi wengi wanajiuliza Rogart Hegga Katapila yuko wapi na anafanya nini kwa sasa?

Mwanaspoti limemtafuta Rogart Hegga ambaye amewahi kupitia bendi nyingi zikiwemo Mchinga Sound, African Stars ‘Twanga Pepeta’ T.O.T Plus, Ruvu Stars na kugundua kuwa hivi sasa yupo na bendi ya Sayari Stars yenye makazi yake Manzese TipTop, Dar es Salaam.

Rogert ni miongoni mwa wakongwe wa muziki wa dansi kulingana na historia yake ambapo akiwa Twanga Pepeta aliwahi kutunga nyimbo kama Fadhila kwa wazazi no.1, Lightnes, La Mgambo, Family conflict, Kauli na Rafiki adui, anasema kitu kinachokwamisha muziki wa dansi Bongo ni ujanjaujanja wa watu wachache wanaotumia nafasi ya mfumo mzima wa kusimamia sanaa na muziki kwa ujumla wake kuanzia kwenye shina.

Anasema wanapenya kwenye ule upungufu hususan kutosimamiwa kikamilifu kwa baadhi ya sheria zinazolinda haki na miiko ya muziki. Hivyo huwafanya wanamuziki kutotambua thamani yao hatimaye kukosa umakini.

Kutokana na uzoefu wake, Rogert ambaye pia katika bendi ya Mchinga sound alitunga nyimbo kama Fadhila kwa wazazi no.2, Nafsi, Katapila na Sifa inaua, ametaja kitu ambacho kikifanyika muziki wa dansi utakuwa na nguvu kubwa kama ilivyokuwa miaka iliyopita.

“Kwanza wanamuziki wa dansi tutambue maisha yamebadilika, tuanzishe utamaduni wa kuambiana ukweli na kutambuana huyu ni nani na anastahili kuishi naye vipi, na hilo litakuwa na wepesi kwa kuunda umoja fulani, humohumo ndipo tutang’amua mengi ikiwemo wapi tuliteleza, wapi tulipuuzia ambapo wenzetu wakatumia fursa (ya kujinufaisha,” anasema.

“ Unajua binadamu hatujakamilika, hasa ukivuka nafasi fulani katika maisha, iwe kusifiwa au uwezo wa kipesa, hapo ndipo wengi hushindwa kuhimili mikiki ya majaribu, mbaya zaidi wengine hukimbilia kuwaamini watu hao pasipo kujua uzito wa udhaifu wao.

“Sasa dawa yake ni kuwa na umoja wa kuambiana ukweli na kupeana miongozo inaweza kusaidia muziki wa dansi kurudi kwenye nafasi yake.”

Kwanini nyimbo za zamani zinapedwa kuliko za sasa?

Rogart anazungumzi watunzi wa nyimbo wa sasa wanakoposea akisema kwenye shoo za baadhi ya bendi huwa wanapiga nyimbo za kukopi na mashabiki huonyesha kuzielewa kuliko nyimbo zao wenyewe za bendi husika.

“Ninaloliona mimi ni ukiona wimbo watu wanaupiga kwa kukopi ujue ni chaguo la wengi, unatajwatajwa, umetendewa haki, ni mzuri. Sasa tunachotakiwa ni kuzifuatilia hizo nyimbo kujua walioshiriki walipita njia zipi,” anasema.

Badi Bakule, Khadija Kimobiteli ndani ya Sayari

Rogart ambaye katika bendi ya Sayari yupo na wanamuziki waliopata kutamba kitambo katika uimbaji kama Badi Bakule, Khadija Mnoga, Ramadhan Kitambi na kwenye drums yupo Emma Chokolate, anasena sio wanapiga tu ‘copy’ ya nyimbo walizotunga katika bendi walizokuwepo awali, bali wameshatunga nyimbo mpya.

Anazitaja kuwa ni pamoja na ni ‘Nipe leso’ ‘Pete ya ndoa’ na ‘Nipe raha’ zilizotungwa na Badi Bakule na ‘Mfa maji’, ‘Sprit Remix’ ‘Jicho la tatu’ ukiwa ni utunzi wake.

Kwa watu wa burudani ya muziki wa dansi, hakuna asiyejua kama Rogart ni mwanamziki hodari na ni mtunzi mzuri wa nyimbo na hadi sasa baadhi ya bendi zinaendelea kutamba na nyimbo alizotunga akiwa kwenye hizo bendi.

Utunzi na kisa kilichotokea

Kuna watunzi wa muziki baadhi yao hupenda kutunga wimbo ambao wakikaa wanasema kweli wimbo huo walifanya kazi ya ziada na je kisa cha wimbo huo kilikuwa cha kweli au ni hadithi tu? Kwa Rogart analezea, “nyimbo iliyonikaa rohoni ni Spirit niliyotunga nikiwa Ruvu Stars Band. Kilichonipelekea kutunga ni namna thamani yako pale utapoitambua itavyokuingiza kwenye misukosukoni,” anasema.

“Utajengewa kila namna ya hila, ukakosa amani hapo ulipo. Kwa kuwa yamenikuta nikaamua kutunga hii nyimbo, kwamba kila mtu ana maana yake tangu kuzaliwa kwake, na kipo kiwakilishacho kipawa chake hapa duniani kwani lipo lengo Mungu alilokuletea.”

Anasema, “ipo siku watakutafuta kama Mwalimu Nyerere, watakusaka kama madini ya thamani, watakulilia kama Yesu Masiya.”

Kuna kipindi wanamuziki Rogart, Adolf Mbinga, Tx Moshi William, Suleiman Mbwembwe na Salehe Kupaza walikuwa na kundi lao waliloliita TFG na walifanikiwa kurekodi nyimbo baadhi zikiwa ni Mama Ife, Zamaradi na Bwana Kijiko remix, hata hivyo kwa nini hawakuwahi kutoa albamu?

“Unajua hili ‘group’ liliasisiwa na mzee Mwendapole (marehemu) baada ya kufanya ‘recording’ hiyo kukatokea kutokubaliana mambo fulani baina yake na mmiliki wa bendi fulani akidai isirekodiwe nyimbo fulani, akidai ni ya bendi yake. Baada ya hapo tukabaki njia panda,” anasema.

Kondoka Twanga

“Unajua kuna msemo usemao nabii hakubaliki kwao. Nimefanya mengi sana Twanga Pepeta na ndio maana wakanibatiza jina la Katapila, we’ mwenyewe unajua hadithi ya Katapila ikoje. Kifupi nimepisha damu changa nao waje na mapya.”

Aliwahi kupata misukosuko huko

Akiwa Twanga Pepeta, anasema aliwahi kupata misukosuko.

“Unajua kwenye safari ya maisha mnapoanzisha harakati fulani hutokea mitihani mingi sana, na kama hakuna mkono wa Mungu mnaweza kuishia njiani,” anaanza kusema.

“Sasa mimi wakati fulani ndani ya bendi kabla hatujabatiza mtindo wa Twanga Pepeta tulipitia vipindi vigumu vyenye mitihani, ukisimuliwa huwezi amini, tena utasisimka, hapo ndipo utakubali kwamba ukipata misukosuko mingi ujue kuna neema kubwa ndivyo ilivyokuwa Twanga mwanzoni.

“Katika misukosuko hiyo mimi nilihusika sana kuipangua kiushauri, wachache sana wanalijua hilo akiwemo Deo Mwanambilimbi mkimfuata atawafafanulia zaidi.”

Banza Stone, Ally Choki

“Banza Stone na Ally Choki walichangia sana katika harakati zetu za kupokea vijiti tulivyoachiwa na wakubwa zetu, kwanza ubunifu wao na kujituma kwao ukijumlisha na ule upinzani wao waliweka hatua nzuri katika muziki wa dansi”

Akimzungumzia Banza Stone, anasema,“ninachokikumbuka kwa Banza Stone (marehemu) alikuwa mtundu sana katika ubunifu. Banza alikuwa na vipaji vingi kama vile kucheza, kurap, kuimba na vingi vingi sana. Alivikusanya pamoja na kuviingiza katika dansi na kulipa heshima, Banza andelee kupewa heshima.”