NO AGENDA: Irene Uwoya, waandishi wa sandakalawe

Sunday July 21 2019

 

By Luqman Maloto

MAMBO mengine usitumie mzani mkubwa kuyapima. Kama hili la supa mrembo, Irene Uwoya kuwachezesha Waandishi wa Habari Sadakalawe, halihitaji kipimo kikubwa cha tafakuri.

Waza; kina nani hupewa fedha kama Irene alivyowapa Waandishi? Unapata jibu kuwa wasanii majukwaani hutuzwa kwa namna hiyo. Mtu mwenye noti zake anasimama mbele kisha anammiminia ‘minoti’ msanii.

Majukwaa ya muziki wa dansi ni kawaida. Tena yule anayekwenda kumwaga fedha huimbwa na kushangiliwa. Wanamuziki, kwa maana ya waimbaji, wapiga vyombo na madansa huwa hawaoni wanadhalilishwa.

Katika ‘pati’ zao za besidei na nyingine, wasanii hutuzana hivyo. Mwenye jeuri yake anakata noti nyekundu za BOT au Benjamins za Donald Trump, anammiminia mhusika na hakuna anayeona amedhalilishwa.

Sasa basi, kwa vile ubongo wa Irene hauna uwezo mzuri wa kuchanganua mambo, akaona vile wao wasanii hutuzwa, anaweza kumtuza mtu yeyote. Tatizo linaanzia hapo.

Unadhani Irene kwenye kichwa chake alikusudia kuwadhalilisha Wanahabari kwa kuwarushia noti za elfu kumikumi? Ukifikiria hivyo, eti alikusudia kuwadhalilisha, utakuwa humjui Irene.

Advertisement

Ukimfahamu Irene, utaelewa kuwa shida ipo kwenye kuchanganua mambo. Shida ni namna ya kufikiri. Jinsi ubongo unavyofanya kazi. Angejua ni kosa asingethubutu. Angeambiwa kitendo alichotaka kukifanya si kizuri, asingefanya.

Irene aliomba msamaha baada ya kuzongwa sana. Pamoja na hivyo, inawezekana hata baada ya kuomba radhi bado hajaona kosa lake. Inawezekana huwa analalamika kwa marafiki zake kuwa anaonewa, kwani hakukosea chochote.

Tena anaweza kusema: “Sasa pale nilikosea nini? Mbona kwenye bendi huwa tunatuza hivyo na haiwi tatizo?” Nimetangulia kusema kuwa shida ipo kwenye namna ya kufikiri. Yaani jinsi ubongo unavyofanya kazi.

TUMWONYESHE KOSA!

Wasanii kwenye bendi huwa hawachezeshwi sadakalawe. Mtu mwenye fedha anamfuata mtu husika, anamrushia pesa, wakati huo anayetuzwa anaendelea kuwajibika.

Hata zikimwagwa katikati maana yake zinakusanywa, wahusika watagawana baada ya hesabu kufanyika. Zaidi, wanamuziki jukwaani ni waburudishaji, hivyo jinsi ambavyo hupewa pesa hutafsiriwa kuwa sehemu ya burudani.

Kwamba, shabiki anakunwa na kazi inayofanywa na msanii au wasanii jukwaani, anakwenda kutoa tuzo ya fedha. Burudani inaongezeka hapo. Na wasanii wakiondoka bila kutuzwa huona ni hasara. Maana ni sehemu ya vipato vyao. Vilevile ni kipimo cha kufanya kazi bora yenye kugusa hadhira. Mwandishi wa Habari anapokwenda kwenye mkutano kuchukua taarifa, anakuwa kazini. Mwandishi wa Habari si mburudishaji kusema unaweza kummiminia noti kwa fujo, halafu burudani inoge.

Muhimu zaidi ni kuwa hakuna Mwandishi wa Habari anayetegemea mikutano ya habari ili kuishi. Itisha mkutano, toa taarifa zako, ondoka. Kama ni taarifa yenye mashiko, itaripotiwa.

Waandishi wa Habari wameajiriwa, hivyo wanatakiwa kufanya kazi ili kutetea ajira zao. Hawawezi kuacha habari yako, eti kisa hujampa pesa, wakati ofisini kwake anadaiwa habari. Hata ambaye hajaajiriwa, anategemea kuripoti ndipo alipwe. Ataiachaje habari yako yenye kufaa wakati anajua itamfanya apate kipato ofisini?

Ni utaratibu ambao umezoeleka wa wadau wa habari kuwapa posho waandishi wanapowaalika kwenye mikutano yao. Hata hivyo, haijawahi kuwa lazima. Haijatamkwa wala haipo hivyo, kuwa bila pesa habari yako hatairipotiwa.

Inawezekana kuwepo kwa Mwandishi kuficha habari nzuri kwa vile hajapewa pesa. Hiyo habari ikiripotiwa na vyombo vingine, ataulizwa mbona yeye hakuiripoti?

Hivyo, kwa kufafanua kosa la Irene ni kuwa alifanya kama ambavyo shabiki hupandwa na mzuka ukumbini na kuanza kuwamwagia pesa wanamuziki. Sasa sijui Irene ule mzuka mbele ya Waandishi wa Habari ulitokana na nini? Waandishi walimburudisha nini? Au zile kamera na maikrofoni?

Mzuka wake ulipandishwa na pesa kwenye pochi, akaona azifanyie shoo? Kosa kubwa la Irene ni kuwafanya Waandishi wa Habari wacheze sadakalawe. Waanze kugombea noti za Shilingi elfu kumikumi.

Ifahamike kuwa, sadakalawe ni tofauti na utuzaji wa majukwaani. Watuzaji majukwaani humwaga fedha kwa walengwa, hivyo wahusika baada ya shoo huzikusanya au wasaidizi wao huwasaidia kukusanya.

Sadakalawe ni mtu kuwa na fedha au vitu vya thamani. Mbele yako wanakuwa watu wengi. Unaamua kurusha atakaepata apate, wa kukosa akose. Michezo ambayo hufanyiwa watoto. Huwezi kukusanya watu wazima uwachezeshe sadakalawe.

Alichokifanya Irene kilikuwa ni sadakalawe. Akawarushia fedha Waandishi bila mpangilio, kwa hiyo mwenye nguvu akusanye nyingi, dhaifu aambulie patupu. Nasikia mpaka kamera zilivunjwa sababu ya waandishi kusukumana.

Hivyo, Irene kama hajui kosa lake, alielewe kuwa kumchezesha sadakalawe mtu mzima sio ustaarabu. Mtu ambaye umemwalika kwa heshima aripoti habari yako halafu unamchezesha sadakalawe, ni ukosefu wa uungwana.

WAANDISHI WALIBUGI

Kazi ya uandishi wa habari ina misingi na maadili yake. Mwandishi mwenye kukubali kuchezeshwa sadakalawe kama mtoto asiyejitambua hilo ni tusi kubwa kwa fani aliyochagua kuitumikia.

Watu wanaponda kuwa waandishi wana njaa. Sikatai, kwani nani ameshiba? Mbona wenye kuonekana wana neema nyingi ndio ambao wanapelekwa mahakamani kwa wizi na uhujumu uchumi?

Sasa basi, tatizo sio kutosheka, bali kujiheshimu. Inawezekana walikuwepo wana habari waliokataa udhalilishwaji wa kugombea pesa, nao wakajikuta wanapigwa vikumbo na waliozitaka elfu kumikumi. Tusisasahau kuwa samaki mmoja akioza wanaoza wote.

Ingetokea Irene anarusha pesa halafu waandishi wangesimama bila kuzichukua, palepale Irene angejua amekosea na kusitisha kuendelea kutoa. Kwa vile aliona zinagombewa, akaona sadakalawe imepokelewa vizuri. Akaendelea.

Waandishi wajiheshimu. Kama wameingia kwenye fani ili wapate pesa, wamechemka. Msingi wa kwanza wa taaluma ya habari ni huduma. Na ili huduma yako iwe na thamani lazima ujitenge na kuonekana unanunulika.

Waandishi waliocheza sadakalawe ya Irene walionesha kuwa wananunulika. Kama elfu kumikumi ziliwatoa thamani kiasi kile, wakiwekewa mabulungutu ili wapindishe huduma zao watakataa? Nani atawaamini kama wanaweza kukataa?

Vyombo vya Habari lazima vitengeneze mfumo bora wa kimaadili kwa waandishi wao. Kila taasisi iunde misingi (values). Wajue kuhusu karata za nje na ndani (outer and inner cards). Karata ya nje ni jinsi ambavyo mwanahabari anapaswa kuwa nje ya ofisi. Akiicheza vibaya karata nje, anaharibu heshima ya taasisi na taaluma kwa jumla.

Mfano, waandishi waliocheza sadakalawe ya Irene, waliitumia vibaya karata ya nje, hivyo taasisi wanazofanyia kazi zimedhalilika na taaluma yote. Waandishi wote tunaonekana walewale.

Karata ya ndani ni ufanisi kazini. Tatizo wengi huzingatia sana karata ya ndani kwa vile ndio inaleta matokeo, wanasahau kwamba matumizi bora ya karata ya nje ndio hujenga thamani ya taasisi na taaluma kwa jumla.

Hivyo, tatizo la sadakalawe ya Irene lipo kwenye ubongo. Irene hakuchanganua vizuri na kujua kosa alilofanya. Waandishi pia ni ubongo, elfu kumikumi ziliwapofusha uwezo wa kufikiri, matokeo yake wamefedhehesha taasisi zao na taaluma kwa jumla.

Advertisement