Baba Kaila anogesha utamu ZIFF 2018

Monday July 9 2018

 

By RHOBI CHACHA

ASIKUAMBIE mtu Shetta a.k.a Baba Kaila anaijua kazi yake. Msimu wa 21 wa Tamasha la Kimataifa la Filamu Zanzibar (ZIFF) juzi Jumamosi lilizinduliwa rasmi visiwani hapa na moja ya wasanii waliopata bahati ya kutia baraka zake ni mwimbaji huyu wa kizazi kipya.

Mkali huyo alikinukisha katia usiku mwingi kwa nyimbo zake matata, huku awali akiwapa fleva wahudhuriaji kwa shoo yake matata na kuwafanya mashabiki kusahau kama ulikuwa usiku mwingi na kupagawa.

Mwanaspoti lililotimba visiwani hapa kushuhudia uzinduzi huo linakudondoshea kwa uchache utamu ulivyokuwa kwenye viunga vya Ngome Kongwe.

UZINDUZI ULIVYOANZA

Tamasha hilo linalofanyika kila mwaka lilizinduliwa kwa shamrashamra za aina yake ambapo mbele ya umati wa wageni waliohudhuria kutoka ndani na nje ya Zanzibar, Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF, Mahmoud Thabit Kombo, aliwashukuru wote.

Kombo alisema anawashukuru wanaoliunga mkono tamasha hilo lililoanzishwa miaka 21 iliyopita na kuzidi kujizoelea umaarufu mkubwa Afrika kwa jumla kutokana na ukweli tamasha hilo linajumuisha wasanii na nwanamuziki wa kimataifa.

WAZIRI ANOGESHA

Licha ya Kombo kusema kuwa, tamasha hilo linatumika kuitangaza vyema Zanzibar lakini bado jitihada zaidi zinahitajika katika kulifanya liwe bora zaidi.

Alisema uchache wa fedha umewalazimu hadi wajumbe bodi yake kutoa fedha mifukoni mwao ili kuhakikisha tamasha linafanyika.

Ndipo aliyekuwa mgeni rasmi wa uzinduzi wa tamasha hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Issa Haji Ussi ‘Gavu’ kukiri Serikali ya Mapinduzi Zanzibar bado haijawatendea haki wasanii wengi visiwani hapa.

Gavu aliyema ipo haja kwa Serikali kusimamia kazi za wasanii pamoja na utafutaji wa soko la kazi za wasanii. Na kudai tamasha hilo ambalo kwa miaka mingi limekua likifanyika bado linaendelea kukabiliwa na changamoto za hapa na pale.

Akitaja changamoto hizo ni pamoja na ukosefu wa udhamini wa uhakika kila msimu wake ukikaribia na alisema atabeba jukumu la kuhakikisha Serikali inakaa na kutafakari njia ya kuandaa udhamini bora kwa lengo la kulitendea haki tamasha hilo.

“Nipo tayari kuhakikisha Serikali inawapiga tafu kwa kuona tamasha linapata wadhamini wa uhakika,” alisema Waziri Gavu.

MZUKA WA SHETTA

Kama ilivyo kawaida ya tamasha hilo kuchanganya masuala ya filamu na muziki, juzi katika uzinduzi huo kulikuwa na burudani bab’ kubwa ambayo iliwapa mzuka wapenzi na mashabiki waliohudhuria kushuhudia uhondo.

Ile kuanza tu, tamasha liliachia filamu matata iitwayo ‘Bahasha’ iliyowavutia wengi na hasa kuonyesha kwenye skrini kubwa na kuwafanya watu wajione kama wapo jumba la sinema.

Filamu ambayo ilipata bahati kufungua, kwani siku zote huwa zinafungua filamu za nje ya nchi kwa lengo lakuangalia filamu yenye ubora.

Mbali na filamu, pia tamasha hilo lilipambwa na burudani za ngoma, bendi na muziki ambapo Mwanamuziki Sitti na bendi yake yenye makazi yake Zanzibar, ilitumbuiza kwa kukata utepe, kisha kufuatiwa na Kikundi cha Maulid ya Home pia kutoka Zanzibar eneo la Mtendeni.

Ndipo usiku mwingi wakati tamasha likikaribia kufungwa ili watu wakakusanye nguvu ya kesho yake yaani jana Jumapili, ikawa zamu ya Shetta ‘Baba Kaila’ aliyeangusha shoo bab’ kubwa.

Shetta alianza kwa kuimba wimbo wake wa Mdananda, kisha kufuatiwa na Kelewa na kumalizia na kitu matata cha Vumba, huku shoo yote ikienda sambamba na amsha amsha za aina yake watu wakisahau matatu yao.

UHONDO MTUPU

KIlichofanyika juzi ni mwanzo tu wa burudani kwani, kazi ndiyo inaanza kwa sababu burudani zipo mwanzo mwisho kwani mpango mzima sasa utaendelea mpaka Julai 15 litakapofikia tamati. Kila siku filamu mbalimbali zitaonyeshwa kwenye skrini kubwa zilizopo Ngome Kongwe sambamba na semina za mafunzo ya uandaaji na uongozaji wa filamu yatakayotolewa na waongozaji wakubwa kutoka nchi mbalimbali.

Advertisement