Kifo kimedhihirisha Muna hakumpenda Patrick wake

Sunday July 8 2018

 

By LUQMAN MALOTO

UNAYEMPENDA utamtakia maisha mema. Zaidi utamheshimu na kumlinda kisaikolojia na kimwili. Utamfichia aibu zake na utahakikisha jamii haijui ule upande wake ambao, wewe na yeye msingependa ufahamike. Upendo wa kweli sio maneno matupu. Ipo gharama kubwa ndani yake.

Mzazi anayempenda mtoto wake atahakikisha anakuwa mchonga barabara nzuri ili mwanaye apite bila wasiwasi. Atakuwa mhimili wa ukuaji mzuri wa mtoto wake. Atamweka mbali na shari za ulimwengu. Hatamchanganya kwenye migogoro yake ya kimaisha. Kamwe hatambebesha mawazo katika umri mdogo.

Utamjua mzazi asiyempenda mwanaye kwa namna anavyoweza kujitahidi kumtenganisha mtoto na mzazi wake wa pili. Ama mama kumfanya mtoto amchukie baba au baba kumweka mbali mtoto na mama yake.

Baba asiyempenda mtoto wake utamwona anavyomkutanisha na ‘mashangazi’ mbalimbali. Atataka wanawake zake awaone wanabeba hadhi sawa na mama yake. Inawezekana akawa na mwanamke mmoja tu lakini akataka mwanaye amwone ndiye mama kamili, wakati mwenyewe halisi yupo.

Kipimo cha juu kabisa cha mama asiyempenda mtoto wake ni pale anapomtambulisha mwanaye kwa akina baba zaidi ya mmoja. Au leo anamwambia huyu ndiye baba yako, kesho anamtambulisha mwingine. Mtoto akiuliza na yule wa siku zile je? Anamjibu: “Yule achana naye, huyu ndiye mwenyewe.” Huyo ni mama mbovu.

Kitendo cha baba kumkutanisha mtoto na ‘mashangazi’ tofauti na kumtaka awaite mama au kumlazimisha amwone mwanamke wako ndiye mama yake, wakati mama yake halisi anamjua na yupo, vilevile mama kumtambulisha mtoto kwa akina baba tofauti, kwa pamoja humwathiri mtoto kisaikolojia katika ukuaji wake. Baba na mama wa hivyo hawampendi mtoto.

KUHUSU MTOTO PATRICK

Mwigizaji wa Bongo Movie, Rose Nungu ‘Muna’ alijaliwa kupata mtoto anayeitwa Patrick. Mtoto huyo akawa maarufu kwenye mitandao ya kijamii hasa Instagram. Patrick akaonyesha kipaji kikubwa. Akatabiriwa kuwa msanii mzuri siku za usoni.

Na utoto wake Patrick akawa kivutio cha wengi. Vyombo vya habari vikavutwa kufanya naye mahojiano. Mtoto naye akaonekana kuota ndoto kubwa katika ukubwa wake. Kuna wakati alisema anaota kuwa mwanamitindo, kipindi kingine alitamani urubani. Alikuwa mtoto mwenye kuutaraji ukubwa wake katika sura chanya. Ungemuona Muna na mwanaye, ungejionea jinsi mama anavyompenda mtoto wake. Namna alivyomweka mbele pengine kuliko chochote. Machoni ungekubali kwamba kila mtoto angekuwa na bahati kumpata mama kama Muna. Kwa mwanamume angewaza mama wa mtoto wake awe mfano wa Muna.

Patrick alifikwa na mauti Jumatano iliyopita baada kuugua muda mrefu. Ni maumivu makubwa kwa Muna na kila aliyempenda mtoto huyo. Kwa Mtanzania mwenye kuliwazia mema Taifa, lazima aumizwe na kuondoka kwa Patrick katika umri mdogo. Maana kwa kipaji alichokuwa nacho na ndoto alizoota, angeweza kuifaa sana nchi yake.

Patrick alifikwa na mauti akiwa hospitalini Nairobi, Kenya. Kama ujuavyo mtu akishafariki dunia, taratibu za maziko hufuata. Utaratibu ukawa mwili wa Patrick usafirishwe kutoka Nairobi hadi Dar es Salaam ambako mazishi yangefanyika. Mazishi hayafanyiki hewani, isipokuwa inakuwepo nyumba ambayo shughuli zote zinafanyikia hapo.

Utata ukaibuka hapo. Muna akataka mazishi yafanyike Mbezi Beach. Mwananyamala nako akaibuka mwanamume anayeitwa Peter Komu ‘Kosovo’, aliyejitambulisha kuwa baba wa Patrick, kwa hiyo akaweka msiba nyumbani kwake. Uamuzi huo wa msiba kuwa sehemu mbili ukasababisha sintofahamu.

Ni hapo ikabumbuluka kumbe Patrick alikuwa na baba wawili. Peter ni wa kwanza na wa pili ni mtangazaji wa Clouds TV, Casto Dickson. Wakati wa mvutano wa mahali sahihi pa kuweka msiba, Muna akasema baba halali wa mtoto ni Casto, akaonya aachwe amzike mwanaye maana hataki kumuumbua Peter.

Peter akakutana na vyombo vya habari, akaonyesha kila ushahidi ndiye baba wa mtoto. Ushahidi wenyewe ukawa, Peter hakuwa tu baba wa kufikirika, bali Patrick alimpata kwenye ndoa yake na Muna kabla hawajatengana. Cheti za kuzaliwa cha Patrick kinaonyesha baba ni Peter.

Zipo picha za ndoa kati ya Peter na Muna, vilevile za sherehe wakati Patrick alivyofikisha siku arobaini. Hivyo ushahidi wote kabla ya kufanya kipimo cha kuoanisha vinasaba (DNA), vinaonyesha Peter ndiye baba wa Patrick. Hata hivyo, Muna anasema baba wa mtoto ni Casto.

Peter alieleza namna alivyokuwa akimhudumia mtoto. Patrick alikuwa akitibiwa kwa bima inayolipwa na Peter. Hata fedha taslimu zilipohitajika, Peter alituma. Halafu mwishoni anaambiwa yeye sio baba, kisha mama anamtambulisha mwanamume mwingine ndiye baba.

MUNA HAKUMPENDA PATRICK

Muna na Peter wametengana, haikuwa sawa hata kidogo Patrick kuingizwa kwenye migogoro yao. Kwa namna yoyote ile, kitendo cha Muna kumtambulisha Patrick kwa baba wawili ni wazi hakuwa akimpenda mwanaye. Hakuwa mwenye kumtakia heri.

Mapenzi ya Muna kwa Patrick yalikuwa ya maonyesho na mauzo ya Instagram pamoja na kwenye vyombo vya habari.

Angekuwa anampenda kweli na kumtakia heri mwanaye angemlinda dhidi ya mkorogo wa baba wawili. Kumtambulisha mtoto baba wawili ni kumvuruga na kumuumiza kwa kujiona tofauti na wengine wenye baba mmoja.

Ushahidi wa Peter unaonyesha Patrick alizaliwa ndani ya ndoa. Hivyo, Muna kama anasema mtoto ni wa Casto, maana yake atakuwa alichepuka nje ya ndoa? Je, aliolewa akiwa na mimba? Au kwa vile walitengana ndiyo Muna anaona bora amnyime Peter haki ya kuwa baba wa Patrick? Jibu lolote lenye ndiyo katika hayo maswali matatu ni kuonyesha Muna amejaa utoto!

Dunia sio mpya hii. Waliishi mababu na mabibi kabla yetu. Iliweza kutokea mwanamke kupata ujauzito kabla ya ndoa. Alipoamua kumtaja mwanamume fulani ndiye baba, basi alibaki huyohuyo. Pengine alimsingizia kwa sababu za kimaisha, lakini hata ungemwekea kisu shingoni angemtaja yuleyule aliyemtaja awali.

Sababu ni kwamba mabibi zetu waliwapenda sana watoto wao, hawakutaka kuwavuruga. Walijua kuwatajia mababa wawili wangeweza kukosa kote. Hivyo, mwanamke alihakikisha anamfungamanisha mtoto wake na baba aliyemtaja hata kama ndani ya nafsi yake alijua hakuwa halisi. Babu zetu nao wakasema kitanda hakizai haramu. Inawezekana Muna alichepuka kwenye ndoa kisha kupata mimba ya Casto au aliolewa na Peter akiwa na mimba ya Casto. Vyovyote iwavyo, kama aliamua kumpa Peter hadhi ya kuwa baba wa Patrick, alitakiwa kubaki na msimamo huohuo. Sio baada ya kugombana au sababu yoyote ile ya kimaisha ndiyo ageuke na kumtaja Casto kuwa baba.

Ni hatari sana kuchanganya wanaume wawili kwa mtoto mmoja. Mwanamke anayefanya hivyo anakuwa hamtakii heri mtoto wake. Ndiyo maana naliona hili lipo wazi Muna alimpenda Patrick kwa maonesho tu. Muna hakuyapenda maisha ya Patrick, hakumtakia heri. Alikusudia kuvuruga kisaikolojia kwa kumfanya mtoto wa aina yake mwenye baba wawili.

Advertisement