Ngoma hizi zimebamba kinoma 2018

Friday December 28 2018

 

By THOMAS NG’ITU

UKIHESABU vidole ni kwamba kabla ya mwaka 2018 kuaga ili kuupisha wa 2019 utapata siku chache mno. Kama siku nne tu shangwe za kuukaribisha Mwaka Mpya zianze, lakini asikuambie mtu kwenye burudani kuna nyimbo zilibamba kinoma mwaka 2018.

Mashabiki wa fani hiyo wamesikiliza nyimbo kibao zilizopata muda wa kurushwa hewani kupitia vituo mbalimbali vya runinga na redio.

Pia, kuna nyimbo nyingine zimekuwa hazipati muda wa kupigwa kwa sababu mbalimbali, lakini katika mitandao zimekuwa zikiongoza kwa kutazamwa kinoma.

Mwanaspoti limekuangazia ngoma kali zilizobamba 2018 kwa kusikulizwa na kutazamwa kwa wingi na mashabiki kupitia mitandao ya kijamii na kufunika kinomanoma!

KWANGWARU

(34 Milioni)

Ngoma hii iliyofanywa na Harmonize aliyemshirikisha Diamond Platinumz, haikupigwa sana katika vituo vya redio na televisheni, kilichokuwa kinatokea ukipita katika kumbi za starehe ni rahisi mno kusikia ikipigwa.

Mashairi yaliyotumika ndani ya wimbo huu yanawafanya watu wapende, pia ni wimbo ambao unachezeka kwani hata kwenye sherehe mbalimbali ulikuwa unatumika.

Kupitia Mtandao wa Youtube hii ndio nyimbo ambayo imetazamwa mara nyingi na wadau wa muziki ulimwenguni ikiwa na miezi minane tangu iwekwe katika mtandao huo.

AFRICAN BEAUTY

(28 Milioni)

Baada ya Diamond kushirikishwa katika Kwangwaru aliacha mwezi mmoja tu baadaye akatoa ngoma hii na kumshirkikisha Omarion ambayo imefikisha watazamaji 28 milioni.

Ni wimbo ambao ameelezea namna ambavyo msichana wa Kibongo anavyopendeza pamoja na mila ambazo watoto wa kike hufanyiwa. Ni wimbo wenye mashairi mazuri lakini pia unachezeka ila kubwa zaidi ni sehemu ambayo alimfanya Omarion kuimba Kiswahili ‘Penzi nitalipamba ngojera huba kama Tanga Sigera, picha twazitwanga kisera baada ya chali kimoko’ hii ni ishara ya kutangaza Lugha Kiswahili.

JIBEBE

(9.8 Milioni)

Wimbo huu ulitoka Agosti, ukiwa umeimbwa na wasanii watatu wa WCB, ukali wa video na mashairi uliufanya wimbo huo kutazamwa mara watu milioni 9.8.

Staili zilizotumika kucheza huu wimbo nazo zilikuwa kivutio kikubwa kwasababu walikuwa wanacheza na kuonyesha dhahiri kwamba wamejipanga upande hata wa kucheza ukiachana na mashairi yenyewe.

KATIKA

(8.4 Milioni)

Familia ya Navy Kenzo ambayo wanakuwa na kazi moja tu ya kutayarisha mdundo na kuingia ndani ya studio yao, mwaka huu wameamua kufunga mwaka na ngoma hii ambayo imemshirikisha Diamond Platinumz.

Mashairi yake sio pendwa sana katika jamii lakini mdundo wake na video ya wimbo ndio umefanya mashabiki wavutiwe kuitazama licha ya Diamond kuwepo katika ngoma hii. Licha ya kutoka Septemba tu, imetazamwa mara milioni 8.4 kitu ambacho kinaashiria kabisa imewavutia wengi.;

NINOGESHE

(6.6 Milioni)

Wamempa jina la African Princess kutokana na namna ambavyo amekuwa na sauti ya pekee katika mashairi yake. Uwezo wake wa kuimba mashairi ya mapenzi umekuwa kivutio kwa wengi wanaopenda nyimbo hizo. Nandy aliutoa wimbo huu Mei, lakini mpaka sasa umetazamwa mara 6.6 milioni na hii ni kwa sababu hauchoshi kutokana na mpangilio uliotumika katika video yake ukiachana na namna ambavyo ameweza kulilia kunogeshwa katika wimbo huo ‘Bodaboda yangu vipi nipande mishkaki’ ni sehemu ya mashairi yaliyotumika katika wimbo huo.

HODARI

(6.3 Milioni)

Mbosso ni msanii ambaye amebarikiwa sauti fulani katika muziki wa Bongo Flava. Amekuwa akitoa ngoma kali za mfululizo lakini hapa tunaingazia Hodari ambayo imetazamwa takribani mara 6.3 milioni tangu iwekwe katika mtandao wa Youtube Septemba. Wimbo huu amemsifia mwanamke wake ni hodari wa mapenzi anapokuwa naye kitandani na hata katika mambo mengine ya kimapenzi na kujikuta jamaa akilewa kabisa kwake.

MWAMBIE SINA

(2.7 milioni)

Wimbo huu umefanywa na kundi jipya kabisa la Kingsmusic, umefikisha idadi kubwa ya kutazamwa ikiwa ndio kwanza imewekwa Oktoba katika Mtandao wa Youtube.

Mashairi ambayo yametumika ni kila msanii aliyeimba amefunguka kwa upande wake jinsi anavyompenda mwanamke wake, huku Kiba akisisitiza hana mtu mwingine wa kutamba naye. Ni wimbo ambao unaweza kusikilizika lakini pia kuchezeka kutokana na mashairi yaliyoimbwa pamoja na mdundo ambao umetumika katika wimbo huu.

JINI KISIRANI

(2.6 milioni)

Amber Lulu amekuwa na matukio mengi makubwa nje ya usanii wake, lakini hilo halijamfanya aache kufanya ngoma ambazo zitakuwa pendwa kwa jamii. Aliachia ngoma hii Febrauri, lakini mashairi yake ni kama amekuwa akitambiana na mwanadada mwenzake katika kutafuta maisha asifuate hatua zake.

GO GAGA

(2.5 Milioni)

Msanii Lavalava naye akitoka Kundi la Wasafi Classic anaingia katika orodha hii baada ya wimbo wake kufikia idadi ya milioni 2.5 kutazamwa katika mtandao wa Youtube tangu auweke Oktoba. Wimbo huu Lavalava amemsifia mwanamke wake amebarikiwa kuanzia umbile lakini pia hata mapenzi ambayo anayapata ni adimu, kiasi cha kujikuta akiimba Go Gaga.

KADAMSHI

(2.4 milioni)

Mkongwe wa Bongo Flava, Dully Sykes alirejea kwa kishindo baada ya kuachia ngoma ya ‘Kadamshi’ akiwa na Harmonize, kiasi cha kufikisha idadi ya kutazamwa mara 2.4 ikiwa imewekwa Septemba.

Katika kiitikio Hermonise ameweza kabisa kutamba na kuonyesha ukali wake ukiachana na verse yake aliyoimba lakini kubwa zaidi ni jinsi ambavyo mashairi yalivyopangiliwa na video yake washiriki wanavyocheza.

FRESH REMIX

(1.8 milioni)

Baada ya Fid Q kuachia ngoma yake ya Fresh, Diamond na Rayvanny walimuomba kurudia ngoma hiyo baada ya kuvutiwa na mdundo uliokuwan ndani ya ngoma hiyo.

Wimbo huu ulifunika upande wa Hip Hop baada ya kufanyiwa Remix na kufikisha idadi ya kutazamwa mara milioni 1.8 licha ya kutimiza miezi 11 tangu iwekwe katika mtandao wa Youtube.

HUENDI MBINGUNI

(1.4 milioni)

Ni aina ya wimbo kama vichekesho fulani hivi kwa namna ambavyo umetengenezwa na wala hakuna ambaye alitarajia kuona kama wimbo huu unaweza kufanya vizuri.

Lakini Whozu alikuwa mjanja katika mashairi yake kwani alikuwa anazungumzia ukiwa mbishi basi huendi mbinguni au ukifanya jambo sio zuri na halimpendezi Mungu basi hauendi mbinguni, licha ya wimbo huu haupo katika maadili ya dini na kuwa katika mfumo wa Bongo Flava lakini ameimba vitu vya maana.

Ukiwa umewekwa Agosti umetazamwa mara 1.4 hii kutokana na kuimba vitu ambavyo vijana wengi wa kisasa wamekuwa wakivifanya katika maisha yao ya kila siku.

CHAUSIKU

(1.3 milioni)

Mkali wa sauti na mashairi ya kulalamika, Barnaba Classic humu alitambaa vizuri na mwanadada Vanessa Mdee mpaka kiasi cha kufikisha idadi ya kutazamwa 1.3 milioni.

Namna ambavyo walikuwa wakipokezana kwa kuimba ni staili ambayo iligeuka kuwa kweli, huku wengi wakiwa hawajatarajia kuona Vanessa kama anaweza kutambaa na ngoma yenye biti kama la mchiriku.

ZAIDI

(1.2 milioni)

Kipenzi cha warembo mwenyewe ndio anavyojiita, lakini katika muziki jina lake maarufu ni JUX, wengi wanapenda namna ambavyo anatunga mashairi yake ya mapenzi. Katika wimbo huu aliouweka Septemba, amezungumzia kwamba azidi kuongezewa mapenzi ili asiruke kabisa kwa mwanadada wake kiasi cha kusema ‘kama wewe ni asali mama, acha nyuki wanivamie’.

PARANAWE

(1.5 milioni)

Ikiwa na wiki moja tu tangu itoke Desemba 10, imefikisha idadi ya 1.5 milioni kutazamwa. Hermonize na Rayvanny wamekuwa wakali katika ngoma zinazosikilizwa. Jina la wimbo ni kama mchezo wa ngumi wa Kibrazili lakini wao wanamuambia mwanamke acheze mchezo huo, ni aina ya muziki fulani hivi unachezeka na kusikilizika.

YATAPITA

(1.3 milioni)

Licha ya kuwa Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule ‘Prof Jay’ amekuwa akitenga muda wake ili aweze kuingia studio na kufanya ngoma kama kawaida kutokana na kipaji chake ni muziki.

Mwaka huu ameufunga kwa kuachia ngoma kali na Hermonize akizungumzia mtu yeyote anayetakiwa asikate tamaa katika lile ambalo analipigania. Aina ya mashairi aliyotumia imefanya kufikia hatua ya kutazamwa mara 1.3 milioni licha ya kuwekwa katika mtandao huu mwezi Oktoba ikiwa imebaki miezi miwili kufunga mwaka.

HATUFANANI

(1.2 milioni)

Baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu, Shetta aliamua kurejea kwa nguvu na ngoma ya Hatufanani akiwashirikisha Blue na Jux na ukweli ngoma hii imefanya vizuri tangu iachiwe.

Ikiwa ina wiki mbili tu baada ya kuachiwa Novemba 30, imetazamwa mara 1.2 milioni lakini mashairi ambayo yametumika, Sheta amezungumzia kutofanana na mtu yeyote anapokuwa anatafuta mafanikio yake.

KADOGO

(1.2 milioni)

King Kiba yeye ametoa kali ya kufungia mwaka baada ya kufikisha 1.2 milioni ya wimbo wake huu kutazamwa licha ya kuwa na siku saba tu tangu uwekwe Youtube.

Inadaiwa msanii huyu amekuwa mvivu wa kuachia ngoma mfululizo kama wanavyofanya wenzake, hivyo anapoachia mashabiki wake wengi wanakua na hamu ya kuona kitu alichokifanya.

Vilevile mashairi ambayo ameyatumia katika ngoma hii amezungumzia vizuri namna ambavyo mademu wa Mombasa, Kenya wanavyokuwa hasa katika upande wa mapenzi.

FIMBO

(1.1 milioni)

Jux ndani ya wimbo huu ameeleza namna ambavyo mrembo wake anavyomnyoosha kiasi cha kushindwa kwenda kwa mrembo yoyote yule kutokanaa na mapenzi anayoyapata.

Wimbo huu uliachiwa Machi mwaka huu lakini mpaka hivi sasa bado upo katika orodha kali ya ngoma ambazo zimetazamwa mara nyingi. Umetazamwa na mashabiki wengi kwenye Mtandao wa Youtube kwani mpaka sasa ni watazamaji 1,1 milioni wamefanya hivyo.

ALISEMA

(1.1 milioni)

Ni kati ya ngoma ambazo Nay wa Mitego ameweza kufunguka katika mashairi yake akizungumzia mambo mengi yanayoendelea katika jamii inayotuzunguka.

Nay wengi walimzoea kuimba mashairi ya kufokafoka lakini humu ameelezea kila baya na jema linaloendelea ‘Kuwa mpinzani sio kupinga kila kitu’, hii ni sehemu ya mashairi katika wimbo huu akizungumzia maendeleo yanayofanywa na Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Imefikia idadi ya kutazamwa mara milioni 1.1 baada ya kuwekwa Oktoba hivyo bado itaendelea kutazamwa zaidi mpaka mwakani kwani ndio kwanza ina miezi miwili tu.

Lakini tofauti na nyimbo zake nyingine ambazo huwa zinakuwa gumzo katika jamii, ndani ya ngoma hii, Nay wa Mitego ameuma na kupuliza.

Hakutaka kuichamba sana serikali kama kawaida yake pale anapotoa ngoma inahusu siasa na jamii kwa jumla.

Advertisement