Mwasiti afichua penzi la Zilla

Muktasari:

  • Mwasiti Almasi amefunguka alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na King Zilla lakini baadaye walikwenda mbele zaidi na kuwa ndugu wa karibu.

STAA wa kike wa Bongo Flava, Mwasiti Almasi amefunguka alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na King Zilla, lakini baadaye walikwenda mbele zaidi na kuwa ndugu wa karibu.

Mwasiti, ambaye alikuwa mmoja kati ya wasanii wa kwanza kufika nyumbani kwa Zilla, baada ya kupata taarifa za kifo cha nyota huyo wa Hip Hop aliyekuwa akitambana na ngoma ya X, amesema msiba huo umemuachia majeraha kwani, amepoteza ndugu wa karibu.

Akizungumza na Mwanaspoti nyumbani kwa Zilla Salasala, Dar es Salaam, Mwasiti aliyetamba na ngoma za Nalivua Pendo, Mapito na Kaa Nao, amekiri waliwahi kuwa wapenzi na rapa huyo na walitokea kuelewana sana na kuwa kama familia moja.

“Nilikuwa na uhusiano na Zilla kwa muda na tulipoachana tukabadilika kuwa ndugu, huu ni msiba mkubwa kwangu na nimepoteza kaka bora,” alisema.

Amesema tofauti na wapenzi wengine wanapoachana hugeuka kuwa maadui, kwao ilikuwa tofauti kwa sababu Godzilla alikuwa mwanamume mwenye haiba ya kipekee.

“Nilipata mshtuko na kuishiwa nguvu kwani sikuamini na taarifa ya kifo cha Zilla, niliamua kuwapigia watu tofauti ili kuthibitisha taarifa hizo, kwa kweli naweza kukaa na maumivu ya Godzilla kwa muda mrefu,” alisema Mwasiti.

Mbali na hiyo Mwasiti amesema kuwa karibu na Godzilla amejifunza kitu alichokuwa nacho cha kukaa na maumivu yake kitu ambacho watu wengine hawawezi kuwa nayo.

Kwa upande wa habari zinazodai kuwa, Godzilla alipokuwa hai alikuwa akilalamika kutopata sapoti ya wasanii wenzake Mwanasiti amesema haya:

“Hili swali natamani Zilla angekuwa hai angelizungumza yeye binafsi, ila binafsi sikuwahi kumsikia akilalamika kuwa hapewi sapoti zaidi ya kusema watu wapendane na kuzidisha upendo.

“Mara ya mwisho niliwasiliana naye wiki mbili zilizopita, baada ya kumwambia anataka kumuunganisha na msanii wake ili waweze kutoa wimbo wa pamoja.

Mwasiti na Godzilla wamewahi kushirikiana katika ngoma za Soldier na First Class, ambazo zilikuwa moto kwenye game.