Majibu konki ya Lulu kuhusu hatma ya ndoa yake

OKTOBA mosi mwaka huu msanii mwenye tashtiti zake mjini, Elizabeth Michael maarufu Lulu, atakuwa amefikisha miaka miwili tangu alipovalishwa pete ya uchumba.

Pete hiyo alivishwa Oktoba mwaka 2018 na mchumba wake ambaye ni mfanyabiashara Francis Siza maarufu Majizo ambaye pia ni mmiliki wa EFM redio na TVE.

Ni kutokana na uchumba huo ambao baadhi wameuona ni wa muda mrefu amekuwa akikutana na maswali ya watu mbalimbali mtandaoni wakitaka kujua lini ataolewa huku wengine wakifika hatua ya kuukebehi kwa kuuita uchumba sugu.

Hii hutokea mara kwa mara hasa pale anapojipiga picha na kuweka kwenye ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram, ambao hadi kufika mwezi huu amefikisha wafuasi milioni tano.

Katika maswali hayo siyo mtu mmoja au wawili humuuliza kuhusu masuala hayo na bila kujali huwapatia majibu konki.

Katika makala haya tutakuletea maswali hayo na majibu yake hayo konki ambayo Lulu aliwahi kuwajibu watu wanaohoji uchumba wake huo, pete na mchumba wake Majizo.

Moja ya swali aliulizwa ni lile la aliloulizwa na Lowata Soningo aliloandika: “Hivi dogo uliolewaga na jamaa yetu au mliishiaga wapi?”

Majibu: Tupotupo tu, mbele hatuchezi wala nyuma hatutingishiki broo.

Mwingine ni Beda Ayman aliyemw-ambia: ’Uzee unakaribia shoga, fanya uolewe.”

Majibu yalikuwa: “Beda kuolewa kwani ni anti-uzee? Akimaanisha kuwa ndio dawa ya kuzuia uzee?

Baada ya Lulu kuweka video fupi ikionyesha wakiwa wamekumbatiana na Majizo.

Swali:Anakuoa lini??

Majibu: Hana hata mpango, njoo mpige.

Swali jingine ni la kutoka kwa Mumuake, ambalo lilifuata baada ya Lulu kuweka picha akiwa kaficha macho yake kwa mkono wake wa kushoto na kuonesha hana ile pete aliyovishwa kidoleni.

Swali: Pete iko wapi

Majibu: Nimesahau nyumbani mume wangu.

Mwingine aliyewahi kumuuliza swali kuhusu lini anafunga ndoa ni Askofu Mashimo, swali alilomuuliza Agosti mwaka jana na kubainisha kuwa tayari imefika mwaka sasa tangu alipovalishwa pete hiyo lakini haoni ndoa.

Majibu ya Lulu yalikuwa ‘Kaka yangu jibu la ndoa yangu linapatikana katika kitabu cha Mathayo 25:13 na useme Ameen,”.

Kwa mujibu wa andiko hilo mstari wa 13 unasema: “Basi kesheni kwa sababu hamuijui siku wala saa.”

Zainabomar60 yeye alimuuliza msanii huyo: “Kwa nini humuweki majizo naye awe smati jamani, usinifokee lakini,”

Majibu: Akiwa smart kichwani na mfukoni inatosha, nyingine aniachie mamsapu niwakilishe.

Mtaalam

azungumza anachopitia Lulu

Mtaalam wa masuala ya saikolojia na uhusiano, Reuben Ndimbo, anasema kiutaratibu mtu hupaswa kuolewa baada ya miezi sita tangu alipovalishwa pete ya ndoa.

Akifafanua zaidi hili, Ndimbo anasema: “Sio kwamba jambo hili la kuolewa baada ya miezi sita tangu ulipovalishwa pete ni sheria, isipokuwa wengi katika jamii yetu ndio wamezoea kuona hivyo.

“Hivyo anapotokea mtu kama Lulu aliyekaa miaka miwili sasa, lazima watu wawe na maswali juu yake,” anasema mtaalam huyo.

Pia aneleza kwamba ukiachilia mbali jamii, hata muhusika anayevalishwa pete, mara baada ya tukio hilo huwa ana matarajio makubwa sana ya kuingia kwenye ndoa na kuongeza kuwa kama hawakuwa tayari wasingepaswa kulifanya jambo hilo mapema.

Je kuna athari?

Ndimbo anafunguka kuwa katika suala la kuvishwa pete na kuachwa muda mrefu hujaolewa lina athari hususani kwa mwanamke kwa kuwa mwisho wa siku mwanaume ndio mwenye uamuzi aoe lini.

Mojawapo ya athari ambazo anaweza kuzipata mtu kama Lulu, anasema ni pamoja na kuvunjika moyo. Ni kutokana na hilo anasema katika maisha yake utaona kuna vitu vinapungua taratibu ikiwemo kutopenda kujichanganya na marafiki zake au ndugu kwa kuhofia watamuuliza jambo hilo.

“Pia mtu wa aina kama hii ya Lulu hupunguza uwezo wa kujiamini mbele za watu na wengine hufikia hatua mbaya kuanza kutembea na wanaume mbalimbali watakaomdanganya kuwa yeye ni mzuri na kujikuta anatumika tu na hiyo ndoa kuisikia kwenye bomba.

‘Ukiachilia hilo kuna suala zima la kuwachukia wanaume na kuona wote wana tabia kama za mchumba wake, huku hasira za mara kwa mara zikiwa hazichezi mbali na yeye,” anasema Ndimbo.

Anachoona kwa

Lulu na Majizo

Ndimbo anasema anachoona kwa Lulu na Majizo kutooana mpaka sasa, huenda walipanga kufanya sherehe kubwa na kila wakiiwazia bajeti yake, hiyo hela wanaona wawekeze kwenye biashara zao.

“Wapenzi mnapokuwa katika nafasi fulani ya kimaisha kuna vitu mnawaza hasa katika suala zima la uwekezaji, hivyo huenda Lulu na Majizo wanaona hiyo hela ya harusi kwa nini wasiiwekeze kwanza iwazalishie na suala la harusi litakuja baadaye kwa kuwa hilo lipo tu,” anasema.

Hili linajibia swali la Lulu alilowahi kuulizwa kuhusiana na ndoa hiyo, na kueleza kuwa anahisi ndoto zake katika kutafuta maisha bado na endapo atakapoingia kwenye ndoa atakuwa ni mke wa fulani na sio Lulu.

Ndimbo anasema wanachofanya wengi kwa maswali ni kutaka kumuumiza Lulu tu.