Dr Dre, P Diddy! Vipi kwa Diamond, Kiba

NewYork, Marekani. ISHU ya kambi za mastaa kwenye mitandao ya kijamii zinabamba sana hadi huko Marekani. Kambi hizo zimekuwa zikiongeza mzuka mwingi mastaa kama ilivyo hapa nyumbani hasa zile za AliKiba na Diamond ama Wema Sepetu na Hamisa Mobeto.

Lakini, huko Marekani wasanii wamekuwa wakitumia wafuasi kupiga pesa na sasa ni miongoni mwa matajiri wakubwa duniani, jambo ambalo linatosha kuwa funzo kwa mastaa wa Bongo Flava, ambao kwa sasa wameanza kuvuka mipaka na kupiga pesa ndefu.

Hawa hapa wasanii 10 wenye majina makubwa kwenye biashara ya muziki na pia, wanaoongoza kwa utajiri duniani kwa sasa. Yaani akaunti zao benki zimenona, wamewekeza kwenye kampuni kubwa na ukija huko kwenye mijengo ya maana, gari kali ndio utashangaa mwenyewe.

10. Ice Cube- $140 Milioni

Ndio! Ice Cube, jamaa amejinga jina lake kupitia muziki kisha akausoma mchezo ulivyo na kuamua kujikita zaidi kwenye filamu. Amecheza filamu kibao kali ikiwemo Anaconda. Awali, alikuwa kwenye kundi la NWA, lakini baadaye akaamua kufanya mambo kivyake na huko ndio akapiga pesa ndefu sana. Anamiliki kampuni kibao za muziki na kila filamu anayotengeneza inabamba.

9. Kanye West- $145 MilionI

Kanye West, mume halali wa Kim Kardashian yaani pesa inafuata pesa unaambiwa. Jamaa aliweka rekodi ya kuuza nakala zaidi ya 100 milioni kwenye mtandao kisha akauza nakala halisi 32 milioni za albamu yake. Ameshinda tuzo za Grammy Awards 21 kupitia muziki. Anamiliki kampuni ya mavazi ya Yeezy ambazo zinambamba kinoma. Pia anahisa kwenye kampuni za Louis Vuitton na Nike.

8. Eminem- $160 Milioni

Rapa mtata kinoma na kwa sasa anaonekana kama kafulia, hapana Eminem bado yuko fiti na anacheza anga za mabilionea duniani. Anamiliki kampuni ya muziki ya Shady Records, pia amejikita zaidi kwenye filamu.

7. Ronald “Slim” Williams- $170 MilionI

Wale wazee wa zamani wanamjua sana huyu jamaa, alianza kutengeneza utajiri wake akiwa na lebo ya Cash Money Records sambamba na kaka yake, Birdman. Uwepo wa msanii Lil Wayne kwenye lebo kumewapa pesa za kutosha hasa kupitia kipindi cha Behind the Music.

6. Bryan “Birdman” Williams- $170 MilionI

Kama ilivyo kwa Slim, Birdman naye amekuwa akitengeneza pesa kupitia Cash Money Records ambayo ni umiliki wa pasu kwa pasu. Awali, walikuwa wakifanya muziki wakiunda kundi la Baby kwenye miaka ya 95.

5. Usher- $180 MilionI

Huyu jamaa anafanya kila kitu unaambiwa. Ni rapa, mwimbaji, anaigiza na mfanyabiashara lakini, alijenga jina zaidi kama mwanamuziki wa R&B. Mbali na muziki, Usher amewekeza kwenye kampuni kubwa ikiwemo ya vifaa vya shule ya Yoobi pamoja na kumiliki migahawa mikubwa kibao. Aliwahi kutoa misaada kwa familia 700 zilizokosa makazi wakati wa kimbunga Katrina mjini New Orleans.

4. Master P- $350 MilionI

Wakati vita ya marapa makinda Lil Bow wow na Lil Romeo inapamba moto, basi nyuma ya kila mmoja kulikuwa na kichwa. Kwa Lil Romeo kulikuwa na baba yake, ambaye ndiye kila kitu Master P na Bow wow alikuwepo Jermain Dupri. Ni noma unaambiwa. Sasa huyu Master P sio mtu wa mchezo mchezo kwani, jamaa ana kisu cha maana. Jina lake ni Percy Robert Miller. Anapiga pesa ndefu kup;itia biashara ya nyumba, vipindi vya luninga, uchapishaji na migahawa ya kutosha tu.

3. Jay-Z- $650 MilionI

Jay-Z ametengeneza ufalme wa peke yake kwenye gemu ya muziki duniani na ana heshima ya kipekee. Ana rekodi za maana tu, lakini kubwa ni uwezo wake wa kutengeneza pesa.

Achana na maisha yake na mkewe Beyonce, Jay Z anaheshimika na kampuni yake ya Roc Nation Sports, imewatoa mastaa wengi wa soka na kikapu. Anamiliki kampuni kibao za mavazi, migahawa na amefanya uwekezaji mkubwa.

2. P Diddy- $735 MilionI

Diddy a.k.a Sean Combs ni bonge la supastaa ana anafanya biashara kibao mbali na muziki. Lebo yake ya mavazi ya Sean John ilianza kubamba miaka hiyo na mpaka sasa ni noma. Pia amewekeza kwenye kampuni kubwa zikiwemo za vinywaji kama Ciroc vodka na Aquahydrate.

1. Dr Dre- $810 MilionI

Big boss kwenye yaani ndio mfalme kwa mkwanja. Anaitwa Dr. Dre na hivi karibuni aliingiza Dola 3 bilioni kwa biashara ya miito aliyoiuzia kampuni ya Apple.

Dili hilo limemfanya Dr Dre kushika namba moja kwa utajiri duniani kwa sasa akimuondoa kwenye reli P Diddy aliyekuwa anaushikilia baada ya Jay Z kuyumba.