Panone FC sasa mambo safi

Monday December 22 2014

By MWANAHIBA RICHARD

PANONE FC ya mkoani Kilimanjaro imepania na kutamba kwamba ina kila sababu ya kufanya vizuri katika mechi zao za mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la Kwanza ambapo katika michezo mitatu ya mwanzo watakuwa ugenini, wataanza na Kanembwa JKT, Mwadui na Polisi Tabora.

Kocha Mkuu wa Panone FC, Maka Mwalwisi, aliliambia Mwanaspoti kuwa uimara wa kikosi chao kwa sasa ndio unaowapa jeuri ya kushinda mechi zote za ugenini ambapo wataanza safari kwa kwenda Kigoma keshokutwa Jumatano ambako watacheza na Kanembwa, mechi hiyo itachezwa Desemba 27.

Kisha itaelekea Shinyanga watakakokutana na Mwadui iliyo chini ya kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ mechi itakayochezwa Januari Mosi mwakani wakati mechi ya tatu itachezwa mkoani Tabora dhidi ya Polisi Tabora, mechi hiyo itachezwa Januari 4,2015 na kurudi nyumbani.

Panone imesajili wachezaji saba katika usajili wa dirisha dogo, hiyo ni kuimarisha kikosi chao ambacho kilianza vibaya katika mechi za mzunguko wa kwanza na kupelekea kushika nafasi ya saba ikiwa na pointi 14.

Ligi hiyo inaongozwa na Mwadui yenye pointi 22, Toto Africans na JKT Oljoro wenye pointi 21 kila mmoja.

Wachezaji waliosajiliwa ni Antony Matogoro kutoka Mbeya City, Jukumu Kibanda (Friends Rangers), Peter Sanga Kimondo FC), Fidelis Jonas (Villa Squad), Newton Nuty kutoka mashindano ya Kombe la Ndondo, Athman Majani alikuwa mchezaji huru na Hussein Ally aliyekuwa anacheza soka la kulipwa Afrika Kusini.

“Sasa hakuna kulala, tunataka pointi tatu za nyumbani na ugenini, lengo ni kupanda daraja, tulianza vibaya lakini kwa sasa naona kikosi changu kipo imara zaidi, wachezaji wote wapo kambini na wameonyesha umoja na mshikamano katika kuleta ushindi ndani ya timu,” alisema Mwalwisi.