Haji Manara aiwakia Yanga

Thursday December 22 2016

WAKATI ikichanganywa na mgomo wa nyota wao, viongozi wa Yanga wamewekwa kwenye hali ngumu baada ya watani zao, Simba kuwakomalia wakitaka walipwe fedha zao Sh 50 milioni zikiwa ni fidia ya beki Hassan Kessy.

Yanga iliamrishwa na Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuilipa Simba kiasi hicho cha fedha kwa kosa la kumsajili Kessy akiwa bado na mkataba na klabu hiyo.

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alisema, bila kujali kama Yanga inadaiwa mishahara na wachezaji ama la, wanachokitaka ni kulipwa chao kwa sasa kama walivyoagizwa na Kamati ya TFF.

Manara alikaririwa akisema wataandika barua kwa TFF kukumbushia deni hilo kwa Yanga kwani, ilishakubaliwa wailipe Simba fedha hizo kutokana na sakata la beki huyo.

“Mpaka sasa Yanga hawajatupatia pesa zetu, tulichoamua ni kuandika barua na kuipeleka TFF ili kuwafahamisha kuwa hukumu iliyotolewa na kamati yao ili tulipwe Sh. 50 milioni hawajapewa hadi leo,” alisema.

Wachezaji wa Yanga walikuwa kwenye mgomo baridi wa siku mbili mfululizo kudai mishahara yao ya Novemba, kitu kilichofanya kikosi hicho kishindwe kufanya mazoezi kwa siku hizo wakati kesho Ijumaa inatakiwa kuingia uwanjani vaana na JKT Ruvu.

Advertisement

Advertisement