Bocco tayari! Sasa ni Aishi na Kapombe

Muktasari:

· Hata hivyo, viongozi wa Simba wanapambana na ofa aliyotoa Kapombe kumshawishi ili ashuke na kumwaga wino jambo ambalo limeidaiwa litawezekana kwa kuwa wanaangalia michuano ya kimataifa mwakani.

SIMBA imemalizana na straika wa Azam, John Bocco na sasa wana kazi moja ya kuwang’oa kipa Aishi Manula, ambaye ni kipa bora wa msimu uliopita na kiraka Shomary Kapombe.

Manula na Kapombe wameonyesha nia ya kutua Simba, lakini ugumu wanaokutana nao hasa kwa Kapombe ni dau alilowaambia Simba ambapo leo Jumatatu vigogo wa Msimbazi watakutana ili kumaliza mjadala huo na wakifikia pazuri basi kiraka huyo atarudi nyumbani.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya Simba ni kwamba, Kapombe ametaka apewe Sh40 milioni fedha ambayo Simba wanadai ni nyingi na wapo tayari kumpa Sh 30 milioni na mshahara wa Sh 2.5 milioni wakati yeye anataka alipwe Sh4 milioni kwa mwezi.

Kapombe kabla ya kutua Azam alikuwa mchezaji wa Simba na hivyo, Simba kuamua kumuuza ambapo ameitumikia Azam kwa zaidi ya miaka miwili na sasa mkataba wake unamalizika Julai. Hata hivyo, viongozi wa Simba wanapambana na ofa aliyotoa Kapombe kumshawishi ili ashuke na kumwaga wino jambo ambalo limeidaiwa litawezekana kwa kuwa wanaangalia michuano ya kimataifa mwakani.

Simba sasa wanaelekeza nguvu zao kuimarisha kikosi kwa ajili ya ligi kuu msimu ujao pamoja na mashindano ya kimataifa, baada ya kupata tiketi hiyo kwa kutwaa ubingwa wa Kombe la FA kwa kuifunga Mbao 2-1.

Habari kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa, matajiri wa klabu hiyo hawataki kumwachia Kapombe hivyo watapambana kwa kila hali kukamilisha dili hilo.

“Kesho (leo Jumatatu) kutakuwa na kikao ambacho kitaamua ila kiukweli tunamuhitaji na kuna uwezekano mkubwa wa kumalizana naye japokuwa dau alilotuambia ni kubwa sana, ila tunaamini kila kitu kitakaa sawa baada ya kumaliza fainali hizi.

“Ila lengo letu pale Azam ni wachezaji watatu Bocco ambaye tayari, Manula na Kapombe pamoja na Deus Kaseke wa Yanga ambaye tumeanza mazungumzo naye ili kuwa na huduma yake msimu ujao,” alisema kiongozi huyo.

Kaseke tayari amemaliza mkataba wake na Yanga na inadaiwa kuwa mabingwa hao hawana mpango wa kumwongeza mwingine.

Mastaa wakubwa wa Azam wanatimka kwenye timu hiyo baada ya uongozi wa juu kuibuka na sera ya kubana matumizi ambapo, wachezaji wote wanaoongeza mikataba hawatalipwa zaidi ya ya Sh10 milioni, jambo ambalo limewakera baadhi yao ingawa uongozi umeshikilia msimamo wake huo.

Hata hivyo, uongozi huo unataka kuwaongezea mishahara tu kama inavyofanyika kwenye klabu za Ulaya.