Jezi ya Niyonzima yampa mzuka dogo

Muktasari:

  • Maka alikabidhiwa jezi hiyo aliyoitumia katika mechi mbalimbali ikiwamo zile za michuano ya Kombe la Mapinduzi na licha ya kukiri kwamba ni nzito, lakini ameapa kukomaa nayo ili kuwasahaulisha mashabiki wa Mnyarwanda huyo aliyehamia Simba.

KIUNGO chipukizi wa Yanga, Maka Edward anazidi kuwa mtamu kwa jinsi zile kampa kampa tena zake zinavyowakuna mashabiki wa klabu hiyo, lakini kama kuna kitu kinachompa mzuka basi ni jezi ya Haruna Niyonzima aliyoirithi Jangwani.

Maka alikabidhiwa jezi hiyo aliyoitumia katika mechi mbalimbali ikiwamo zile za michuano ya Kombe la Mapinduzi na licha ya kukiri kwamba ni nzito, lakini ameapa kukomaa nayo ili kuwasahaulisha mashabiki wa Mnyarwanda huyo aliyehamia Simba.

Akizungumza na Mwanaspoti kiungo huyo alisema anatambua uzito wa jezi hiyo, lakini anajitahidi kwa kadri ya uwezo wake kuitendea haki kwa kutekeleza majukumu yake ilimradi kuwapa raha wana Yanga.

Maka alisema anaamini uwezo wa Niyonzima hasa alipokuwa Yanga, lakini atacheza kwa kiwango chake akiwa ndani ya jezi hiyo, bila kujali Niyonzima alifanya nini Jangwani.

“Ukweli unajulikana, jezi aliyokuwa anavaa ilimfanya Niyonzima azimikiwe na mashabiki wa Yanga na hata alipoondoka watu waliumia, hivyo kama nitashindwa kufanya vyema nitawaumiza zaidi ndio maana najitahidi kupambana, ila jezi nzito.”

Akizungumzia nafasi aliyopata ya kuanza katika mechi dhidi ya Singida United Kombe la Mapinduzi, alisema ilikuwa kama zali kwake. “Kocha Msaidizi (Noel Mwandila) aliniuliza kama naweza kucheza dakika 90 nilipomjibu ndio hakuwa na kauli nyingine, mchana nikajikuta katika kikosi na nikasema nafasi hii natakiwa niitumie vizuri na kucheza kwa umakini wa hali ya juu kwani nikiharibu ni ngumu kupata nafasi tena,” alisema kwa furaha.