Wachezaji wetu wana kitu cha kujifunza kwa nyota wa Iceland

FAINALI za Kombe la Dunia zinazoendelea kule Russia zinasisimua na kuleta burudani kwa mashabiki wa soka nchini. Hii ni kwa sababu ya matokeo yanayoendelea kutokea kwenye mechi za makundi. Hakuna aliyetarajia kama Argentina inayoundwa na mastaa wakali wa kufumania nyavu ingeshindwa kufurukuta ndani ya kundi lake.

Michuano ya msimu huu inathibitisha kuwa hakuna timu nyonge, japo wawakilishi wa Afrika wameendelea kuwasononesha mashabiki wake kwa kushindwa kufanya kweli.

Wakati mashabiki wakiendelea kusikilizia ili kujua timu zipi zitakazopenya hatua ya 16 Bora, nyota wa soka nchini wanaozifuatilia fainali hizo wana jambo moja la kujifunza Russia, hasa kwa nchi ndogo ya Iceland ambayo juzi ilicharazwa mabao 2-0 na Nigeria.

Iceland yenye ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 103,000 ikiwa na idadi ya watu wapatao 348,580 tu ipo Russia ikishiriki kwa mara ya kwanza, ikiwa ni miaka miwili tu tangu walipocheza Fainali za Mataifa ya Ulaya, Euro 2016 na kufika robo fainali.

Inawezekana si wote wanaofahamu kuwa kikosi cha wachezaji 23 walioenda Russia wa taifa hilo, zaidi ya nusu ni watu wenye taaluma zao za maana tu.

Kwa mfano katika pambano lao la kwanza la fainali hizi za Kombe la Dunia walipoibana Argentina na kutoka nayo sare ya bao 1-1 huku Lionel Messi akikosa penalti, kipa aliyedaka mkwaju wa staa huyo, Hannes Halldorsson, kitaaluma ni mtayarishaji wa filamu.

Mbali ya kipa huyo, asilimia kubwa ya wachezaji wa Iceland ni madaktari kama ilivyo kwa kocha wao, Heimir Hallgrimsson ambaye ni daktari wa meno.

Wapo pia watangazaji katika kikosi hicho, wapakia chumvi na waoka mikate kuonyesha kuwa mbali ya soka bado kuna maisha ambayo wachezaji wanapaswa kufanya ili kujitengenezea fedha za maana.

Ndio maana tunasema wachezaji wetu na vijana wengine wenye ndoto za kucheza soka wanapaswa kujifunza jambo ndani ya kikosi cha Iceland, kwani mbali ya namna walivyoipigania nchi yao na kuipeleka kwenye fainali hizo za Russia na zile za Euro 2016 ikifanya maajabu kwa kuiduwaza England kwa kuizuia isiingie robo fainali pale Ufaransa, lakini pia wanafanya kazi nyingine, tena zikiwamo za kisomi.

Kwa hapa Tanzania, ni wachezaji wachache wenye elimu zao wanaocheza soka kwa mafanikio, wengi wao wanaocheza ni watu wenye elimu kuanzia kati kurudi chini na walioshtuka waliamua kuachana kabisa na soka ili wakomalie kitabu kujiinua kimaisha.

Hata baadhi ya wadau wa soka wana fikra mgando za kuamini kuwa soka haliwezi kuchezwa na wasomi ndio maana wasomi wamejazana kwenye kikapu na michezo mingine inayoangaliwa kama ya wasomi na matajiri kama gofu, tenisi na kadhalika, kitu ambacho sio kweli.

Bado wengi hawaamini kama mwanamichezo anaweza kuwa na fani nyingine mbali na mchezo anaoucheza.

Ndio maana bondia Mmarekani, Phil Williams, alipokuja nchini kupambana na Francis Cheka na kupigwa kwenye pambano la kuwania ubingwa wa Dunia wa WBF, wengi walimshangaa kusikia eti ni kinyozi. Ilikuwa ni kitu cha ajabu kusikia kinyozi tena kutoka Marekani akija Tanzania kupambana na Cheka, lakini wakasahau kuwa bondia aliyekuja kupigana naye, yaani Cheka enzi hizo alikuwa muokota chupa mtaani!

Hii ni kwa sababu wengi bado hawaamini kama kuna kazi nyingine nje ya michezo ambayo mtu anashiriki, ndio maana Iceland ni kama darasa fulani kwa nyota wetu hasa wa soka kuwa wanapaswa kubadilika na kutotegemea soka pekee katika maisha yao.

Kuwa na taaluma nyingine itakayokuwa ikiwaingizia fedha bila ukomo ni faida kwao hata pale wanapokuja kupatwa na matatizo na kuacha kucheza kama kuumia na tatizo jingine, wasivurugwe na kuyumba.

Na hata wengine wenye uwezo wa kujiendeleza kimasomo wasijivunge, kuna maisha mengine nje ya soka na umri wa kusakata soka ni mchache kulinganisha na maisha ya kuteseka mitaani watakapostaafu. Wajifunze kwa mastaa wenzao wa nyuma kina Leodegar Tenga, Lawrance Mwalusako ama Mtemi Ramadhani ama Ally Mayay na Aaron Nyanda ambao leo hawayumbi kwa vile walicheza wakiwa na elimu zao.

Kucheza soka kutabakiwa kuwa kwenye damu yao kwa vile wanacho kipaji hicho, lakini kuwa na ujuzi mwingine wa kitaaluma ni jambo zuri zaidi.

Kwa maana hii, hawa wachezaji chipukizi walio mashuleni, wanapaswa kukuzwa wakifahamu kuwa soka na elimu ndio mpango mzima kwa sasa. Wapige soka na kitabu juu.