Uzuri Emery ameishi kimasikini, kitajiri

KARIBU Emirates Unai Emery. Karibu EPL, ligi ya vichaa. EPL ndio kipimo cha makocha wote duniani. Ni ndoto ya makocha wengi.

Unaweza kutamba Ufaransa, Ujerumani, Hispania na kwingineko, lakini kama hujakanyaga Ligi Kuu England (EPL), heshima yako bado inakuwa ndogo. EPL ndio kipimo cha akili kwa kocha yeyote. Karibu Emery.

Hata kocha Pep Guardiola, msimu wake wa kwanza England alikula za uso na Man City yake, akarudi nyuma kujipanga, na alipoingia akavunjvunja kila aina ya rekodi.

Ni wazi haikuwa jambo jepesi kwa mabosi wa Arsenal kumpata mrithi wa Arsene Wenger.

Ni ngumu kuziba pengo la mtu uliyeishi naye kwa miaka 22. Ni kama vile ndoa imevunjika na inabidi uchumbie upya. Inahitaji utulivu mkubwa, vinginevyo utapata danga.

Wenger alikuwa na udhaifu wake. Wenger alikuwa na changamoto zake, lakini bado anabaki kuwa kocha mwenye historia kubwa na Arsenal.

Haijalishi kwamba taji lake la mwisho la EPL aliwapa 2004, bado kuziba pengo lake ni kazi nzito.

Ndio maana mabosi wa Arsenal walianza kuwafikiria kina Mikel Arteta, Patrick Vierra na wengineo kama mbadala wa muda mrefu. Hata hivyo kwa sasa alihitajika mtu mwenye wasifu mkubwa zaidi.

Unapoachana na Wenger kwa sababu ya kushindwa kupata mataji, unahitaji kocha mwenye akili ya mataji. Emery ana akili hiyo. Katika miaka mitano tu iliyopita ameshinda mataji tisa tofauti.

Tena rekodi tamu zaidi ni kwamba mataji matatu kati ya hayo ni ya Europa Ligi. Japokuwa hakufanya vizuri kwenye UEFA, lakini alikuwa mbabe kwenye Europa. Tena taji moja kati ya hilo alishinda mbele ya Liverpool. Raha iliyoje.

Pamoja na kwamba baadhi ya watu wanaikosoa Arsenal kwa kumpa kazi kocha huyo Mspanyola, kuna kitu kimoja hawakifahamu. Kitu cha tofauti kwa Emery ni kwamba ameishi maisha ya kimasikini na kitajiri. Tena ametamba kote kote.

Anajiunga na Arsenal akitokea PSG. Nani asiyefahamu utajiri wa PSG? Pale PSG pesa haijawahi kuwa tatizo. Fungu lolote kocha analohitaji kwa ajili ya kununua mchezaji mahiri lipo. Hakuna mchezaji wa PSG anayeuzwa. Yaani ni ngumu kwa klabu yoyote kununua mchezaji kutoka pale PSG.

Kocha ana uhakika na maisha yake. Mchezaji ghali zaidi duniani alikuwa pale kwake. Ni Neymar Santos. Wachezaji wengine wa maana kama Edinson Cavani, Angel Di Maria, Blaise Matuidi na wengineo wapo. Unahitaji nini tena?

PSG inaishi kifahari. Kocha akisema kitu kinafanyika usiku huo huo. Mabosi wa timu hiyo hawaoni shida kumnunua staa yeyote yule, labda akatae mwenyewe.

Emery ametoka kwenye ufahari huo. Ametoka kwenye bahari ya pesa. Bahati mbaya kwake ni kuwa anakwenda Arsenal ambayo haina ufahari huo.

Hata hivyo, hilo haliwezi kuwa tatizo kwake. Kabla ya kwenda PSG, Emery alikuwa akiishi kimasikini tu pale Sevilla. Hakukuwa na bajeti yoyote kubwa ya usajili.

Sevilla ni timu ya kawaida pale Hispania. Haina ubavu kama Barcelona na Real Madrid, japokuwa imekuwa mshindani wao kwa nyakati fulani. Ni ngumu Sevilla kufanya usajili wa nguvu.

Mara nyingi Emery alifanya usajili wa wachezaji kutoka timu za kawaida, akawatengeneza na kuwa mastaa wakubwa.

Pamoja na kuishi maisha hayo ya kimasikini, aliitengeneza Sevilla kuwa timu tishio Ulaya. Mafanikio yake makubwa kama kocha aliyapata pale Sevilla. Aliitawala Europa Ligi akiwa na Sevilla. Huyu ndiye Emery Unai.

Alifundisha pia timu nyingine za kawaida kama Spartak Moscow, Valencia na Almeria.

Kote huko hakukuwa na ufahari wa kusajili majina makubwa. Ni ngumu kocha kumtaka staa fulani na kumpata. Hata hivyo alipambana.

Rekodi zake za nyuma hazinipi shaka hata kidogo. Alifanya vizuri na timu ndogo na kubwa pia. Ukiweza kutamba ukiwa Sevilla, unashindwaje kufanya vizuri na Arsenal? Ni ngumu.

Emery ana nafasi kubwa ya kufanya vizuri na Arsenal. Nina sababu nyingi za kuamini hivyo. Sina shaka naye hata kidogo.

Sababu ya kwanza ni rekodi mbovu ya Wenger. Kufundisha Arsenal kwa sasa wala sio presha kubwa. Haina mafanikio makubwa kwa miaka ya karibuni zaidi ya kushinda tu mataji ya FA.

Kazi kubwa ya kwanza kwa Emery ni kuirejesha Arsenal ndani ya nne bora. Sio kazi ngumu sana. Wenger ameshindwa kwa miaka miwili mfululizo. Ni kazi inayowezekana kwa Emery.

Arsenal haina malengo makubwa Ulaya kama PSG. Lengo la pili kubwa kwa Arsenal ni kushinda taji la EPL. Wamelikosa taji hilo kwa miaka 14 sasa. Ni kazi ambayo haina presha kubwa sana kuifanya.

Unapofundisha timu ambayo ilipata mafanikio miaka mingi nyuma, unakuwa na presha ndogo. Sio kama David Moyes alivyoipokea Manchester United kutoka kwa Sir Alex Ferguson. Aliipokea ikiwa ya moto. Ilikuwa imetoka kushinda EPL.

Miaka miwili nyuma ilikuwa imetoka kucheza fainali ya UEFA. Miaka michache tu nyuma ilikuwa imetoka kushinda taji la UEFA. Ilikuwa na presha kubwa na ndiyo maana Moyes alichemsha.

Ni tofauti na Arsenal. Emery ameipokea ikiwa imetoka kudorora. Kitu chochote kidogo atakachokifanya kitaonekana kuwa na maana kubwa.

Hili ndilo linanifanya niamini kuwa timu hiyo itakuwa vizuri msimu ujao.

Yote kwa yote sasa naiona EPL mpya. Huku Pep Guardiola, kule Jose Mourinho, hapa Jurgen Klopp na pale Emery. Inapendeza sana. Nasikia na yule Kocha wa Napoli, Maurizio Sarri naye yuko mbioni kumrithi Antonio Conte pale Chelsea.

EPL imekuwa tamu. Ila huyo Guardiola atawanyoosha sana.