Uzi mpya Simba moto, yatua Bongo kibabe

KIKOSI cha Simba kimerejea nchini usiku wa kuamkia jana Jumatatu wakitokea Uturuki na mchana wake mabosi wa klabu hiyo watautambulisha uzi mpya ambao utatumiwa na timu hiyo katika mechi zake za msimu wa 2018-2019.

Katika utambulisho huo nyota wa timu hiyo akiwamo Nahodha John Bocco, James Kotei, Emmanuel Okwi na Nicholas Gyan ndio waliotumika kuonyesha uzi huo na kama ilivyokuwa msimu uliopita nyumbani zitakuwa nyekundu na ugenini nyeupe.

Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ kabla ya kuonyesha uzi huo mpya alitangaza kuingia mkataba na kampuni ya A1 Production Limited inayotengeneza kinywaji cha MO Energy utakaokuwa na thamani ya Sh 250 milioni.

“Tumeingia mkataba huo na tunawakaribisha kampuni nyingine kuja kufanya uwekezaji katika timu yetu, “ alisema Try Again.

“Pesa tulizopata kutoka udhamini huu tunazipeleka moja kwa moja katika uwanja wetu wa pale Bunju na habari njema ni kwamba tumekubaliana na mwekezaji Mohammed Dewji ‘MO’, ambaye ataweka pesa na mara moja tunaanza ujenzi,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa A1 Production, Sudi Mwanasala alisema mkataba huo ni wa mwaka mmoja kama mambo yataenda vyema watauongeza wa sasa utakapoisha.

“Thamani ya mkataba ni Sh 250 milioni na tunaimani kubwa tutapata matangazo ya kutosha kwani Simba ni sehemu kubwa ya matangazo hapa nchini, “ alisema Mwanasala.

Katika hatua nyingine Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alifafanua kuwa baada ya Simba kuziba miaya ya wapigaji, wanaamini watavuna zaidi ya Sh 300 milioni tofauti na Sh 200 walizokuwa wakipata awali. “Tunaomba wepenzi na wanachama wa Simba kununua jezi zao ambazo si zile feki na zitauzwa sehemu maalumu kwa Sh 25,000 tu na zitaanza kuuzwa Jumanne (leo) kwa Dar na baadaye zitakuwa nchi nzima,” alisema Manara, aliyedokeza mipango ya kuanzisha gazeti la klanbu la Simba Nguvu Moja na kuzika yote yaliyokuwa zamani.

Katika hatua nyingine kikosi cha Simba waliokuwa kambini Uturuki walipojichimbia katika mji wa Kaptepe, wakijifua kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na michuano mingine itakayoshiriki na usiku wa kuamkia jana Jumatatu wamerejea.

Mwanaspoti lililokuwa sambamba na timu hiyo Uturuki, pia ndio waliowapokea usiku huo wa manane kwenye Uwanja wa Kimataifa ya JNIA na kushuhudia msafara huo wa nyota wakiongozwa na Kocha Mkuu Patrick Aussems.

Kigogo mwingine wa Simba aliyekuwapo uwanjani hapo ni Mulamu Nghambi Mjumbe wa Kamati ya Mabadiliko ya Simba, aliyekuwa sambamba na mkewe pamoja na dereva wa Kocha Mkuu wa Simba.

Nyota wa klabu hiyo walionyesha kufurahia safari yao ya Ulaya na kuahidi kuliamsha dude kuanzia kesho Jumatano watakapovaana na Asante Kotoko ya Ghana katika hitimisho ya Simba Day kwenye Uwanja wa Taifa.

KUHUSU FC E KSAIFA

Ikiwa kambini nchini Uturuki, kikosi cha Simba kilicheza mechi za kijipima nguvu, ambapo mastraika wake Emmanuel Okwi na Meddie Kagere walitupia kwenye ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya FC E Ksaifa ambayo imepanda daraja kushiriki Ligi Kuu ya Palestina msimu huu.

Hata hivyo, katika toleo letu la jana, tuliandika kimakosa kuwa timu hiyo inaundwa na muungano wa madereva wa teksi mjini Kartepe. Ukweli kuwa FC E Ksaifa ni miongoni mwa 14 zilizopiga kambi kwenye Hoteli ya Green mjini Kartepe, sambamba na Simba.