Utata ulioibuka uchaguzi wa Simba umalizwe kiungwana

Muktasari:

  • Uchaguzi wa Simba ilishindwa kuwasilisha mapema kalenda ya uchaguzi huo, huku baadhi ya kanuni za uchaguzi kwa mujibu wa Katiba ya Simba kukinzana na zile za TFF kama wasimamizi wa soka la Tanzania.

MCHAKATO wa Uchaguzi Mkuu wa Simba uliopangwa kufanyika Novemba 3, umeingia dosari baada ya Kamati ya Uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza kusitisha.

Kamati hiyo iliyopo chini ya Revocatus Kuuli, imetangaza hatua kwa madai kuwa, Kamati ya Uchaguzi wa Simba ilishindwa kuwasilisha mapema kalenda ya uchaguzi huo, huku baadhi ya kanuni za uchaguzi kwa mujibu wa Katiba ya Simba kukinzana na zile za TFF kama wasimamizi wa soka la Tanzania.

Moja ya kanuni zilizoainishwa na Kamati ya Kuuli ni ile ya gharama za fomu za wagombea, na Kamati ya TFF inasema kwa nafasi ya juu ya uongozi yaani Uenyekiti ama Urais, haizidi Sh 200,000, huku Simba ikitoza Sh500,000.

Kwa nafasi ya Ujumbe TFF inaainisha haizidi Sh 100,000, lakini Simba yenyewe imewapiga wagombea Sh 300,000 na pia hata kampeni zimevuka ule muda uliopo katika Katiba ya TFF ya kufanywa kwa siku tano.

Simba wenyewe wamedai kampeni za Simba kufanywa kwa mwezi mmoja na mambo mengine ambayo ni wazi yameufanya uchaguzi huo kuingia dosari kama ilivyotabiriwa baada ya kuibuka kwa wanachama kuanza kuulalamikia.

Kuuli amekiri Katiba ya Simba (ambayo Mwanaspoti imekuwa ikiichapisha tangu ulipotangazwa uchaguzi huo) ina upungufu, japo hakupenda kuingilia sana na kusisitiza lazima Kamati ya Uchaguzi ya Simba kukutana nao ili kuujadili uchaguzi huo ambao jioni ya jana ulikuwa ukiingia kwenye hatua ya usaili.

Mwanaspoti kama mdau mkubwa wa michezo hususani soka, bado tunaamini jambo hili linaweza kutatuliwa mapema na Simba kuendelea na uchaguzi wake kama walivyopanga.

Kitu muhimu ni kila mmoja kutekeleza wajibu wake, Kamati ya TFF kuwajulisha kimaandishi wenzao wa Simba, kisha Kamati hiyo ya Simba kuangalia mambo yua kurekebishwa mapema ili mambo yao yaendelee kama kawaida.

Tunaamini muda upo wa kutosha wa kufanyika kwa marekebisho katika baadhi ya mambo yaliyoibua utata na suala la kulalamikiwa kwa Katiba na baadhi ya wanachama wa Simba ni kutaka kufukua makaburi tu kwa sasa.

Hii ni kwa sababu rasimu hiyo ya katiba ilijadiliwa na kupitishwa na wanachama kwenye mikutano halali kabla ya kwenda kuidhinishwa kwa Msajili Mkuu wa Vyama vya Michezo nchini kuifanya Simba iwe na Katiba Mpya ya Mwaka 2018.

Katika suala la utata wa vipengele vya ada, muda wa kampeni na mengine yapo chini ya kamati hizo yaani Kamati ya Simba na ile ya TFF.

Inawezekana kuna baadhi ya watu wakafurahia hili lililojitokeza sasa kwa sababu walishaanza kuutulia shaka uchaguzi huo kwa jinsi kamati ilivyokuwa ikuiendesha mambo yake kwa usiri mkubwa hata kuanika majina ya waombea.

Lakini pia kuwa watakaovurugwa kwa tamko hilo la kamati ya Kuuli kama ni kutaka kuwaharibia uchaguzi wao, lakini yote kwa yote meza ya mzungumzo ipo kwa nia ya kuleta suluhisho na pande hizo zikiafikiana bado uchaguzi unaweza kufanyika kama ulivyopangwa.

Kitu kizuri ambazo Mwanaspoti kinafurahia ni kwamba viongozi wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba chini ya Mwenyekiti, Boniface Lyamwike alinukuliwa wakati akitangaza uchaguzi huo kwa kusema;

“Katiba itakayotumika ni ya mwaka 2018 inayotambulika kisheria na imepitishwa na msajili wa vyama na klabu za michezo, lakini kwa kuwa Simba ni mwanachama wa TFF pale ambapo kutaonekana kuna upungufu, tutalazimika kutumia Katiba ya shirikisho.”

Hii inathibitisha kuwa, bado yaliyoainishwa na Kamati ya Kuuli yana mantiki na wajibu wa kamati ya Lyamwike ni wajibu wao kulimaliza suala lao kiungwana.

Kila mara inapotokea tofauti, shurti kumalizwa kiungwana na kila mmoja kuridhia na kufanya kile kinachopaswa kufanyika.

Hatutarajii tena kuona unaibuka mgogoro mkubwa na hata uchaguzi kushindwa kufanyika.