Tumeachana na Ninje kisomi ila ametuangusha

MUDA haujawahi kusema uongo. Tangu enzi za Yesu Kristo na Mtume Muhammad (SAW) mpaka sasa muda ndio shahidi wa kweli. Jambo lolote gumu lipe muda, utapata ufumbuzi wake.

Ni kama tunavyomalizana na Ammy Ninje sasa. Aliibuka ghafla. Akawa na nguvu kubwa kwenye soka letu. Nguvu yake ilikuwa kubwa.

Hakuna ubishi kuwa Ninje ni kocha mwenye wasifu mkubwa. Kwenye makaratasi, unaweza kumpa timu yoyote nchini. Siyo bure watendaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) waliamua kumpa timu mbalimbili ndani ya miezi minne tu. Ukisoma wasifu wake, lazima umpe timu.

Hapa nchini hatuna makocha watano wenye vyeti bora kama vya Ninje. Makocha wengi nchini wana vyeti vya kawaida tu. Vyeti vya Ninje ni sababu tosha ya kumpa timu. Hata kama ningekuwa pale TFF, ningempa pia timu.

Nani asiyependa kufanya kazi na makocha wasomi? Hakuna. Tunawapenda makocha wetu wasome zaidi na zaidi. Tutawalazimishaje kwenda kusoma? Ni kuwatambua hawa kina Ninje na kuwapa timu mbele yao.

Bahati mbaya Ninje ametupa wakati mgumu. Ametuangusha. Alituangusha kule Kenya kwenye michuano ya Chalenji na ametuangusha sasa.

Hatuwezi kumtetea tena. Tunaachana naye kisomi sasa.

Mwanzo ilibidi tutumie nguvu kubwa kumtetea Ninje. Alichofanya uwanjani kilikuwa tofauti na wasifu wake wa kwenye makaratasi. Alionekana kuwa na upeo mkubwa lakini timu yake haikuweza kucheza vizuri. Pengine anafundisha mambo magumu kwa wachezaji wetu wanaopenda vitu vyepesi.

Ilibidi tujifiche kwenye upande huu wa pili. Tuliamini kwamba Ninje ni kocha bora wa vijana. Ndio kazi aliyokuwa akiifanya pale England. Ndio kazi aliyokuwa akiifanya pale Hull City kwa miaka nenda rudi.

Unaachaje kumpa timu ya vijana kocha Mtanzania aliyewahi kuifundisha timu ya vijana ya Hull City? Huwezi. Utampa nani kama siyo yeye? Hakuna. Ilibidi tumpe timu Ninje tu.

Kulikuwa na sababu nyingi za kumpa Ninje timu ya vijana chini ya miaka 20. Kwanza, timu hiyo haina mafanikio makubwa yoyote. Haijawahi kufanya jambo lolote kubwa la kujivunia. Tuliamini kuwa huenda Ninje akawa wa kwanza kutupeleka nchi ya ahadi.

Pili, timu za vijana ndio eneo sahihi kwa Ninje. Amejifunza ukocha akiwa kwenye timu za vijana. Amefundisha timu za vijana kwa miaka yake yote. Ilibidi tumpe kazi kwenye eneo alilobobea zaidi. Bahati mbaya ameshindwa kufanya vizuri pia.

Ni wazi sasa Ninje hatufai tena. Kule kwa wakubwa alichemsha, na huku kwa watoto amezingua. Hatuna sababu ya kumtetea tena. Muda umetuonyesha uwezo wake halisi. Amechemka

Kuna sababu nyingi za Ninje kufanya vibaya na timu zetu. Kwanza, hajawahi kufundisha soka hapa nchini. Hawafahamu vizuri wachezaji wa Tanzania. Yupo Tanzania lakini akili yake ipo England.

Anafundisha mambo ya Kizungu ambayo hapa Bongo ni nadra kufanikiwa. Soka la Tanzania na Afrika liko kivyake. Siyo kama lile la Ulaya. Ndio maana timu nyingi zikisaka kocha zinaweka wazi kuwa zinahitaji mwenye uzoefu mkubwa na soka la Afrika. Umewahi kujiuliza kwanini?

Pili, timu zetu za taifa bado hazijawa na msingi mkubwa kama zile za Ulaya.

Mfano Ulaya utakuta mchezaji ameanzia timu ya vijana chini ya miaka 11, 13, 15 na 17. Unapokutana naye kwenye timu ya vijana chini ya miaka 20 kazi yako inakuwa nyepesi.

Hapa kwetu tuna wachezaji waliotoka kwenye ile Serengeti Boys ya Gabon tu. Hatuna msingi wa timu za vijana chini ya miaka 15 wala 13. Wachezaji wengi wanaibukia vichochoroni na kuwa mastaa wakubwa tu kwa jitihada zao.

Hili nalo limempa changamoto Ninje. Alikuwa anawapa elimu kubwa watu waliosoma kidogo. Yaani ni kama kufundisha vitu vya Chuo Kikuu kwa wanafunzi walitoka darasa la saba. Wanaweza kuelewa vichache ila siyo vyote.

Kama Ninje anahitaji kufanya kazi hapa nchini, ni muda mwafaka kwake kuanza kujifunza kuhusu soka la Tanzania. Ni muda wake kuanza kujifunza kuhusu wachezaji wa Tanzania.

Asitishwe na vyeti vyake vikubwa. Ashuke chini na kuanza kujifunza upya. Yawezekana miaka miwili ijayo akawa kocha mkubwa zaidi hapa nchini na akatupa mafanikio.

Yawezekana miaka mitatu ijayo akawa kocha mkuu wa Taifa Stars na kufanya vizuri. Kuanguka siyo mwisho wa kujaribu. There is always next time Ninje.