fainali

Muktasari:

  • City waliteketea mabao 3-0 kutoka kwa Liverpool katika pambano la robo fainali Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, lakini leo wanaweza kutawazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu England kama wakiwachapa wapinzani wao Manchester United katika dimba la Etihad.

MANCHESTER, ENGLAND

NI kama fainali. Pep Guardiola na Manchester City yake wamechafuliwa sana Anfield Jumanne usiku, lakini leo huenda wakamaliza shughuli ndefu ya Ligi Kuu England iliyoanza Mei mwaka jana na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England.

City waliteketea mabao 3-0 kutoka kwa Liverpool katika pambano la robo fainali Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, lakini leo wanaweza kutawazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu England kama wakiwachapa wapinzani wao Manchester United katika dimba la Etihad.

City wapo mbele ya United kwa pointi 16 na endapo watashinda pambano la leo watafikisha pointi 87 ambazo hazitaweza kufikiwa na Manchester United ambayo kama ikishinda mechi zote itafikisha pointi 86 tu.

Staa wa zamani wa Arsenal na timu ya taifa ya England, Paul Merson amedai anatarajia City kushinda katika mechi ya leo ingawa anaamini Kocha wa United, Jose Mourinho atapaki basi na hatacheza kama Liverpool walivyofanya Jumanne usiku.

“Natarajia Man City kushinda. Kama ukisema kwa Man United ni suluhu ya 0-0 wanaweza kukukata mkono. Nadhani United wataingia uwanja kwa ajili ya kusaka suluhu lakini sioni ni kwa namna gani City watashindwa kuwafunga ndani ya dakika 90.

“United haitacheza kama Liverpool ilivyocheza. Hawana ubavu wa kufanya hivyo uwanjani,” aliongeza Merson na kukiri kipigo walichopewa City na Liverpool kinaweza kuwachanganya.

“Uwezo wa kujiamini wa City utakuwa umeyumba kiasi. Watakuwa wamepoteza uwezo mwingi wa kujiamini baada ya kichapo kile cha Liverpool. Hawakaupiga shuti lolote katika lango. Timu pekee ambayo inaweza kuisumbua City ni Liverpool kwa sababu ndio timu pekee ambayo inaamua kucheza mpira dhidi ya City,” aliongeza Merson.

“Ninadhani timu nyingine zinaogopa. Wanakwenda katika mechi dhidi ya City na wanaonyesha heshima kubwa sana, lakini mafanikio ya Liverpool yanaanzia kwa watu wake watatu wa mbele. Wana mbio sana na wanarudi nyuma kwa haraka.”

Katika pambano la leo, mwamuzi anatarajiwa kuwa Martin Atkinson na kuna uwezekano kocha, Jose Mourinho akawa mnyonge baada ya kusikia jina la mwamuzi aliyeteuliwa kuchezesha mechi hiyo.

Mourinho alikerwa na kiwango cha mwamuzi huyo katika pambano kati ya Manchester United ugenini kwa Chelsea Stamford Bridge msimu uliopita ambapo alishindwa kumtoa nje kwa kadi nyekundu mlinzi, David Luiz kwa kumnyanyulia daluga kiungo, Marouane Fellaini.

“Ilikuwa mechi kubwa kwa klabu zote mbili na tulihitaji mwamuzi atoe haki. Tunataka mwamuzi imara lakini hatukumpata. Sijui kwa nini alipewa mechi hiyo. Lazima niseme nilipoona mwamuzi ni yeye nilihofia sana,” alisema Mourinho mara baada ya pambano hilo.

Kama vile haitoshi, mwamuzi huyo alimtoa nje kwa kadi nyekundu Fellaini kwa kumpiga kichwa mshamabuliaji, Sergio Aguero katika pambano ambalo lilimalizika kwa suluhu ya 0-0 Old Trafford.

Si Mourinho tu ambaye amewahi kumlalamikia mwamuzi huyo. Kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson naye aliwahi kumlalamikia mwamuzi huyo katika pambano la robo fainali za FA mwaka 2008 wakati alipowanyima penalti kutokana na kitendo cha mlinzi, Sylvain Distin kumwangusha Cristiano Ronaldo.

“NI ujinga na siwezi kuelezea hili. Waamuzi wanafukuzwa kwa sababu ya mambo kama hayo lakini yeye ataenda kuwa mwa muzi wa mechi nyingine wiki ijayo,” Alisema Ferguson.

Hata hiyo, licha ya kulaumiwa huko lakini United imekuwa na bahati pindi mwamuzi huyo anapochezesha mechi za watani hao wa jadi. Katika mechi nne zilizopita alizochezesha miaka ya 2009, 2010, 2012 na 2017 United ilishinda mechi tatu na kutoa suluhu moja ya bila kufungana msimu uliopita.