Yatakayoibeba Yanga leo Taifa

Muktasari:

  • Yanga ilihamishiwa kwenye Kombe la Shirikisho baada ya kufungwa na Township Rollers ya Botswana katika Ligi ya Mabingwa Afrika hivyo ni fursa ya kurekebisha makosa yao.


YANGA inashuka katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam dhidi ya Welayta Dicha ya Ethiopia leo Jumamosi ikiwa ni mechi ya kwanza ya kusaka tiketi ya kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na kama hesabu zitakwenda vibaya basi mambo yatakuwa tofauti.

Yanga ilihamishiwa kwenye Kombe la Shirikisho baada ya kufungwa na Township Rollers ya Botswana katika Ligi ya Mabingwa Afrika hivyo ni fursa ya kurekebisha makosa yao.

Hakuna ubishi kuwa Yanga inatakiwa kupambana kiume kuhakikisha inalinda heshima yake kubwa Afrika kwa kuwaondosha Waethiopia hao ambao wanashiriki michuano ya Afrika kwa mara ya kwanza.

Mwanaspoti limeifanyia uchunguzi Dicha na kubaini mambo kadhaa ambayo Yanga wanapaswa kuyazingatia kama kweli wanahitaji ushindi.

Dicha wasimiliki mchezo

Dicha sio timu kongwe lakini kikosi chao kina ubora wa kiufundi na hiyo inabaki kama silaha yao kubwa kuelekea kwenye mechi hiyo.

Yanga hawatakiwi kuwaruhusu Dicha wamiliki mpira kwa muda mrefu hasa katika safu yao ya kiungo. Kazi ya kukaba inatakiwa ifanyike kwa ustadi mkubwa kisha kuwashambulia kwa haraka ili kuwapa wakati mgumu lakini pia Yanga wanatakiwa kutulia na pasi zao kutokana na namna wapinzani wao wanajua kucheza kwa kuziba nafasi.

Kuwapunguza kasi

Dicha hawachezi soka la kuremba hasa wanapokuwa ugenini wanacheza soka la kujihami na kushambulia kwa kushtukiza na mashambulizi yao zinapigwa pasi chache tu na tayari wanakuwa wamefika lango la mpinzani.

Mabeki na viungo wa Yanga wanatakiwa kuacha kuzubaa kama walivyofanya katika mchezo wa kwanza dhidi ya Township Rollers vinginevyo watalizwa mbele ya mashabiki wao.

Ubaya zaidi ni kwamba hao Dicha wana miili midogo lakini soka lao ni hatari. Ukiwaona unaweza kuwadharau kutokana na aina ya miili yao, ila ukweli Yanga wanatakiwa kutambua wachezaji wa Dicha wanaweza kukuingiza mkenge kama ilivyowatokea Zamalek ambayo ilijikuta ikiondoshwa na Waethiopia hao bila kutarajia.

Licha ya kuwa na miili midogo lakini soka lao ni kubwa hasa wanapofanikiwa kuwakamata kwa kucheza soka lao la pasi za haraka. Yanga wanatakiwa kuanza pambano kwa kasi na kupata mabao ya kutosha kuwapa kazi mapema na sio kutangulia kuwadharau wapinzani wao.

Mashuti yao balaa

Ukuta wa Yanga unaweza kuwa chini ya kipa Youthe Rostand, Hassan Ramadhan Kessy, Andrew Vincent ‘Dante’ Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Gadiel Michael kutokana na kukosekana kwa waandamizi kama Kelvin Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro.

Wanachotakiwa kukijua ni kwamba Dicha wakikaribia golini wanafanya kitu wenye uhakika nacho kama sio kupiga pasi za kuua (killer pass) basi wanapiga mashuti makali na kazi hufanywa na washambuliaji wao na hata viungo.

Kuisaidia safu ya ulinzi ya Yanga viungo wa timu hiyo Raphael Daudi,Thabani Kamusoko na hata mawinga Yusuf Mhilu na Ibrahim Ajib wanatakiwa kuwa sehemu ya ukabaji wakati timu yao imepoteza mpira.

Kiungo, ushambuliaji noma

Yanga inatakiwa kuwa makini na mtu anayeitwa Arafat Djako ambaye anajua kucheza vyema na viungo wake lakini kazi kubwa kwa Yanga ni kuhakikisha wanategua mitego ya viungo wa wapinzani wao hao ambao ni rahisi kwao kuongeza nguvu kwa Arafat na kuzalisha mashambulizi makali.

Yanga wanatakiwa kumaliza mchezo huu hapa hapa nyumbani kwani sio kitu rahisi kushinda ugenini kutokana na mazingira ya Ethiopia kuwa magumu. Kufanikiwa hilo wanatakiwa kupata mabao mapema na mengi.

Ushindi mkubwa kwa Yanga bila wao kuruhusu bao unaweza kuwa mtaji muhimu kwao kuelekea mchezo wa marudiano utakaopigwa Aprili 18 kule Ethiopia ambako hali ya hewa nzito inaweza kuwa tatizo kubwa kwa Yanga muhimu kupata mabao ya kutosha nyumbani kisha ikajipange ikiwa ugenini.