Yanga yampangia Mdoli chumba!

Muktasari:

  • Mwanaspoti imekitembelea kikundi hicho cha Yanga Kidali chenye makao yake makuu, Tandale kwa Mtogole jijini Dar es Salaam na kuongea mwenyekiti kundi hilo, aliyejitambulisha kwa jina la Salum Habibu, alifunguka mengi kuhusu mdori huyo.

UNAWEZA ukachukulia poa vibwanga na vibweka vya mashabiki au vikundi kibao vya soka la Bongo, ila sio kwa Yanga Kidali. Unaambiwa wana mdoli wa kuamsha popo uwanjani wenye baraka za Padri kutoka Italia. Kama ni mhudhuriaji mzuri wa mechi za Yanga na umekuwa ukijichanganya na mashabiki mbalimbali, basi inawezekana ukawa umeonana na mashabiki wa kundi la Yanga Kidali wakiwa na mdoli ila usijue una miujiza gani. Sio mdoli wa mchezo ule, una bonge la stori namna ulivyopatikana kutoka kwenye taifa la Italia ambalo lilitawazwa Wafalme wa soka wa Dunia 2006 nchini Ujerumani, baada ya kuifunga Ufaransa kwa mikwaju ya penalti 5-3 baada ya sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90.

Mwanaspoti imekitembelea kikundi hicho cha Yanga Kidali chenye makao yake makuu, Tandale kwa Mtogole jijini Dar es Salaam na kuongea mwenyekiti kundi hilo, aliyejitambulisha kwa jina la Salum Habibu, alifunguka mengi kuhusu mdori huyo.

MDOLI UNA MENGI

Mdoli wa Yanga, ulionekana machoni kwa mashabiki wa timu hiyo, ukiwa umewekwa kwenye akaunti ya Padri Mtanzania ambaye yupo Italia kama Father Christmas, Desemba 25, mwaka 2011. Kikundi cha ushangiliaji cha Yanga Kidali chini ya Mwenyekiti Habibu, kikautamani mdoli huyo na kuamua kumuandikia ujumbe Padri, aliyetajwa kwa jina moja la Mpeka, ili awapatie kwa ajili ya amsha amsha uwanjani.

Miezi mitatu badaye Padri Mpeka, aliwatumia mdoli huyo, akiwa kama Father Christmas na Mwenyekiti wa kikundi hicho, Habibu alienda kuuchukua makao makuu ya NSSF jijini Dar es Salaam. Kwa kuwa ulikuwa kwenye mwonekano wa Father Christmas, wakaubadilisha sura na kuweka nyingine, wakatoa nguo nyekundu na kumvalisha za kijani kisha wakampa jina la ‘Super Mkong’oto’ kwa kuwa Yanga kipindi hicho ilikuwa kwenye ubora wa hali ya juu uwanjani.

Mwenyekiti wa kundi hilo, Habibu anaeleza kasheshe baada ya kuubadilisha hakuna mtu aliyepata ujasiri wa kuutunza kwa kuwa walikuwa wanaogopa na kuamua kuupangishia chumba.

“Kila mtu alikuwa anaogopa kwenda naye kwake, akihofia watoto kutokana na ukubwa wake, tukakubaliana kwa pamoja kumtafutia chumba cha wakati huo, tulikuwa tunakilipia Shilingi 40,000, ila kwa sasa mambo magumu tumemtafutia cha Shilingi 30,000 kila mwezi,”anasema.

Anasema wanaposafiri mechi za mikoani, mdoli huo wanamchukulia chumba kwenye nyumba ya kulala wageni, ili kuhakikisha anakuwa salama na haibiwi.

MAVAZI YAKEi

Anaeleza kwamba kila msimu wanamshonea nguo zenye thamani ya Shilingi 70,000 na wamejipanga mechi ya watani wa jadi Aprili 29, atokelezea na mavazi mapya.

“Tumeamua kuipa nafasi mechi ya watani ndio maana tunamshonea nguo mpya, lakini inapotokea tumefungwa kila mmoja anakua anaona mzito kuubeba kuogopa kejeli,” anasema

MASTAA WAJITOKEZA

Mastaa wa Yanga, Hassan Kessy, Juma Abdul, Papy Tshishimbi, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Malimi Busungu na Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Boniface Mkwasa wamewahi kutembelea maeneo alipo mdoli huyo.

“Mara nyingi Mkwasa anatutia moyo na anakuja hapa kusalimia wanachama, hii inaonyesha kuwa ametutofautisha na wengine,” anasema.