NINAVYOJUA: Yanga wakubali Manji mkubwa kuliko klabu yao

Joseph Kanakamfumu 

Muktasari:

Ndiyo, haya ni maneno yaliyobuniwa tangu siku nyingi enzi hizo Yanga inaanzishwa, yakiwa na lengo la kumfanya yeyote anayetaka kujihusisha na Yanga, iwe kuwa mwanachama, kuwa kiongozi au kuwa mchezaji na hata shabiki, kuelewa kuwa masilahi ya klabu ndiyo yanayopaswa kuzingatiwa kwanza.

YANGA kwanza mchezaji baadaye! Yanga Kwanza kiongozi au mwanachama baadaye! Yanga ni kubwa kuliko mtu yeyote!

Ndiyo, haya ni maneno yaliyobuniwa tangu siku nyingi enzi hizo Yanga inaanzishwa, yakiwa na lengo la kumfanya yeyote anayetaka kujihusisha na Yanga, iwe kuwa mwanachama, kuwa kiongozi au kuwa mchezaji na hata shabiki, kuelewa kuwa masilahi ya klabu ndiyo yanayopaswa kuzingatiwa kwanza.

Ni maneno yaliyobuniwa kuifanya klabu ionekane kuwa na nguvu kubwa mbele ya jamii, ijapokuwa kwa hali inavyoonekana sasa linaweza kuwa somo jingine kwa wanachama wa klabu hiyo.

Hali hii imenifanya nikumbuke maneno mengi yaliyosemwa na wale wenzangu na mimi ambao hata kuichangaia klabu shilingi mbili kwa siku hawawezi, ila domo lao ndilo linawafanya kuwa na kiburi huku wakilishwa maneno na baadhi ya watu walio na mawazo mgando kuwa Yanga ni kubwa kuliko mtu yeyote.

Yalisemwa haya baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu yao, Yusuf Manji kuandika barua ya kujiuzulu. Kama kawaida, wasio na fikra za karne hii waliendelea kushikilia msimamo wao kuwa Yanga ni kubwa kuliko Manji. Siku hazigandi na leo hii tumeona ukubwa wa Yanga uko wapi. Yanga hii ya wanachama walioshindwa kuwalipa mishahara Vincent Bossou na Donald Ngoma waliogoma kucheza dhidi ya Simba wakidai mishahara ya miezi miwili pesa isiyozidi Sh15 milioni.

Ukubwa wa klabu ambao huwezi kuisafirisha timu Mwanza, Shinyanga na kurudi huku klabu ikilipa posho bila tatizo. Ilibidi itumike mbinu ya kuchangisha watu kupitia mitandao.

Yanga haiwezi kuwa kubwa kuzidi watu wenye pesa kwa sababu Yanga haijawahi kuwa taasisi inayoweza kujisimamia kwenye uendeshaji wake.

Yanga haijawahi kuwa na mizizi na wala haina mizizi misingi ya jinsi ya kuendesha klabu. Yanga ina majengo yasiyoisaidia klabu kupata mapato, si kile kijumba cha Mtaa wa Mafia au Mtaa wa Twiga.

Yanga haijaweka au kuitumia misingi iliyokuwa nayo angalau ya kuwategemea wanachama. Miaka inakwenda kwa kasi huku wapenzi wa Yanga wakilipa kodi ya serikali, kuchangia jamii zinazowazunguka, kuchangia misiba, harusi lakini bado ni kazi kubwa kuichangia timu yao kwa hiari.

Manji alikuwa kila kitu ndani ya Yanga. Alifanya usajili wa gharama kubwa kwa wachezaji muhimu na alileta makocha kutoka nje ya nchi. Ni yeye ndiye aliyetoa pesa iliyotumika kuiandaa timu ndani na nje ya nchi na kuisaidia kupata matokeo iliyopata kwa miaka hii aliyokuwapo, hapo una kiburi cha kusema Yanga ni kubwa kuliko Manji! Angalia jinsi klabu isivyo na misingi thabiti ya uendeshaji.

Huku ndiko tunakwenda kuujua ukweli kamili baadaye kwani sasa ripoti ya usajili inapitiwa na viongozi wa matawi ambao hawawezi hata kuichangia klabu milioni tano.

Ndio hao wanaoipitia ripoti ya Kocha Mkuu inayohitaji watu wachache wenye ufundi wa kuangalia uhalisia na uwezo wa wachezaji waliopo, nani anatakiwa kuingia na nani atoke. Wanafanya nini hao?

Hayo yote yanahitaji nguvu ya fedha ndani ya klabu. Usajili si kitu cha mchezo mchezo. Ili kuendelea kutawala soka la kileo, ni lazima uwe na pesa. Vinginevyo hutoweza kusajili wachezaji wa kiwango cha juu.

Bila pesa huwezi kuiandaa timu vizuri na huwezi kupata mkusanyiko wa wachezaji bora watakaokupa matokeo bora na mazuri. Yanga haina ukubwa wowote kwa kutegemea watu wenye midomo tu waliokuwa wakidharau uwepo wa Manji.

Walikuwapo baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji waliodiriki kukosoa na kudharau mchango aliokuwa akiutoa Manji. Hata pale waliposimamishwa walitumia vyombo vya habari kutuaminisha kuwa Yanga ni kubwa kuliko Manji.

Hata hivyo, ndio hao hao walioshindwa kuwalipa Chirwa na Tambwe mishahara ya miezi miwili. Wapo madarakani na wameshindwa kabisa kuziba pengo la kutokuwapo kwa Manji.

Hawa ndio walioongoza kelele za kutaka Manji asipewe timu wakisema Yanga ni kubwa ingawa wameshindwa kutudhibitishia ukubwa wa klabu. Yanga ni mfano wa taasisi lakini kwa jina tu, kwani haina msingi wowote wa kuiwezesha isimame.

Nilitegemea wale waliowahi kwenda mahakamani kuzuia ukopeshwaji wa timu uliokuwa ukifanywa na Manji, watasimama sasa kuiwezesha klabu.

Enzi za klabu kuishi kwa matumaini ya ukubwa wa jina zimepitwa na wakati, hili la Yanga ni somo kuwa wale wanaotoa pesa zao kwa mapenzi kuisaidia klabu hatuna budi kuwaheshimu.