Yanga inataka kurudia kosa lile lile la 1998

Muktasari:

  • Kuna misemo ya wahenga hao imekuwa ikigusa ukweli na unaoishi milele, licha ya kuwepo kwa mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia duniani yanayozuzua. Kama kuna msemo ambao unaosema, kufanya kosa sio kosa, ila kurudia kosa ndio kosa.

JAPO kuna watu wanaowachukulia poa wahenga kwa misemo yao, wakidai eti imepitwa na wakati, ila jamaa hao walikuwa vichwa.

Kuna misemo ya wahenga hao imekuwa ikigusa ukweli na unaoishi milele, licha ya kuwepo kwa mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia duniani yanayozuzua. Kama kuna msemo ambao unaosema, kufanya kosa sio kosa, ila kurudia kosa ndio kosa.

Msemo huo unaweza kulinganisha na jambo ambalo Yanga inataka kulifanya. Ndio, Yanga imetangaza kumnyakua Kocha Mkuu, Zahera Mwinyi kutoka DR Congo, ikiwa ni siku chache tangu itinge hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Utajiuliza, Yanga imefanya kosa gani kwa kumnyakua kocha huyo Msaidizi wa Timu ya Taifa ya DR Congo ‘The Leopards’ iliyonyooshwa na Taifa Stars mwezi uliopita? Tulia!

REKODI TAMU

Yanga inastahili pongezi kwa kuitoa kimasomaso Tanzania kwa kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika 2018 pamoja na kuwa katika hali ngumu.

Yanga imefuzu makundi kwa mara ya tatu ikiwa ni rekodi kwa klabu za Tanzania, ilifanya hivyo kwa mara ya kwanza katika Ligi ya Mabingwa Afrika 1998 na kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kutinga hatua hiyo kabla ya Simba kufuata nyayo 2003. Miaka miwili tu iliyopita, Yanga ilitinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika 2016.

TATIZO LIPO HAPA

Wakati Yanga ilipofuzu kwa mara ya kwanza makundi ya Ligi ya Mabingwa 1998 ilikuwa chini ya Kocha Mkuu wa Muda, Tito Mwaluvanda ambaye alimpokea aliyekuwa Kocha Mkuu aliyetimuliwa, Mwingereza Steve McLennan. Mwaluvanda alipewa timu akiwa hana umaarufu wowote na Mwenyekiti wa Yanga wakati huo marehemu Rashid Ngozoma Matunda alimtambulisha mbele ya wanachama kama msimamizi wa mazoezi huku timu ikiendelea kusaka kocha wa uhakika.

Unajua nini kilichotokea? Kocha Mwaluvanda aliiwezesha Yanga kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Ligi Kuu ya Muungano na kuifikisha timu hatua ya makundi baada ya kuzitoa Rayon Sports ya Rwanda na Coffee ya Ethiopia. Mechi yao ya kwanza ya Kundi B ilianza nyumbani dhidi ya Manning Rangers ya Afrika Kusini na kutoka nayo sare ya bao 1-1, Wasauzi wakichomoa bao jioni kabisa.

Sare hiyo ilichukuliwa sivyo ndivyo na Mwaluvanda na msaidizi wake Fred Felix ‘Minziro’ waliondolewa kwa kigezo hawana uwezo wa kuifundisha timu katika hatua hiyo. Wakamkebehi kuwa ni msimamzi wa mazoezi tu na wakaamua kumchukua Raoul Jean Pierre Shungu aliyekuwa akiinoa Rayon iliyotolewa na Yanga katika raundi ya kwanza na kupewa Abeid Mziba ‘Tekero’ kuwa msaidizi wake.

Yanga ilifanya uhuni wa kumtimua Mwaluvanda kwa vile tayari ilishakuwa na uhakika wa kumleta Shungu raia wa DR Congo enzi hizo Zaire ambaye alishindwa kuhimili vishindo vya Kocha Mwaluvanda ambaye kwa sasa ni marehemu kwa kutolewa kwa faida ya mabao ya ugenini iliyotokana na sare ya mabao 3-3 baada ya mechi mbili.

Yanga iliamini Mcongo huyo angeipa mafanikio kuliko miujiza aliyokuwa nayo Mwaluvanda aliyewavusha salama kwenye hatua ya mtoano na kutinga makundi, huku akiwa hana jina kubwa, ila walisahau msemo wa usitupe mbachao kwa msala upitao.

AIBU TUPU

Kocha Shungu alianza kibarua chake katika mechi ya pili dhidi ya Raja Casablanca mjini Casablanca, Morocco ambako unajua nini kilichotokea huko?

Yanga ilipigwa mabao 6-0 katika mchezo ambao uliipa fedheha kubwa Vijana wa Jangwani kwani kabla ya hapo ilikuwa haijawahi kufungwa idadi hiyo katika mechi moja ya kimataifa, mbali na kipigo cha Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba mwaka 1977.

Baada ya kichapo hicho cha aibu kilichoshuhudia nahodha Kenneth Mkapa akilimwa kadi nyekundu dakika ya tatu, Yanga ilisogea Ivory Coast kuvaana na ASEC Memosas na kuambulia kipigo cha mabao 2-1.

Yanga ikaja ikaialika Raja Casablanca jijini Dar es Salaam na kulazimisha sare ya mabao 3-3 kabla ya kwenda Afrika Kusini na kulala ugenini 4-0 dhidi ya Manning Rangers kisha kuhitimisha mechi zake kwa kucharazwa nyumbani mabao 3-0 na ASEC. Kitu pekee ambacho Yanga inajivunia kunolewa na Shungu ni kuibebesha taji la Kombe la Kagame 1999 Uganda, taji la Kombe la Nyerere 1999 na Ligi Kuu ya Muungano mwaka 2000, lakini hakuiwezeshja kubeba taji la Ligi Kuu wala kutamba michuano ya Caf kwani kwa misimu yake mitatu Mtibwa Sugar na Simba zilitawala.

KOSA NI NINI?

Kwa mara nyingine tena, Yanga imetinga makundi bila ya Kocha Mkuu, kwani Mzambia George Lwandamina alibwaga manyanga kutokana na hali tete iliyopo ndani ya klabu hiyo na kurejea kwao Zambia akijiandaa kurudi tena Zesco United. Kuondoka kwa Lwandamina sio ishu sana, ila tatizo ni kwamba Yanga kurejea tena kosa kama la mwaka 1998 kwa kumnyakua kocha kutoka DR Congo, huku ikipangwa kwenda kuanza ugenini dhidi ya Waarabu kama ilivyokuwa miaka 20 iliyopita.

Yanga iliyopangwa Kundi D itaanza karata zake kwa kuwafuata USM Alger ya Algeria katika mechi inayotarajiwa kuchezwa Mei 6, huku ikiwa na kocha mkuu mpya, Zahera Mwinyi aliyenyakuliwa kutoka DR Congo. Ikitoka hapo itacheza na Gor Mahia ya Kenya na Rayon Sports ya Rwanda na kuamua hatma yao kutinga robo fainali.

Rekodi zinaonyesha, Yanga haijawahi kufanya vizuri chini ya makocha wa Kicongo zaidi na ilivyokuwa kwa Babu Tambwe Leya ambaye kwa sasa ni marehemu.

Shungu na mwenzake Jean Polycarpe Bonganya wote walitua Jangwani, lakini waliishia patupu kwa kushindwa kuipa mafanikio ya kujivunia hasa kimataifa na katika Ligi Kuu na Bara, lakini ni kama vile mabosi na Wanayanga wameisahau historia.

NINI KIFANYIKE?

Hata ukirejea rekodi za Zahera hana kitu cha kusisimua katika maisha yake ya ukocha hata kama jambo hili Wanayanga hawatapenda kulisikia. Lakini kwa Yanga ndio yenye maamuzi ya kocha gani ainoe timu yao, basi ni lazima wamvumilie Kocha Zahera na wasitarajie miujiza katika muda mfupi alionao katika kikosi hicho kabla ya kuanza ngarambe zake za mechi za makundi ya Shirikisho Afrika.

Licha ya uzoefu alionao Kocha Zahera wa kucheza na kufundisha soka Ulaya na barani Afrika, bado ni vigumu kumtabiria mapema kuwa ataleta miujiza Jangwani, hata kama ni kweli soka wakati mwingine huwa na matokeo ya ajabu na kubebwa na bahati.

Inawezekana ni kweli Lwandamina amewazingua kwa kuondoka kienyeji baada ya kushindwa kutekelezwa mahitaji yake, lakini Mzambia huyo alistahili zaidi kuwepo ndani ya Yanga ili kumaliza ngwe hii aliyoianzisha kwa jasho na damu.

Hata hivyo, kwa kuwa Mzambia ameshasepa na tayari wamemnasa Mcongo, Yanga inapaswa ijipange kusaka kocha mkuu mpya ambaye atakuja kuiletea mafanikio zaidi, kwa sababu kilichoipata Caf ikiwa chini ya Shungu kinaweza kutokea tena kwa Zahera. Sitashangaa kama timu hiyo haitavurunda katika hatua hii pamoja na ushujaa wote iliouonyesha hadi kufikia hatua hiyo ya makundi.

Tusibiri tuone, ila ukweli ndio huo hata kama unauma.