Yanga ikemee pepo la umasikini kwa nguvu zote

Muktasari:

  • Miongoni mwa sifa ambazo tajiri anazo ni kuiheshimu pesa. Kiwango chochote cha pesa kiwe kidogo ama kikubwa kina thamani kwa tajiri.

MATAJIRI na masikini wanatofautiana sana na wala hakuhitajiki upeo mkubwa au elimu ya kiwango cha shahada ya uzamivu kujua tofauti iliyopo baina ya tajiri na masikini.

Miongoni mwa sifa ambazo tajiri anazo ni kuiheshimu pesa. Kiwango chochote cha pesa kiwe kidogo ama kikubwa kina thamani kwa tajiri.

Ni nadra kuona tajiri anaidharau fedha eti kwa sababu ni ndogo na ndio maana sio jambo la kushangaza kuona wafanyabiashara na mabilionea wakubwa kama Said Salim Bakhressa, Mohammed Dewji ‘MO’, Yussuf Manji, Reginard Mengi na Salim Asas wakifanya biashara ya bidhaa zinazouzwa kwa kiasi kidogo cha fedha wakiamini hata fedha ikiwa ndogo, ina thamani kubwa.

Usidhani kwamba matajiri hawa hawako timamu kufanya biashara ya vitu vidogo vidogo wakati tayari wanajishughulisha na uuzaji au kutoa huduma zenye thamani kubwa, bali wanaipa heshima kubwa fedha.

Wanaamini kwamba utajiri walionao au uwekezaji mkubwa walioufanya visingeweza kufanikiwa ikiwa wasingeweza kuvuna kiasi kidogo cha fedha kutoka kwa mtu mmoja mmoja

Sifa nyingine ya tajiri ni kuheshimu na kuipa thamani kubwa njia au mbinu aliyotumia kupatia utajiri na mali zake.

Kama utajiri ulimjia kwa kufanya biashara ya chakula, ni lazima aendelee kujihusisha nayo hata ikitokea amebuni aina nyingine za biashara kwa ajili ya kuendeleza mapato yake.

Lakini pamoja na hizo, tajiri pia ana sifa ya kutoridhika na kila wakati anafikiria kupata fedha na mali nyingi zaidi ya zile alizonazo kwa wakati huo. Unapoona tajiri anabuni miradi na mingi zaidi ya ile aliyonayo, fahamu kwamba analenga kuongeza kiasi cha fedha kwenye akaunti yake na sio vinginevyo.

Ikiwa mtu hana tabia au sifa hizo zilizoorodheshwa hapo juu, ni wazi kwamba hana roho na akili ya kitajiri na badala yake mawazo na fikra zake ni za kimasikini.

Siku zote masikini hana heshima kwa pesa na ndio maana anaweza kuidharau na kuacha kabisa kazi ambayo inampatia mshahara wa Sh500,000 kwa sababu tu ameshinda bahati nasibu ya Sh100 milioni au amepata kiasi fulani kikubwa cha fedha baada ya kuuza kiwanja au nyumba.

Kinyume na tajiri, mtu mwenye akili za kimasikini pia huwa hathamini njia ambayo imempatia fedha ingawa pia ni nadra kuona mtu mwenye roho ya namna hiyo anawaza kufanikiwa zaidi ya pale alipofikia.

Baada ya Yanga kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, nimeshtuka kusikia kauli kutoka kwa baadhi ya wanachama na mashabiki wake kwamba hawana mpango na Sh80 milioni ambazo timu inayotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara hupewa kwa sababu timu yao imejihakikishia kupata kitita cha zaidi ya Sh 600 milioni kutoka kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

CAF hutoa fedha hizo kama mgawo kwa timu zinazofanikiwa kufuzu hatua ya makundi ya mashindano hayo ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Inawezekana wanazungumzia suala hilo kwa utani ili kuwakejeli watani wao wa jadi, Simba lakini kama kweli hoja hiyo inatoka moyoni, nadhani Yanga inapaswa kuomba Mungu roho hiyo isiote mizizi katika kipindi hiki ambacho Ligi Kuu inaelekea ukingoni.

Unapozidharau Sh 80 milioni kisa umepata Sh 600 milioni, maana yake umejisahaulisha kwamba usingeweza kushiriki mashindano hayo yaliyokupatia Sh 600 milioni kama ungeshindwa kutwaa ubingwa ambao unakupatia kiasi kidogo cha fedha.

Kuamini kwamba kwa kuwa umepata Sh600 hupaswi tena kuzitolea macho Sh80 milioni, unajaribu kutuaminisha kwamba unaamini fedha hizo ambazo CAF hutoa, zitamaliza matatizo ya Yanga hata isiposhiriki mashindano ya kimataifa mwakani jambo ambalo sio kweli.

Lakini pia unajaribu kutengeneza picha kwamba kwa Yanga kutinga hatua ya makundi, ni mafanikio makubwa ambayo yanaifanya timu hiyo isitumie tena nguvu ya kufika mbali zaidi ya hapo.

Bila shaka uongozi, benchi la ufundi pamoja na wachezaji wa Yanga hawatoingia katika akili na mawazo hayo mgando ya kudharau ligi ya ndani kwa sababu tu wamefanikiwa kuvuna kiasi cha Sh600 milioni kutoka CAF.

Ni mawazo yanayoonyesha uduni wa fikra ambayo hayapaswi kuungwa mkono na kupewa kipaumbele kwenye klabu kubwa na kongwe kama Yanga ambayo ina umri wa zaidi ya miaka 80 tangu ilipoanzishwa mwaka 1935.

Yanga inatakiwa iendeshwe kwa mtazamo wa kitajiri, ule wa kuthamini kiwango chochote cha fedha, kuheshimu njia waliyotumia kupatia mafanikio lakini pia kuwaza kufika mbali zaidi ya walipo sasa.

Akili hii ya kuwaza kwamba Sh80 milioni za ubingwa wa Ligi Kuu hazina thamani tena kisa timu imevuna Sh 600 milioni.